Kikosi cha Cosmopolitan, mabingwa wa soka Tanzania mwaka 1967. Kushoto anaonekana kocha wa timu hiyo Mansour Magram.
NA DANIEL MBEGA
LIGI Kuu ya soka Tanzania Bara kwa
msimu wa 2014/2015 imehitimishwa rasmi Jumamosi Mei 9, 2015 kwa michezo saba
iliyotimiza jumla ya mechi 182, huku mabao 15 yakifungwa siku ya mwisho na
kufanya jumla ya mabao 346 kwa msimu mzima, ukiwa ni wastani wa mabao 1.9 kwa
kila mechi.
Kwa kuangalia katika kumbukumbu za
utafiti wangu, hadi kufikia jioni ya Jumamosi Mei 9, 2015, jumla ya mechi 6,068
zilikuwa zimechezwa katika harakati za kusaka ubingwa wa Tanzania tangu Ligi ya
Taifa ilipoanza mwaka 1965.
Mechi hizo zilizaa jumla ya mabao 10,838,
huku mabao mengine yakiwa yamepatikana kwa njia ya matuta, hasa katika kipindi
cha 1965 hadi 1976 ambapo Ligi ya Taifa ilikuwa inaendeshwa kwa mtindo wa
mtoano.
Mfumo halisi wa Ligi yenye kutoa
pointi kwa kila mechi ulianza mwaka 1977 na ulianzishwa na mkimbiaji wa zamani
wa Tanzania, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini (FAT),
Chabanga Hassan Dyamwale, ambapo mshindi alikuwa akipata pointi mbili wakati
timu zilipotoka sare ziligawana pointi moja moja.
Mfumo huo wa kutoa pointi mbili kwa
mshindi ulibadilika mwaka 1994/95 ambapo sasa timu zilizoshinda zikaanza kupewa
pointi tatu. Hii ilitokana na mabadiliko ya Sheria za Soka za Kimataifa ikiwa
ni katika kuzipa hamasa timu zifanye vizuri zaidi uwanjani kwa ushindani.
Huwezi kuamini nikisema kwamba,
mpaka sasa hakuna hata timu moja ambayo imewahi kuwepo kwenye Ligi miaka yote
tangu mashindano hayo ya kusaka bingwa yalipoanzishwa. Hakuna hata moja.
Miamba ya soka Tanzania, Simba na
Yanga, ingawa ndiyo iliyocheza mechi zaidi, haijapata kushiriki mashindano hayo
katika nyakati fulani hasa kwenye miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Kwa mfano; mwaka 1967 Simba
(Sunderland wakati huo) na Yanga zilijitoa kwenye Ligi kwa sababu mbalimbali.
Mwaka 1970 na 1971 Simba haikufuzu kwa hatua ya mwisho ya Ligi hiyo baada ya
kushindwa kwenye Ligi ya Mkoa wa Pwani. Ikumbukwe kwamba, wakati huo
kuliendeshwa mashindano ya mikoa na mabingwa wa mikoa hiyo ndio waliofuzu kwa
ngazi ya Taifa.
Hata mwaka 1975 wakati Mseto
ilipotwaa ubingwa, ikiwa klabu ya kwanza kupeleka taji hilo nje ya Dar es Salaam,
Simba haikuwemo baada ya kushindwa kufurukuta kwenye Ligi ya Mkoa wa Pwani.
Lakini pamoja na Yanga kushiriki, haikuweza kutetea ubingwa wake baada ya
kushuhudia fainali ikizikutanisha timu zote za mikoani, Mseto ya Morogoro na
Nyota Mtwara.
Dondoo:
- Bao la kwanza
kabisa la Ligi ya Taifa lilifungwa Juni 5, 1965 katika mechi ambayo Manchester
United ya Tanga iliifunga Sunderland pia ya Tanga 1-0.
- Mchezaji Martin wa
Coop United ndiye wa kwanza kufunga mabao matatu ‘hat trick’ kwenye Ligi.
Alifunga mabao matatu katika ushindi wa timu yake wa mabao 5-1 dhidi ya African
Sports Desemba Mosi, 1967.
- Kitwana Ramadhan
Manara ‘Popat’ ndiye mchezaji wa kwanza kubadilisha namba na kung’ara zaidi
uwanjani. Alikuwa kipa wa Cosmopolitan na Taifa Stars hadi mwaka 1965 alipoamua
kuhamia kwenye ushambuliaji na kuwa mwiba kwa ngome za wapinzani.
- Mseto iliwahi kutoa
kipigo cha mbwa mwizi kwa mahasimu wao Nyota Afrika ya Mtwara baada ya kuifunga
mabao 15-2 kwenye mechi ya Ligi ya Taifa ngazi ya Kanda. Hii ilikuwa Mei 22,
1977 ambapo mabao ya Mseto yalifungwa na Edward Hiza, Hassan Shilingi (mawili), Juma Mensah, Haji
(manne), Ahmad Omar, Kassam (manne), na Vincent Mkude (mawili). Mabao ya Nyota
Afrika yalifungwa na Mkenda na Joseph.
- Kwa mara ya
kwanza masuala ya soka kwenda mahakamani ilikuwa mwaka 1982 wakati Simba ilipoweka
pingamizi kuzuia mechi za Ligi ya Taifa zisiendelee mpaka rufani yake kuhusu
usajili ijadiliwe. Mechi zilisimama, lakini baadaye zikaendelea baada ya Simba ‘kupigiwa
magoti’ na kufuta pingamizi hilo.
- Yanga iliwahi
kutumia dakika 88 kukomboa bao bila mafanikio. Hii ilikuwa Mei 26, 1990 wakati
bao la Mavumbi Omar la meta 40 katika dakika ya pili lilipoweza kuipa ushindi
Simba.
- Neno ‘Uteja’
lilianza kutumiwa zaidi kwenye soka mwaka 1990 na mashabiki wa klabu za Coastal
Union na African Sports za Tanga wakimaanisha Simba na Yanga walikuwa wateja
wao kwa sababu timu hizo kila zilipotia pua Mkwakwani zilipata kipigo.
- LĂ©opold ‘Tussle’
Mukebezi na Mecky Maxime ndio wachezaji pekee walioweza kudumu katika klabu
moja maisha yao yote ya soka. Mukebezi alichezea Balimi ya Bukoba miaka ya 1970
hadi mwanzoni mwa 1980, wakati Maxime aliichezea Mtibwa Sugar hadi alipostaafu
2010.
Fuatilia www.brotherdanny.com
kila siku kwa dondoo mbalimbali za michezo
-------------------------------
No comments:
Post a Comment