Lowassa wakati akiwa Waziri Mkuu.
Picha mbalimbali zinazomuonyesha Lowassa akiongea na makundi mbalimbali ya wafuasi.
Na Daniel Mbega
“MKAKATI wasukwa kuwaondoa Lowassa na Membe urais 2015”, “CCM
yamtolea uvivu Lowassa urais 2015”, “Mkakati wa kumfukuza Lowassa CCM waiva”,
“CCM yamuonya tena Lowassa”, “CCM haitaruhusu wanunua urais 2015”.
Naam. Hivi ni baadhi tu ya vichwa vya habari ambavyo
kwa miaka takriban mitano sasa vimekuwa vikipamba magazeti na mitandao ya
kijamii kuhusu harakati za muda mrefu za Chama cha Mapinduzi (CCM) ‘kumzuia’
Mbunge wa Monduli na waziri mkuu mstaafu, Edward Ngoyayi Lowassa, asiwanie
urais mwaka 2015 kupitia chama hicho.
Na katika kipindi hiki ambapo kasi ya
kujipanga kwa kuwania kuteuliwa imepamba moto, siyo ajabu kuona maandiko mengi
yakimponda kada huyo wa CCM na kumkatisha tamaa kabisa asitie mguu kwenye
kinyang’anyiro hicho.
Yawezekana CCM – au baadhi ya watu ndani ya
CCM – wana sababu zao za kumwekea kauzibe Lowassa, lakini binafsi naamini kuna
mkorogano ndani ya chama hicho, mkorogano ambao hauna tofauti na mwaka 1995 na
hata 2005.
Tungekuwa kwenye michezo, tungesema ‘Kombe
liko wazi’, lakini kwa sasa tunasema kiti cha urais kitakuwa wazi baada ya Rais
Jakaya Kikwete kumaliza muda wake Oktoba 2015.
Waliozuiwa na mkwara wa kifo wa Sheikh Yahya
Hussein mwaka 2010, sasa wamenyoosha makucha yao, lakini wanafanya kila namna
kuwazibia wengine na zaidi inaonekana vita ya vigogo wa CCM wengi imehamia kwa
Lowassa.
Mwenzenu mpaka nashangaa. Kwani Lowassa
ametenda dhambi gani kubwa kiasi cha CCM kumchukia? Hivi ana damu ya kunguni au
nyota ya Punda?
Yeye mwenyewe amekaririwa akisema: “Natazamwa na CCM kila kona!” Yaani
kila anachokifanya, CCM lazima waseme, wamwekee vikwazo, wazushe kashfa na
mambo mengine kadha wa kadha.
Lowassa ana fedha za kutosha. Hilo halina
ubishi. Lakini fedha hizi zisiwe chanzo cha kuleta chokochoko na vikwazo kwake
kugombea.
Maswali ya namna gani alivyozipata – kwa
kisingizio cha hoja ya Mwalimu Julius Nyerere – kwa sasa hayana msingi sana
hasa inapotokea kwamba hakuna mtu yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma za ufisadi
dhidi yake.
Wapo baadhi ya watu wanaotaka kuuaminisha umma
wa Watanzania kwamba Lowassa ni fisadi wa kutupa, kwamba anatumia fedha kununua
‘upendo’ kwa wananchi wa kada zote na mambo kadha wa kadha.
Mbona hawawawekei vikwazo wale waliotajwa
kwenye orodha ya ukwapuaji wa fedha za Akaunti ya EPA na hata Escrow?
Wanawaogopa?
Kuna mambo mawili kwa Lowassa. Anakubalika kwa
sababu alijijengea msingi muda mrefu na mikakati yake ni ile yenye kuzaa
matunda. Halafu pili, amekuwa karibu na wananchi na ndiyo maana makundi yote ya
kijamii yanamuunga mkono kiasi kwamba amekuwa kimbunga ndani ya CCM.
Haikunishangaza wakati yeye mwenyewe
alipotamka kwamba ‘Huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono’. Ndiyo. Huwezi kuzuia
nguvu ya umma kwa sababu hivi sasa kila kona unayopita habari ya mjini ni
Lowassa kuwa rais!
Vyombo vya habari vyenyewe vimeandika sana
kuhusu kukubalika kwa Lowassa na wananchi, hata kama ndani ya CCM hawamtaki.
Miongoni mwa vichwa vya habari ni hivi: “Lowassa atikisa urais 2015”, “Kumbe Lowassa
ni tishio CCM”, “Lowassa aongoza urais”, “Lowassa amtesa Kikwete”, “CCM hoi kwa
Lowassa... sasa Lowassa ana nguvu kuliko chama”, “Moto wa Lowassa sasa
waitikisa CCM” na vingine kadha wa kadha.
Binafsi naamini kitu kimoja ambacho kiko
dhahiri kwa wanaompinga Lowassa: wanaogopa kuumbuliwa kutokana na madudu
wanayoyafanya.
Viongozi wengi wa serikali ni wazembe, na
uzembe ni adui namba moja wa Lowassa, kama ilivyokuwa kwa Mbunge wa zamani wa
Monduli, wajina wake Edward Moringe Sokoine.
Nchi hii kwa mahali tulipofikia, tunahitaji
tupate kiongozi dikteta kidogo na mwanadiplomasia kidogo – sifa alizonazo
Lowassa.
Tunataka kiongozi ambaye atakuwa na uamuzi
mgumu, asiyelea uozo na anayeweza kuweka vipaumbele na kuvisimamia.
Jenerali Idi Amini Dada alikuwa dikteta, wengi
tunamchukia kwa matendo yake yasiyo ya kibinadamu, lakini mimi nampenda kwa
kitu kimoja tu: alikuwa halei uozo. Alipata kusema: “Wewe ni waziri, una mamlaka, ofisa wako wa chini anavurunda halafu
unasubiri mpaka Jenerali Amini aje amwajibishe. Basi hufai hata kushika nafasi
hiyo!”
Naam. Lowassa anaweza kuondoa ombwe hili la
uzembe na kuwanyorosha wale wanaodhani ni miungu-watu hata pale wanaposhindwa
kutimiza majukumu yao ipasavyo. Anaweza, si tumeona katika kipindi alichokaa
kwenye uwaziri mkuu?!
Tupo kwenye umaskini mkubwa, watu wanateseka bila
sababu ya msingi. Vijana wanashabikia tu kama wehu, wengine ni wasomi lakini wanapelekwa
kama upepo, wakisikia hiki "hewala", wakisikia kile "sawa",
wakiambiwa hivi "alhamdulilah", wakiambiwa kile "poa tu".
Hawataki kuchambua na kuielewa siasa kwamba kwenye siasa kuna majungu, fitna, kuchongeana,
uchu wa madaraka na mali na mambo mengi.
Sina haja ya kuyataja aliyoyafanya Lowassa
katika kipindi chake cha miaka miwili na mwezi mmoja na siku nane alichokaa
pale Magogoni, lakini kwa kifupi tu ni kwamba, yeye si mtu wa kupoteza mwelekeo
na anasimamia kile anachokiamini. Halafu siyo kigeugeu na siyo mvivu.
CCM inayafahamu yote haya na imekuwa ikifanya kila jitihada
kuhakikisha inakwamisha harakati zake. Watu wameibuka na sababu kadha wa kadha
kama Lowassa ni fisadi; ana utajiri mkubwa, sijui alikataliwa na Mwalimu
Nyerere na kadhalika. Msimsingizie Mwalimu Nyerere kuhalalisha fitna zenu
bwana.
Sasa wameibuka na hoja nyingine ambayo kwayo naona ni ya
unyanyapaa mkubwa. Eti Lowassa ni mgonjwa na hivyo hastahili kuchaguliwa.
Hapa ndugu zangu mnamkosea Mungu. Hivi mmesahau ule wimbo wa
Selemani Kungubaya wa Salamu za Wagonjwa? Anaimba hivi: “Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima kuwa mfu,
mgonjwa kuwa salama…”
Naamini uzima wa mtu anayeujua ni Mungu. Leo hii mnaomsema
kwamba anaumwa, kesho mnaweza kutangulia mbele za haki mkamwacha anadunda na
afya njema kabisa.
Kwa hakika, CCM msifanye makosa kwa chuki zenu kumtema
Lowassa katika kinyang’anyiro hiki. Mwacheni apite kwenye vikao vyote na
wanachama waamue wenyewe.
Wanafunzi, viongozi wa dini na makundi mbalimbali
yanayojitokeza kumuunga mkono hayajakosea.
Mkifanya makosa ya kumtema, hakika mtawafuata ZAPU na
wengineo.
Kazi yangu kusema, ni haki yangu ya Kikatiba.
Wasalaam.
0656-331974
Makala hii ni kwa hisani ya gazeti la WAJIBIKA la Mei 25, 2015
No comments:
Post a Comment