Rais Kikwete (kulia) akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya walipokutana nchini Afrika Kusini.
Mheshimiwa Rais,
Nimesikiliza hotuba yako Bungeni kuhusu msimamo wa Tanzania
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ilikuwa nzuri na uliondoa shaka iliyokuwa
imetanda miongoni mwa Watanzania na hata wale waliodhani pengine utawakashfu
ama kuwalalamikia marais wenzako ndani ya EAC ambao wanakutenga.
Pamoja na ukweli kwamba binafsi sikuitegemea, lakini nimeridhika kwa kiasi kikubwa. Nilitegemea ungezungumzia kuhusu Operesheni ya Kuzuia Ujangili ambayo wabunge wameizuia (pengine kwa hofu kwamba kwa hatua ilipofikia, wale waliokamatwa wanaweza kuwataja miongoni mwao wanaojihusisha upopoaji wa tembo na wanyama wengine kwa maslahi yao).
Pamoja na ukweli kwamba binafsi sikuitegemea, lakini nimeridhika kwa kiasi kikubwa. Nilitegemea ungezungumzia kuhusu Operesheni ya Kuzuia Ujangili ambayo wabunge wameizuia (pengine kwa hofu kwamba kwa hatua ilipofikia, wale waliokamatwa wanaweza kuwataja miongoni mwao wanaojihusisha upopoaji wa tembo na wanyama wengine kwa maslahi yao).
Wakati mwingine ukiona wabunge
wetu – ambao tumewazowea – wanalivalia njuga jambo fulani, inabidi ujiulize mara
mbili mbili kwamba kuna kitu wanachokikusudia, siyo bure. Sitaki kulizungumzia
hili kwa sababu hata mwenyewe unakumbuka wakati ule walipoleta kwako hoja ya
posho ili usaini – ukala jiwe.
Nilitegemea utazungumzia kuhusu Katiba Mpya pamoja Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, lakini haya yote – kama ulivyosema mwenyewe kwenye
utangulizi wako – hayakuwemo kwenye hotuba yako.
Badala yake ukazungumzia mambo manne tu – suala la ardhi,
uhamiaji, ajira pamoja na sarafu moja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba
ndio msimamo wetu, lazima Watanzania wapewe kipaumbele na tusiruhusu maeneo
hayo yakaingia kwenye jumuiya, tutakwisha kabisa. Masuala haya hata Mtanzania
anayeishi kule nyumbani Kibaigwa anayajua!
Lakini ulipotoa msimamo kwamba Tanzania haikusudii kujitoa
kwenye EAC hata kama akina Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni na Paulo Kagame
wataendelea kukutenga katika vikao vyao, nilifarijika. Nikakumbuka kwamba hawa
jamaa, au niseme hizi nchi – hasa Kenya na Uganda – ndizo zinaelekea kuwa
chanzo cha kuvunjika kwa Jumuiya ile ya kwanza mwaka 1977.
Kuna kitu ambacho kwa upeo wa akili yangu nimekiona
kufuatana na huu msimamo wa hawa jamaa. Yoweri Kaguta Museveni wakati akipigana
msituni hadi kuingia madarakani mwaka 1986 alikuwa akiungwa mkono na Mataifa ya
Magharibi, hasa Marekani. Yeye ndiye alikuwa ‘mtu wao’ katika ukanda huu kwa
ajili ya kulinda maslahi yao.
Baadaye alipokuja Meja Paulo Kagame, jasusi ambaye
alisaidiwa na Tanzania kwa mafunzo kama tunavyosikia, Marekani ikamuunga mkono
hasa baada ya mauaji ya Juvenal Habyarimana na Cyprien Ntyaramira mwaka 1994
yaliyofuatiwa na mauaji ya kimbari. Mpaka sasa hakuna anayetaka kuzungumza wala
kunyoosha kidole kwa yeyote aliyehusika na njama za kuilipua ndege ya Rais
Habyarimana. Hakuna.
Kwa miaka yote hiyo ameungwa mkono na Marekani (iwe kwa siri
au hadharani), lakini kitendo chake cha kuendelea kuwaunga mkono waasi katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kimeonyesha kuwakasirisha Marekani na mataifa
mengine ya Magharibi ambayo yanamuona amekuwa mwiba. Ugomvi uliopo ni mawe
yaliyoko kwenye ardhi ya Congo.
Upepo ukabadilika tena mwaka 2008 wakati Marekani
ilipoichagua Kenya (chini ya Emilio Mwai Kibaki) kuwa ndiyo ngome ya vikosi
vyake vya kijeshi vya AFRISOM na AFRICOM kupambana na magaidi wa Al-Shabaab na
kurahisisha kusaidia majeshi ya UM katika migogoro inayoendelea Afrika. Kagame akawa
rafiki wa zamani wa Marekani.
Marekani wakawa na uhakika kwamba kama Raila Odinga
angeshinda Urais Kenya, basi maslahi yao yangeweza kuendelea kulindwa. Pamoja na
udhaifu wake alionao, lakini Marekani iliamini Odinga angeweza kuwa bora zaidi
ya Kenyatta, ambaye mpaka sasa hivi inaonekana hawamkubali huku akiwa na kesi
katika Mahakama ya Kimataifa huko The Hague.
Bahati mbaya zaidi, George Walker Bush alionekana kujiandaa
kutafuta swahiba mwingine kwenye ukanda huu. Akakuona wewe – kwa maana ya
Tanzania – kuwa unafaa kwa kuwa hufungamani na upande wowote. Akaja na kufanya
ziara ya siku nne, ikiwa ni ziara ndefu zaidi kwa Rais wa Marekani katika nchi
za Kiafrika.
Alipochaguliwa Obama mwaka 2008 na hata mwaka 2012, Wakenya
walikuwa na matumaini makubwa kwamba Marekani ‘haitapindua’ kwa lolote kwa kuwa
Obama ni Mjaluo wa Kisumu. Walidhani pamoja na kuwa mkuu wa Ikulu ya Marekani,
bado angeweza kutoa hisani kwa nchi yake ya asili. Kinyume chake, Obama
anaongoza kwa kufuata Katiba na Sera za Marekani.
Alipopanga ya ziara ya Afrika kwa mara ya pili, Wakenya
waliamini angekwenda kwao. Lakini angekwendaje wakati Uhuru anatuhumiwa kwa
machafuko yaliyosababisha mauaji? Marekani haiamini kama Uhuru hana hatia,
pengine mpaka hukumu itakapotolewa.
Badala yake, akakumbuka kwamba mwenzake Bush aliacha swahiba
huku, hivyo akaamua kuja Tanzania. Jamaa walipiga kelele weee wakidhani
utaratibu huo ungebadilisha, waliposhindwa kushawishi, wakaamua kususia kuja
Dar es Salaam wakati Obama alipotua.
Sasa kinachoonekana hapa ni kwamba, wanakuonea gere tu wewe
kuwa rafiki wa Marekani. Kuanzia Museveni, Kagame na Kenyatta ambao wanahisi
kwamba umewazibia fursa zao kwa taifa hilo kubwa duniani.
Kama zipo sababu nyingine ambazo mimi na Watanzania wenzangu
hatuzijui, labda, lakini kwa uelewa wangu, nadhani chuki zao dhidi yako ni gere
tu, hakuna kingine zaidi.
Mheshimiwa Rais, mimi nakushauri chapa kazi, wacha waseme
weee, watachoka. Watakufa navyo vijiba vya roho.
Wasalaam.
No comments:
Post a Comment