Na Daniel Mbega
Ndugu zangu,
Kwanza kabisa niwieni radhi kwa kushindwa kuendelea na
simulizi yetu ya kufutilia Nyayo za Chifu Mkwawa kwa siku kadhaa. Hii imetokana
na sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wangu.
Hata hivyo, karibuni tuendelee na simulizi yetu.
Tuliona jinsi Chifu Mkwawa alivyoirejesha himaya mikononi mwake kutoka kwa Mwambambe Mwalunyungu. Kadhalika tuliona Wajerumani walivyoingia Tanganyika na kuanza kuwashambulia watawala wa jadi kama Abushiri wa Pangani na sasa walikuwa wanaelekea Bara, wakipanga kwenda kupambana na Chifu Mkwawa wa Uhehe.
Tuliona jinsi Chifu Mkwawa alivyoirejesha himaya mikononi mwake kutoka kwa Mwambambe Mwalunyungu. Kadhalika tuliona Wajerumani walivyoingia Tanganyika na kuanza kuwashambulia watawala wa jadi kama Abushiri wa Pangani na sasa walikuwa wanaelekea Bara, wakipanga kwenda kupambana na Chifu Mkwawa wa Uhehe.
Vikosi hivyo, chini ya von Zelewiski, viliondoka Kilwa Julai
22, 1891 vikipitia himaya ya Ngoni Mafiti kuelekea Kisaki hadi Myombo karibu na
Kilosa, ambapo viliwasili Lugalo Agosti 16, 1891. Huko njiani vikosi hivyo vilikuwa
vimeteketeza vijiji kadhaa na havikukutana na upinzani mkali. Walikuwa
wamewaona Wahehe wenye silaha njiani, lakini walikimbia baada ya kuwafyatulia
risasi. Hali hiyo inaonekana ndiyo iliyompa ujasiri von Zelewiski wa kusonga
mbele akiamini kwamba Wahehe wangelazimishwa kusalimu amri.
Jeshi la Mkwawa
Mtwa Mpangile, mdogo wake Chifu Mkwawa, ndiye aliyekuwa
kamanda wa jeshi la Wahehe. Ndiye aliyeongoza jeshi hilo katika vita vya
Lugalo. Kama ilivyokuwa kwa wapiganaji wote wa Kihehe, Mpangile alikuwa na
uzoefu mkubwa wa vita ingawa ni vite dhidi ya makabila mengine, lakini siyo kwa
jeshi imara lenye mbinu kama la Wazungu.
Tofauti na makabila mengine ya Kiafrika ambayo machifu wao
ndio waliokuwa mstari wa mbele, Wahehe walikuwa na mbinu kama za Wazungu kwa
kumwacha chifu wao nyuma akiamuru namna ya kushambulia.
Jeshi la Wahehe kwenye vita vya Lugalo lilikuwa na
wapiganaji 3,000. Ndilo lililokuwa imara zaidi kulinganisha na makabila mengine
yote yaliyolizunguka.
Ushindi dhidi ya makabila mengine ya jirani ulikuwa umewapa
ujasiri mkubwa na uzoefu wa vita na kwa hakika walikuwa wamejitolea kuhakikisha
wanapambana kufa au kupona kuhakikisha wanailinda nchi yao dhidi ya wavamizi wa
kigeni.
Wengi kati ya wapiganaji wa Kihehe walikuwa na mikuki na
ngao zilizotengenezwa kwa ngozi kama zile zilizokuwa zikitumiwa na Wazulu.
Wengine walikuwa na mashoka.
Chifu Mkwawa alikuwa anafahamu kwamba majeshi ya Wajerumani
yalikuwa yanakuja kwenye himaya yake. Taarifa zilikuwa zimemfikia mapema mno na
kuifahamu mikakati yao yote. Vijana wake mashujaa waliviona vikosi vya
Wajerumani wakati vikikaribia Uhehe na kupeleka taarifa za uwezo wa jeshi hilo
la Wazungu, hivyo alikuwa amejiandaa kuwakabili.
Tutaendelea…
No comments:
Post a Comment