Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 18 November 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (3)

Eneo la makaburi alimozikwa Chifu Munyigumba na baadhi ya wanafamilia ambalo limezungushiwa uzio. Hapa panahitajika kuwa sehemu ya Makumbusho ya Taifa, ni urithi wetu - Mali Kale.

Na Daniel Mbega

Utawala wa Munyigumba Kilonge Mwamuyinga ulidumu kwa muda wa miaka 19 tangu alipomuua kaka yake Ngawonalupembe mwaka 1860.
Mtwa Munyigumba alifariki mwaka 1879 katika Kijiji cha Rungemba akiwa amefanikiwa kuziunganisha koo zaidi ya 100 ambazo baadaye ndizo zilizozaa kabila la Wahehe. Wakati Munyigumba anafariki, Mtwa Mkwawa, ambaye ni mtoto wake wa kwanza wa kiume, alikuwa na umri wa miaka 24. Lakini tayari alikuwa amepigana vita nyingi dhidi ya Wabena, Wasangu na Wangoni kiasi cha kupewa jina la Mkwavinyika na akawa Chifu Mdogo katika eneo la Kalenga.
Kutokana na umri mdogo wa Mkwawa, ikabidi asikabidhiwe kwanza uchifu wa kabila lote kwa wakati huo, hivyo ukoo ukamteua mdogo wake Munyigumba, Mtwa Mhalwike, aliyezaliwa na mke wa tatu wa Mtwa Kilonge, Mama Sekindole.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya Mtwa Munyigumba kufariki na kutawazwa kwa Mhalwike, utawala huo ukapinduliwa na mmoja wa wafuasi wake na pia mkwewe aliyekuwa amemuoa binti yake Kilemaganga (mtanisahihisha nikikosea, kwa sababu haya ndiyo niliyoyapata kwa sasa katika utafiti wangu).
Mtu huyo, Mwambambe Mwalunyungu aliyekuwa na asili ya Unyamwezi, alikuwa anatokea eneo la Wassa na enzi za utawala wa Munyigumba ndiye hasa alikuwa akitumwa kazi ndogo ndogo kiasi cha kupendwa na hatimaye akapewa binti wa Chifu.
Ukoo wa Mwambambe bado ungalipo na kwa mujibu wa mahojiano niliyoyafanya na mmoja wa vitukuu wa Malangalila Gamoto, Mheshimiwa Joseph Mungai mjini Iringa mwaka huu, mmoja wa vitukuu wa Mwambambe aitwaye Gideon Mtaki anaishi Dodoma na ninakumbuka aliwahi kuwa Mbunge wangu katika Jimbo la Mpwapwa kati ya mwaka 1985 hadi 1990 wakati nikiishi huko.
“Huyu Mwambambe aliwaza moyoni mwake, kwa nini mdogo wake Munyigumba atawale? Nchi hii nitaichukua mimi mwenyewe,” anasimulia Malugala Mwamuyinga, mjukuu wa Msengele Kilekamagana, ambaye ni mdogo wake Mkwawa.
Mwamuyinga anasema, Mwambambe alimvia Mhalwike kichakani, akampiga na kumchinja katika eneo hilo la Rungemba, jirani kabisa na yalipo makaburi ya ukoo. Alipomaliza kazi yake hiyo haramu akaenda mahali ambako watu walikuwa wanakunywa pombe na kusema: “Nchi hii ni yangu. Kama mnabisha nendeni kule kwenye miti mkamtazame Mhalwike.” Walipokwenda huko wakakuta maiti ya Mhalwike ikiwa imechinjwa kama kuku.
Kama nilivyoeleza, wakati huo Mtwa Mkwawa alikuwa bado mdogo sana kupewa madaraka ya kutawala nchi na kwa vile tayari Mwambambe alikuwa ameupindua utawala, wakahisi Mtwa Mkwawa angeweza kuuawa kwa sababu ndiye mtoto mkubwa wa kiume wa Munyigumba na ndiye hasa aliyetarajiwa kutawala. Hivyo, ikabidi wamkimbize kwenda kumficha Dodoma kwa Mtemi Mazengo wa Wagogo. Mtemi huyo wa Wagogo akawapa hifadhi katika eneo la sasa linalojulikana kama Kibakwe na maeneo ya jirani kama Mwanawota, Rudi na Chinyanghuku huku akipewa pia na binti wa kumuoa. Hii ndiyo sababu Wagogo wanawaita Wahehe wajomba zao na wanaheshimiana mno.

Tutaendelea…

No comments:

Post a Comment