Mti wenye miaka zaidi ya 100 katika eneo la Lundamatwe ambapo mganga wa jadi Ngondo Kimamula aliwatengenezea dawa wapiganaji wa Mkwawa kabla ya kumpiga Mwamubambe Mwalunyungu.
Eneo ambalo inaelezwa kwamba ndiko vichwa vta wapiganaji wa Mwambambe vililundikwa baada ya kuuawa na wapiganaji wa Chifu Mkwawa.
Makaburi ya ukoo wa Ngondo Kimamula Mbugi katika eneo la Lundamatwe.
Na Daniel Mbega
Ndugu zangu,
Tunaendelea na simulizi ya historia
ya kufuatilia ‘Nyayo za Chifu Mkwawa’. Tumeona jinsi ambavyo baada ya kifo cha
Chifu Munyigumba mkwewe Mwambambe Mwalunyungu alivyomuua baba yake mdogo Chifu
Mkwawa, Mtwa Mhalwike na yeye akajitangazia mtawala wa himaya ya Wahehe, ingawa
wakati huo walikuwa bado hawajaanza kuitwa ‘Wahehe’.
Tumeona pia namna wazee walivyoamua kumkimbiza Chifu Mkwawa na kumficha Dodoma (Idodomhya) kuepuka asije akauawa na Mwambambe.
Tumeona pia namna wazee walivyoamua kumkimbiza Chifu Mkwawa na kumficha Dodoma (Idodomhya) kuepuka asije akauawa na Mwambambe.
Kwa hiyo basi, baada ya Chifu Mkwawa
kukimbizwa, Wahehe hawakufurahishwa na utawala wa Mwambambe ambaye mpaka sasa anachukuliwa
kama adui mkubwa zaidi katika historia ya kabila hilo kuliko hata Wajerumani. Hivyo,
wakapanga mbinu za siri kumrejesha Mtwa Mkwawa kutoka uhamishoni.
Mtwa Mkwawa, wakati huo akiwa
amejifunza mbinu za juu za kivita kwa msaada wa Chifu wa Wagogo, akaamua
kurejea na kuunda jeshi lake ili kupambana na Mwambambe katika harakati za
kuurejesha utawala huo.
Hata hivyo, katika mapigano hayo, wapiganaji
wengi wa Mtwa Mkwawa waliuawa na Mwambambe, mtu ambaye anadaiwa kuwa alikuwa
akitumia zaidi mitishamba kushinda vita nyingi, dawa ambazo inaelezwa kwamba
ndizo alizokuwa anatumia ndizo zilizokuwa zikitumiwa na Mtwa Munyigumba na Mwambambe
mwenyewe ndiye aliyekuwa akielekezwa kuzitafuta porini.
Kutokana na wapiganaji wengi kuuawa
na Mwamubambe, wapiganaji wengine walikuwa wakilia na kupiga kelele; “Hee Hee
Hee! Mtwa tuisila!” wakimaanisha; “Hee Hee Hee! Mtwa tunakwisha!” Hapa hasa
ndipo lilipoanza jina la kabila la Wahehe kutokana na kelele walizokuwa
wakizipiga.
“Wafuasi wake walikuwa wanakufa sana. Siku moja Mkwawa
akajiwa kwenye ndoto na baba yake Munyigumba ambaye alimwambia kwamba hilo jitu
hawataliweza. Lilikuwa likichomwa mikuki linachomoa na kuwarushia wao na
kuwaua,” anasema Malugala Mwamuyinga.
Inaelezwa kwamba, Munyigumba alipomtokea Mkwawa kwenye ndoto
akamwambia, roho ya Mwamubambe iko kwenye kidole au kwenye kisigino. Hata
wakifanya namna gani hawawezi kumuua. Hivyo akamtaka amtafute Mkimayena Mwakinyaga
amwambie akamchome Mwambambe kwenye kisigino au kidole.
Lundamatwe
Mwambambe alikuwa na jeshi kubwa na
wafuasi wengi wenye uwezo wa vita, Mtwa Mkwawa akalazimika kujipanga upya ili
kuwapiga na kuyarejesha maeneo yote yaliyokuwa yametwaliwa na Mwambambe.
Mapambano makali kabisa ya Mkwawa na
wafuasi ya Mwambambe yaliianzia eneo ambalo leo hii linafahamika kama
Lundamatwe (Lundika Vichwa), lakini yapata kilometa mbili kutoka Barabara Kuu
ya Tanzam upande wa kusini.
Hapa palikuwa nyumbani kwa mganga
Ngondo Kimamula Mbugi, pembezoni mwa Mto Ruaha. Inaelezwa kwamba, mganga huyo
aliamua kuchukua jukumu la kuwaandaa wapiganaji wa Mkwawa kukabiliana na maadui
zake.
Wapiganaji wa Mkwawa baada ya
kuganguliwa wakaondoka kupambana na Mwambambe na wafuasi wake ambapo waliwapiga
na kuwaua zaidi ya wapiganaji 1,000.
Mwambambe alipona mambo yamemzidia
akatimua mbio, lakini wapoganaji wa Mkwawa wakaanza kumfukuza.
Kwa vile Mkwawa alikuwa ameelekezwa
na baba yake ndotoni kuhusiana na Mwambambe, akaamua kumtuma Mukimayena
Mwakinyaga, ambaye alikuwa mganga wa kienyeji, ili akamuue.
Mwakinyaga akaenda na kumkuta Mwambambe anakunywa pombe.
Mbele ya umati wa watu, akamchoma mkuki kwenye kidole. Mwambambe akadondoka
chini na kuanza kutapatapa bila kukata roho.
“Mwamubambe akamuuliza Mwakinyaga, ‘Umenifanya nini?’
Mwakinyaga akasema, ‘Aah ni mikuki tu’. Basi alipoona mambo yamekuwa magumu,
akamwambia; ‘Kaniitie Mkwawa aje’. Mkwawa alipofika Mwambambe akamwambia;
‘Wakorofi kama mimi wapo wengi ndani ya utawala wako, kwa hiyo sasa ukazane’.
“Kwenye ndoto, baba yake alikuwa amemwambia Mkwawa kwamba
akishafika aukite mkuki wake chini. Basi Mkwawa akaukita mkuki chini. Ndipo
Mwambambe akakata roho,” anaeleza Mwamuyinga.
Mwamuyinga anasema kwamba, kwa vile Mwambambe alikuwa
amewatesa na kuwaua Wahehe wengi, baada ya kufa ikabidi, kwa hasira, wananchi
wale wamkatekate vipande vipande na kuila nyama yake ili lisiwepo kabisa
kumbukumbu lake.
Baada ya hapo Mtwa Mkwawa akaendesha
mapambano ya kuyakomboa maeneo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa Munyigumba,
kampeni ambayo iliendelea moja baada ya nyingine kwa mafanikio makubwa kuliko
hata awali.
Tutaendelea…
No comments:
Post a Comment