Usanii wa Profesa Kapuya ni matusi
kwa Wanyanyembe
Toleo la 316
18 Sep 2013
MANAMBA ni binadamu, nguvu kazi ya
vijana waliokuwa wakitumikishwa kwenye kilimo cha mashamba makubwa ya mkonge na
hasa katika mikoa ya Morogoro na Tanga, enzi za wakoloni wa Kijerumani na
Mwingereza.
Manamba hao walitoka katika maeneo
mbalimbali nchini, lakini wengi kulingana na historia ya manamba, walitoka
mikoa ya magharibi mwa Tanzania - Tabora na Kigoma; mikoa ya kusini -
Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini - Iringa,
Mbeya na Rukwa.
Ukiacha manamba wa mkonge, mradi
mwingine mkubwa uliovuta manamba wengi kutoka maeneo hayo, ni ujenzi wa Reli ya
Kati, inayoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na matawi yake ya Kigoma na Mpanda.
Kwa wanaofahamu historia ya manamba
waliotumiwa na wakoloni hao wa Kijerumani na Kiingereza kama nguvu kazi yao ya
kulima mashamba ya mkonge na kuvuna, pamoja na kupasua miamba na kujenga reli
kutoka Dar es Salaam hadi maeneo hayo, wanatambua kwamba manamba waliotokea
njia ya Kigoma na Tabora, baadhi yao walitokea katika nchi za DR Congo, Burundi
na Rwanda.
Kama ambavyo wakoloni hao wakati
mwingine walilazimika kutumia nguvu kuwapata vijana wenye nguvu wa kwenda
kulima mashamba yao ya mkonge, ndivyo pia wakoloni hao walivyotumia nguvu
kuwasaka vijana wenye nguvu wa kwenda kushiriki ujenzi wa reli hiyo ya kati kwa
ujira mdogo mno ikilinganishwa ukubwa wa kazi walizozifanya.
Baada ya Uhuru wa iliyokuwa
Tanganyika, umanamba unaonekana kama udhalili. Siasa za wakati wa Uhuru
zimeugeuza umanamba kama utumwa. Lakini, kusema ukweli, umanamba katika mkonge
na ujenzi wa reli ya kati, enzi hizo, ilikuwa ni ufahari na ajira iliyowainua
wengi kiuchumi.
Mwanzoni mwa ukoloni huo, vijana hao
walilazimishwa kwenda kufanya kazi hizo. Lakini baadaye, baada ya jamii ya
vijana kuona tofauti ya kiuchumi kati ya vijana waliotoka kwenye umanamba na
waliobakia nyumbani na wazazi wao wakichunga ng’ombe na mifugo mingine, baadhi
ya vijana walitoroka majumbani, bila kuwaaga wazazi wao na kwenda kushiriki
kazi hizo.
Ilifika mahali ikawa ‘fasheni’
katika baadhi ya jamii zetu kwamba ili kijana aanze kujitegemea, kwa kuoa,
kuanzisha mji wake na kuwa na familia yake, ili aaminiwe na jamii anaweza
kujitegemea na kuitunza familia, kipimo cha uwezo huo kilikuwa kazi ya manamba.
Kijana alilazimika kwanza kufanya kazi za manamba ili apate fedha za kuanzia
maisha na kununulia mifugo!
Ujenzi wa reli ya kati na kilimo cha
mkonge, ndizo ajira kuu za uhakika zilizokuwapo enzi hizo kwa kijana wa
Tanganyika ambaye elimu kwake ilikuwa kitu cha anasa kutokana na sera za
wakoloni wote wawili hao. Enzi hizo, kazi za manamba hazikuwa kazi za kitumwa
kama ilivyokuja kuelezwa baadaye na wanasiasa wetu baada ya Uhuru, bali ndizo
kazi za mishahara zilizokuwepo!
Lakini kikubwa zaidi ya ajira, kazi
za manamba ndizo zilikuwa msingi wa kwanza uliowaunganisha na kuwaweka pamoja
vijana wa Kitanganyika katika kambi. Vijana wa Kitanganyika kutoka makabila
tofauti nchini, walikusanywa, kuchanganyika na kuishi pamoja kama ndugu kwenye
kambi za mkonge na ujenzi wa reli, wakichukua likizo kwenda makwao na kurejea
tena kwenye makambi hayo.
Ndiyo maana leo, ni rahisi kukuta
watu wa makabila mbalimbali ya Tanzania, na hasa ya Wangoni wa Songea, Waha wa
Kigoma, Wanyamwezi wa Tabora, Wahehe wa Iringa, Warundi na Wanyarwanda
walioingia manamba kupitia mikoa ya Kigoma na Kagera, wakiwa na kizazi chao
katika maeneo kadhaa ya mikoa ya Morogoro na Tanga kulikokuwa kukilimwa mkonge
kwa wingi.
Lakini pia kizazi cha manamba hao
kinaonekana leo katika miji mikubwa na midogo ambako njia ya reli ya kati
inapita. Kuna vijana na watu wazima walioamua kutorudi makwao na kuhamia maeneo
hayo moja kwa moja. Hao kwetu nyumbani tukiwaita ‘Abhalobhezi’
(Walowezi).
Kijiji cha Kaliua, kilichoko
wilayani Urambo, Tabora, kilikuwa ni kijiji kidogo tu, wakati Profesa Juma
Athuman Kapuya anazaliwa mwaka 1945. Kwa asili, Kaliua ni kijiji cha
Wanyamwezi, kabila kubwa linalopatikana katika Mkoa wa Tabora.
Kwa sasa, Kaliua ni mji mdogo katika
wilaya hiyo ya Urambo, na una mwingiliano wa watu kutoka makabila mbalimbali ya
Tanzania, waliohamia hapo kutokana na shughuli za kiuchumi, wakiwemo manamba
walowezi waliokuwa wakifanyakazi katika mashamba ya mpunga na tumbaku pamoja na
masalia ya manamba waliokuwa wakijenga reli ya kati inayopita katikati ya mji
huo mdogo.
Kiutawala, eneo la mji wa Kaliua kwa sasa liko Mkoa wa
Katavi. Kwa hiyo, Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, si Mnyamwezi
wa Tabora tena, bali ni Mnyamwezi wa Katavi. Ameungana na kabila la ndugu zao
Wapimbwe, kabila la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kaliua kuna idadi kubwa ya Waha
kutoka Kigoma. Kwa wasiofahamu tu, Muha wa Kigoma ni ama atakuwa Muha Mhutu au
Muha Mtutsi. Ni kama ilivyo kwa Mrundi au Mnyarwanda. Kila Mnyarwanda au Mrundi
ni ama atakuwa Mhutu au Mtutsi! Hao wapo hata Kagera. Wapo Wahaya wenye asili
ya Ututsi, Uhutu na au Unyankole.
Ningekuwa na uwezo wa kifedha wa
kutafiti kizazi cha Profesa Kapuya, Mnyamwezi wa Kaliua, bila shaka yoyote,
utafiti wangu ungenifikisha kwenye ukweli halisi kwamba kizazi cha Profesa
Kapuya kina mizizi Mkoa wa Kigoma au ng’ambo, na kwa hiyo Profesa Kapuya
mwenyewe ana damu ya ama Kihutu au Kitutsi!
Nafikia hitimisho hilo la utafiti
wangu huo kutokana na imani kwamba mtu akishaathiriwa na umanamba, akaathiriwa
na utumwa, inakuwa vigumu kwake kusimama peke yake. Hata ukimjazia vyakula vya
aina zote ndani, atakwenda kuomba tu chakula kama hicho hicho alichonacho ndani
kwake, kwa jirani.
Tukio la wiki iliyopita mjini
Tabora, limenikumbusha umanamba wetu, limedhihirisha taathira ya umanamba na
utumwa kwa baadhi ya jamii zetu. Kwamba kwa kuwa kiutawala sasa Profesa Kapuya
hawezi kuwa sehemu ya Wanyamwezi wa Tabora, na kwa kuwa Wanyamwezi wa sasa,
baada ya kizazi cha Mirambo na Isike kutoweka, hawawezi kujisimamia na kujitawala
wenyewe, mwanasiasa huyo na msomi huyo aliratibu na kusimamia hafla ya
kusimikwa kwa Chifu mpya na Mlezi mpya wa Wanyanyembe wote, Edward Lowassa.
Kwamba kwa hekima, busara na fikra
za Profesa Kapuya, Wanyamwezi wote kwa ujumla wao, wakiwemo kina Profesa
Ibrahimu Lipumba, Aden Lage, Samuel Sitta, Said Mkumba, Rostam Aziz na
wengineo, hawana sifa ya kuwa Machifu na Walezi bora wa Wanyanyembe, bali
wanahitaji Laigwanan wa Kimaasai kuwaongoza, Edward Lowassa.
Kumbe kwa Mnyamwezi, umanamba
haujaisha. Mnyamwezi bado ni mtu wa kubebeshwa mzigo mzito, na si yeye
kubebesha mtu! Kwa hakika kabisa, hili la profesa Kapuya kuwachagulia kiongozi
Wanyanyembe, ni usanii wa kisiasa, ni aibu na fedheha kubwa kwa yeyote
anayejiita Mnyamwezi!
Chanzo: www.raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment