Kaburi la Munyigumba lililopo Rungemba, Mufindi.
Daniel Mbega
UKITAJA mashujaa wa Afrika,
lazima pia umtaje kiongozi mkuu wa Wahehe, Chifu Mkwavinyika Munyigumba Kilonge
Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa. Huyu ana mambo mengi aliyoyafanya, ya
kujivunia, ambayo kizazi hiki hakifundishwi tena shuleni na hivyo historia yake
inapotea.
Nitajaribu kueleza kwa ufupi ufupi tu kile ambacho
nimekipata katika utafiti wangu wa historia mjini Iringa, lakini kwa vile bado
ninaendelea na utafiti huo, nakaribisha taarifa zozote kuhusiana na kiongozi
huyo shujaa.
Maandiko kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga ‘Mkwawa’, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.
Maandiko kadhaa yamekuwepo kuhusiana na historia ya Wahehe na hasa ukoo wa Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga ‘Mkwawa’, lakini yote hayo hayakunizuia kuisaka historia hiyo.
‘Jicho halishibi kuona na sikio halikinai kusikia!’ Hivyo
nikaamua kufunga safari hadi Rungemba, yaliko makaburi ya Mtwa Munyigumba na
ndugu wengine wa ukoo huo, yapata kilometa 62 kutoka Iringa mjini.
Wapo walioandika kwamba chimbuko la Mtwa Mkwawa ni Ungazija,
lakini simulizi ninazokutana nazo hapa ni tofauti, maana zinatoka katika vinywa
vya wanaukoo wa Muyinga, ambao nao wameipata ama kurithishwa kutoka kizazi na
kizazi kutokana na simulizi za mababu zao.
Wale waliopata kuandika kwamba asili ya akina Mkwawa ni
Ungazija wanaeleza kuwa mtawala wa Ngazija aliyeitwa Yusuf Hassan ambaye
alikuwa Mwarabu, alizaa watoto wawili wa kiume, Hassan ‘Mbunsungulu’ na Ahmad.
Wanasema kwamba Mufwimi alikuwa mmoja wa watoto watatu wa Mbunsungulu aliozaa
na mwanamke wa Kikaguru. Ndugu zake wengine walikuwa Ngulusavangi na Ngwila,
kwa maelezo yaliyo kwenye baadhi ya maandishi ambayo yanatoweka kutokana na
Watanzania kukosa utamaduni wa kutembea, kujifunza na kudadisi.
Rungemba ni kijiji ambacho hakijasikika sana katika historia
kama lilivyo jina la Mkwawa, lakini hapa ndipo kwa kiasi kikubwa lilipo
chimbuko la Chifu huyo wa kabila la Wahehe na ndipo lilipo kaburi la Mtwa
Munyigumba.
Ignas Pangiligosi Muyinga, maarufu kama Malugala Mwamuyinga
(62), ambaye ni kitukuu wa Msengele Kilekamagana, anaona fahari kuisimulia
historia ya ukoo huo maarufu.
“Shina la ukoo wetu linaanzia kwa mtu aliyeitwa Mufwimi
(yaani Mwindaji), ambaye mababu zetu walitusimulia kwamba alitokea Ethiopia,”
Malugala anaanza kueleza. “Mufwimi alipita akiwinda kutoka Ethiopia, Kenya
kabla ya kuingia Tanganyika na kujikuta yupo Usagara na hatimaye eneo la
Nguluhe-Dabaga akipitia Ikombagulu, himaya ya Chifu Mwamduda. Wengi
walimfananisha na mtu wa kabila la Wakamba kutoka Kenya kutokana na umbile lake
kubwa.”
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na
makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu,
Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe,
Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao waliishi Udzungwa, Kitelewasi na
Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi
wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya
sasa), Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya
Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mufwimi alikuwa mwindaji mkubwa wa nyati ambapo aliichoma
nyama yake kwa kuipaka chumvi ambayo ilikuwa haifahamiki kwa wakazi wa himaya
hiyo, alimpelekea zawadi ya nyama-choma Chifu Mwamduda aliyeipenda mno kwa
ladha yake.
Alipendwa na kukaribishwa na Mwamduda kuishi kwake, lakini
akaanzisha mapenzi ya siri na Semduda, binti wa Chifu huyo, ambaye alikuwa
amewakataa wachumba wengi. Binti huyo akapata ujauzito. Mufwimi akaogopa kwa
kuona amefanya kosa kubwa.
Tutaendelea nayo….
No comments:
Post a Comment