Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 8 November 2013

KIBANDA AFUNGUKA KUTESWA KWAKE

Absalom Kibanda akiwa hospitalini na mkewe Angela Semaya

Na Waandishi Wetu8 Novemba 2013
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari Cooperation (2006) na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda amezungumzia tukio la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa kwake lililotokea Machi mwaka huu.


Amesema amefanyiwa unyama huo kutokana na  majukumu yake ya kikazi akiwa kama Mhariri na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na sio masuala yake binafsi kama ambavyo inaelezwa na baadhi ya watu.
Kibanda aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kukabidhiwa Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Uandishi Uliotukuka ya Daud Mwangosi kwa mwaka wa 2013, ambayo imetolewa kwa mara ya kwanza na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC)  jijini Mwanza.
Alisema amekuwa kimya kwa muda mrefu ingawa vyombo vya sheria vimekuwa vikidai uchunguzi kuhusiana na tukio la kupigwa kwake unaendelea licha ya kuwapo kwa taarifa kuwa uchunguzi huo unafanywa ndivyo sivyo.
“Katika ofisi mbalimbali za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi, viongozi wanapeleka taarifa kwamba tukio lile ni kutokana na sababu binafsi, jambo ambalo halina ukweli kwani naamini siku moja ukweli utakuja kuthibitika juu ya tukio hilo kwani mimi kwa asilimia 100 tukio la kupigwa kwangu lilitokana na kazi yangu nikiwa kama Mhariri na Mwenyekiti wa Jukwaa ala Wahariri,” alisema Kibanda.
Akizungumzia kuhusiana na tuzo hiyo na kifo cha Mwangosi, Kibanda alisema tukio la kifo cha Mwangosi lina mfanya asahau maumivu, mateso na ulemavu alioupata na kuwasihi wanahabari kusimama imara na kuweka kando kumbukumbu zote za matukio mabaya yanayowakabili na badala yake washikamane na kupaza sauti zao kupigania uhuru wa vyombo vya habari na wana habari kwa ujumla.
Tuzo hiyo iliambatana na zawadi ya Sh.  milioni 10, hata hivyo Kibanda alitoa asilimia 10 ya fedha hizo kwa ajili ya kutoa sadaka kwa Mungu na nusu ya fedha zilizobaki alizitoa kwa mjane wa marehemu Daudi Mwangosi ili ziweze kusaidia kuendeleza familia hiyo.
Akikabidhi tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication, Tido Mhando alisema mauaji ya Daudi Mwangosi ambaye aliuawa kwa kulipuliwa na bomu katika kijiji cha Nyororo mkoani Iringa  ulikuwa ni mwanzo wa matukio ya ukatili kwa wanahabari hapa nchini ambapo wamekuwa wakinyamzishwa ili kuficha uovu wa baadhi ya watu wachache.
Alisema mwendelezo wa matukio hayo dhidi ya wanahabari  ni pamoja na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari yakiwamo magazeti ya Mwananchi, Mtanzania na Mwanahalisi, huku wakitumia kisingizio cha kuwapaka matope wanahabari kuwa ni wachochezi na wavunjifu wa amani.
“Mambo hayo yasiwarudishe nyuma wanahabari, wakaacha misingi ya kazi yao na badala yake waungane katika mapambano ya kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari unakuwepo nchini” alisema.
Awali Meneja wa Udhibiti wa Viwango wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pilly Mtambalike alisema takwimu zinaonyesha kwamba katika kipindi cha mwaka jana pekee, jumla ya waandishi wa habari 73 waliuawa katika matukio mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la Misaada la Sweden (SIDA), Anetle Bolmewilhelm aliwataka wanahabari kuhakikisha wanafikia mwisho wa vitendo vya unyanyasaji na ukatili unaofanywa dhidi yao na watafanikiwa iwapo tu watashikana na kupaza sauti zao kwa pamoja.
Kwa upande wake Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya aliwataka wanahabari kutambua kuwa watu wanaweza kuua lakini hawawezi kuua mawazo mazuri na nia nzuri ya wandishi wa habari ya kuhabarisha jamii na kwamba kama jamii inahaki ya kujua, kerikali nayo ina wajibu wa kutoa habari.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment