Kaburi la Musengele Kilekamagana Munyigumba Mwamuyinga 'Msigawabena' ambalo liko pembeni mwa kaburi la baba yake, Munyigumba.
Na Daniel Mbega
Ndugu zangu,
Tunaendelea na simulizi ya ‘Nyayo za Chifu Mkwawa’. Tumeona jinsi
Mufwimi alivyotoka Ethiopia (kwa mujibu wa simulizi za ukoo wa Mwamuyinga) na
hata alipoingia katika himaya ya Chifu Mwamduda na kujenga naye urafiki kwa
sababu ya mawindo yake.
Kwamba baada ya kuwa na uhusiano wa siri na binti wa chifu huyo akawa amempa ujauzito, hivyo akaogopa kwamba Chifu Mwamduda akipata taarifa angeweza kumuua.
Kwamba baada ya kuwa na uhusiano wa siri na binti wa chifu huyo akawa amempa ujauzito, hivyo akaogopa kwamba Chifu Mwamduda akipata taarifa angeweza kumuua.
Jioni moja akamwita Semduda na kumweleza kwamba yeye
anaondoka, lakini akampa maagizo, ikiwa atajifungua mtoto wa kike amwite
Mng’anzagala na akiwa wa kiume amwite Muyinga Mufwimi (maana yake ni
Mhangaikaji Mwindaji).
Mufwimi alitoroka kwa hofu ya kuuawa na Mwamduda. Akaendelea
kuwinda huko na huko hadi Itamba alikouawa na nyati. Hakuna ajuaye lilipo
kaburi lake.
Lakini kumbe mtawala huyo alifurahi kusikia bintiye ana
mimba ya Mufwimi, maana alijua sasa angekubali kuolewa. Kwa bahati nzuri, binti
huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi kama
alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.
“Kijana huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamduda hakuwa na
mtoto wa kiume, akaamua kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga
Mufwimi aliyekuwa hodari wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka
kikeni, na hapo ndipo uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa
Muyinga,” anafafanua Malugala.
Muyinga Mufwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa
kiume – Maliga, Nyenza na Mpondwa. Mtwa Maliga naye akazaa watoto watano wa
kiume ambao ni Kitova, Mudegela, Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.
Inaelezwa kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova
yeye atakuwa tabibu (mganga wa tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa
maana hiyo Kitova alikuwa akitibu maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa
vita na kizazi chake ndicho kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha
Image mpaka sasa.
Mudegela Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele,
Wisiko, Kilonge, Kipaule, Mkanumkole, Lusoko na Mwakisonga. Hata hivyo, uchifu
wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Kilonge
Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe na Munyigumba,
lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu, mkewe wa tatu
aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma, Magoyo na
Magohaganzali.
“Kilonge
alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni Kijiji cha Lupembe lwa Senga
(maana yake Pembe ya Ng’ombe), kaburi lake lilikuwa na pembe mbili za tembo,
ingawa nasikia pembe zile ziliibwa na tunaambiwa walioiba wote walikufa
ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na kuzichimbia ili iwe
kumbukumbu,” anasimulia Malugala.
Hata hivyo, uchunguzi wa mwandishi
wa makala haya umebaini kwamba, kaburi la Kilonge Mudegela liko katika kijiji
cha Uleling’ombe, umbali mfupi tu kutoka kijiji cha Mawambala katika Kata ya
Ukumbi wilayani Kilolo. Huko huwa wanafanya matambiko mbalimbali yakiwemo ya
kuombea mvua!
Utawala una mambo yake, wakati
mwingine unatumia njia halali na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema,
Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza
kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.
“Kwa hiyo akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe
ili yeye atawale, halafu akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa
mkewe, lakini wakati anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
“Baada ya mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama
Sekinyaga akamwita Malangalila Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu
Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa
kaka yake ingawa yeye ndiye aliyemlea,” anaeleza Malugala.
Malugala anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama
huyo kujifungua ambapo alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo
Munyigumba akakasirika na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanawe.
Inaelezwa kwamba, alipomfukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika
maeneo ya Sadani, lakini baadaye Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu,
hivyo ikabidi amrudishe.
“Sasa wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda
kumuua huko Sadani, hata kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto
Malangalila Gamoto. Kwa hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro
baba zao,” anaeleza.
Munyigumba alikuwa na wake watano –
Sengimba, Sendale, Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba
mdogo. Sengimba mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na
Wiyolitwe; Sendale alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele
Kilekamagala Msigawabena; Sekinyaga alimzaa Malangalila Gamoto (kwa
Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.
Tutaendelea tena..
No comments:
Post a Comment