Na Daniel Mbega
Ndugu zangu,
Wengi wanaikumbuka Vita ya Maji Maji
iliyodumu kwa miaka miwili baina ya Watanganyika na Wajerumani kati ya mwaka
1905 hadi 1907. Kinachofanya waendelee kuikumbuka ni mbinu zilizotumiwa na
Mtawala wa Wangindo kule Kilwa, Kinjekitile Ngwale huko kwenye Bonde la
Ngalambe alipowapaka na kuwanywesha dawa wapiganaji wake na kuwasadikisha
kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.
Utaalamu huo ulisambaa karibu sehemu kubwa ya Kusini mwa Tanzania pamoja na Nyanda za Juu ambapo uliwaongezea ujasiri mkubwa wapiganaji hao waliokuwa wakiitetea ardhi yao isitawaliwe na Wazungu.
Utaalamu huo ulisambaa karibu sehemu kubwa ya Kusini mwa Tanzania pamoja na Nyanda za Juu ambapo uliwaongezea ujasiri mkubwa wapiganaji hao waliokuwa wakiitetea ardhi yao isitawaliwe na Wazungu.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba, Chifu
Mkwawa na watemi wengine wengi wa wakati huo, pamoja na kuwa na mbinu za
kupigana vita, walitumia jadi, kwa maana ya dawa za kienyeji, katika kupanga na
kupambana na maadui zao.
Kama ambavyo tunaelezwa katika
Vitabu Vitakatifu kwamba, Wafalme wa Israel – tangu enzi za Nabii Musa –
walikuwa wanawauliza kwanza Makuhani kabla ya kupanga vita, ndivyo watawala
wetu wa Kiafrika walivyofanya nao kwa kuomba miungu yao iwasaidie, hasa wakati
huo kwa vile dini ya Kikristo ilikuwa haijaenea.
Kwa
kutambua mafanikio ambayo alikuwa ameyapata katika vita dhidi ya Mwamubambe
Mwalunyungu na wafuasi wake, Chifu Mkwawa alimtumia pia mganga wa jadi Ngondo
Kimamula Mbugi katika timu yake ya kumtabiria nini ambacho kingetokea, kama
anavyoeleza kitukuu wa mganga huyo, Robert Gabriel Meza Mwaigoga.
Mwaigoga anaeleza kwamba, wapiganaji wa Chifu Mkwawa
walikunywa dawa Lundamatwe, mahali pale pale waliponywea kabla ya kupambana na
Mwambambe, katika eneo linaloelekea Mto Ruaha, takriban kilometa tisa hivi
kutoka Lugalo ambako ndiko walikotakiwa kupambana na Wajerumani.
Chifu Mkwawa alikuwa na bunduki moja aliyopewa na Waarabu
wakati ule wa Biashara ya Watumwa, lakini wapiganaji wake wote walikuwa na
silaha za jadi kama mikuki, kombeo, pinde na mishale na mapanga.
Inaelezwa kwamba, akiwa tayari amepewa siri zote za
lilivyokuwa jeshi la Wajerumani chini ya Emil von Zelewiski na silaha
walizokuwa nazo, Chifu Mkwawa aliwaeleza wapiganaji wake kwamba, watajipanga
vyema katika kingo za bonde ambalo Wajerumani wangepita, lakini hakuna ambaye
alitakiwa kushambulia mpaka yeye atakapofyatua risasi ya kuashiria mapambano.
Ngondo Kimamula Mbugi alikuwa amewapaka dawa ambazo
aliwasadikisha kwamba, hakuna Mjerumani ambaye angeweza kuwaona kabla ya mapambano,
na wakati huo Wahehe wangekuwa tayari wamewavamia na kuwashambulia, hivyo hata
kama wangefyatua risasi zao zingetoka maji.
Sehemu waliyopita Wajerumani pale Lugalo ilikuwa nyembamba
kama mkia, kukiwa na kingo kila upande, hivyo kuwawia vigumu kuweza kufanya
mashambulizi ya aina yoyote. Zaidi ya hayo, msitu uliokuwepo ulitoa hifadhi
nzuri kwa wapiganaji wa Chifu Mkwawa.
Kosa alilokuwa amelifanya Von Zelewiski, pamoja na uzoefu
mkubwa wa vita aliokuwa nao, ni kujiamini kupita kiasi na kutotuma wapelelezi
wakachunguze njia na uimara wa jeshi la Mkwawa. Aliamini kwamba, jeshi hilo
lilikuwa kama yale mengine aliyoyapiga sehemu nyingine na kwamba huenda Chifu
Mkwawa hakuwa na nguvu kama za Abushiri wa kule Pangani aliyepigwa mwaka mmoja
nyuma.
Inasimuliwa kwamba, malengo ya Von Zelewiski yalikuwa kwenda
kuivamia ngome ya Chifu Mkwawa kule Kalenga, lakini hakujua kama tayari Wahehe
walikuwa wamejipanga njiani kukifanya kile ambacho hakuna aliyekitarajia.
Ili kuwazuia Wajerumani wasithubutu kufanya shambulio
lolote, Wahehe ambao tayari walikuwa wanafahamu uwezo wa jeshi hilo la maadui
pamoja na kulifahamu eneo lote na kupanga ni mahali gani waanze kushambulia,
walipanga kuwazuia wasitumie mtindo wao wa nusu duara kushambulia. Kwa kuwa
walikuwa wamepata taarifa za Wajerumani walivyopigana huko Pwani, Wahehe
walikuwa wamejiandaa kuhakikisha wanakabiliana vilivyo na askari hao.
Tutaendelea…
No comments:
Post a Comment