Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu
na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Prof. Isaya Jairo akizungumza na Wahasibu kutoka
Taasisi za umma na binafsi waliohudhuria katika hafla ya kutoa tuzo ya Taarifa
bora ya Fedha kwa mwaka 2015, katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (NBAA)
kilichopo Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Kamishna Msaidizi wa Sera wa
Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Shogholo Msangi akizungumza na Washindani wa
tuzo ya Taarifa bora ya Fedha kwa mwaka 2015 kutoka Taasisi za umma na binafsi
takribani 56, katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC) kilichopo Bunju nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mhasibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango Fungu 50 Bw. Christopher Lupama akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, Bw. Pius Maneno baada ya
kukabidhiwa tuzo ya Taarifa Bora ya Fedha kwa mwaka 2015, ambayo imevuka asilimia
75 kwa ubora, katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (NBAA) kilichopo Bunju nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Baadhi ya Maafisa walioambatana
na Mhasibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50, Bw. Christopher Lupama,
wakipeana mkono na Viongozi wa Serikali na Bodi ya NBAA baada ya kupokea tuzo ya
Taarifa bora ya Fedha kwa mwaka 2015, katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC)
kilichopo Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Wahasibu nchini wametakiwa kuzingatia viwango vya uhasibu
vinavyotakiwa na kukubalika kitaifa na kimataifa wakati wa kuandaa taarifa za
fedha kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi Sera, kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Shogholo Msangi, wakati akikabidhi
tuzo za Taarifa Bora za Fedha kwa mwaka 2015/2016, kwaniaba ya Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Dotto James tukio lililofanyika katika Kituo cha Taaluma ya
Uhasibu (APC), kilichoko Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam
Katika
tukio hilo ambalo liliambatana na kufungwa kwa Mkutano wa mwaka wa Wahasibu unaojumuisha
nchi za Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha na Mipango, kupitia Fungu 50, imepata
tuzo ya kuandaa vitabu bora vya mahesabu vinavyokidhi viwango vilivyowekwa na
Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA).
Bw. Msangi amesema kuwa taarifa za fedha hutumika katika matumizi
mbalimbali katika Sekta ya umma na binafsi, hivyo iwapo taarifa hizo zitakuwa
katika viwango vyenye ubora zitaongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Amesema kuwa taarifa hizo pia hutegemewa na wawekezaji katika
kupanga maamuzi yao ya uwekezaji hapa nchini hatua itakayosaidia nchi kufikia
malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu
na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Bw. Pius Maneno, amesema kuwa, kumekuwa na
mafanikio makubwa katika utoaji wa taarifa za fedha kwa upande wa Taasisi za
Umma na Binafsi mwaka huo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Mwaka uliopita Taasisi nyingi za umma zilishindwa kufikia
asilimia 75 ambacho ndicho kiwango cha chini kabisa cha Taasisi kuingia katika ushindani
wa Tuzo ya taarifa bora ya Fedha ya mwaka, lakini kwa mwaka huo, Taasisi za
Serikali zilizokidhi kiwango hicho ni zaidi ya Asilimia 50.” Aliongeza Bw.
Maneno.
Aidha, amesema kuwa katika kutafuta mshindi wa Tuzo hiyo taasisi
mbalimbali zimehusishwa ikiwemo Mamlaka ya Bima Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es
salaam, Taasisi ya Utawala wa Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kabla ya
matokeo kuthibitishwa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA Prof. Isaya Jairo amebainisha
faida za tuzo ya taarifa bora ya fedha kuwa ni pamoja na kujenga uwazi,
uwajibikaji, uadilifu na kuwa na taarifa ya fedha yenye viwango.
Amezitaka Taasisi nyingi kushiriki katika ushindani ili kuboresha
taarifa za fedha za Mashirika yakiwemo ya umma na binafsi, huku akitoa wito kwa
Serikali kuziagiza Taasisi zake kushiriki kikamilifu.
Miongoni mwa wizara zilizoibuka na ushindi wa Tuzo hiyo ni Wizara
ya Fedha na Mipango Fungu 50 ambapo iliwakilishwa na Mhasibu wake Mkuu Bw.
Christopher Lupama kupokea Tuzo hiyo, ambaye amebainisha kuwa Tuzo hiyo imewapa
nguvu ya kuendelea kufanya vizuri katika utoaji wa Taarifa ya Fedha yenye
viwango.
Taasisi 56 zimeshiriki kuwania tuzo hiyo inayoandaliwa kila mwaka
na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
No comments:
Post a Comment