TANZANIA
EDITORS FORUM (TEF)
Mkurugenzi
Jamii Forums aachiwe mara moja
Kwa muda
wa siku tatu sasa Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa
wa Dar es Salaam.
Hadi sasa,
si Melo, familia yake au wanasheria wake walioelezwa kosa linalomfanya
ashikiliwe. Wanasheria wa Melo wameweka kambi katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar
es Salaam, lakini hakuna majibu ya maana wanayopewa na wala Melo hafikishwi
mahakamani.
Taarifa
wanazotoa askari waliopo kituoni hapo, ambazo si taarifa rasmi, ni kwamba Melo
anashikiliwa kwa nia ya kumtaka awape polisi majina wanayoyahitaji ya
wachangiaji wa masuala mbalimbali katika mtandao wa Jamii Forums kwa mujibu wa
Sheria ya Makosa ya Mtandaoni huku wakidai ni maelekezo kutoka “juu”.
Siku ya
Jumatano, Desemba 14, 2016 polisi wamefika ofisini na nyumbani kwa Melo
wakapekua sehemu zote. Taarifa kutoka ofisini kwa Melo zinaonyesha polisi
wamechukua nyaraka mbalimbali ikiwamo hati ya kusajili kampuni, leseni ya
biashara na nyingine.
Pia polisi
wameondoka na wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Jamii Forums kwa mahojiano
zaidi.
Taarifa
nyingine zinaonyesha kuwa polisi wanaomshikilia Melo wanajiapiza kuwa hata kama
mawakili wake watakwenda mahakamani hawatamwachia hadi atekeleze wakitakacho.
Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) linafuatilia kwa karibu mwenendo na utendaji wa Jeshi
la Polisi juu ya suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni unaotolewa na Ibara
ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).
Katika
siku za karibuni, TEF na Watanzania kwa ujumla wanashuhudia ukiukwaji mkubwa wa
haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi linaloelekea kuacha kuheshimu
misingi ya utawala wa Sheria na Katiba ya Tanzania.
Melo kama
mtuhumiwa anayo haki ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma katika muda
usiozidi saa 24. Kitendo cha polisi kumshikilia kwa siku tatu, ambapo hatujui
kama anateswa au la, ni uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.
Tamko la
Haki za Binadamu la Mwaka 1948 linavitaka vyombo vya dola kuheshimu utawala wa
sheria ambao pamoja na mambo mengine msingi wake ni kuheshimu mgawanyo wa
madaraka (separation of power). Kitendo cha Polisi kuanza kuchukua sheria
mkononi kwa kukamatakamata watu, kuwatisha waandishi wa habari na watetezi wa
haki za binadamu hakikubaliki.
TEF
inalitaka Jeshi la Polisi kumwachia mara moja Melo bila masharti au kumfikisha
mahakamani na kumfungulia mashitaka kwa mujibu wa sheria ikiwa ana kosa.
Tunamwomba Rais John Magufuli aingilie kati mzozo huu na kuwafahamisha polisi
kuwa wanayoyatenda wanapalilia mbegu ya chuki katika nchi jambo ambalo si jema
waliache mara moja.
TEF
inaungana na Watanzania kulaani kitendo cha polisi kumkamata Melo kwa kutumia
sheria mbaya isiyokubalika ya Makosa ya Mtandaoni. TEF inatetea haki ya uhuru
wa kutoa mawazo na kukataa ukandamizaji huu wa polisi wanaodai wana maelekezo
kutoka juu chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Mungu ibariki
Tanzania.
Theophil
Makunga,
Mwenyekiti,
Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es
Salaam, Desemba 15, 2016
No comments:
Post a Comment