Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kuelimisha jamii kuzuia ukatili wa kijinsia. WiLDAF inashirikiana na mtandao wa mashirika yanayopinga ukatili wa kijinsia (MKUKI), wadau wa maendeleo na mashirika mengine kuadhimisha kampeni hizi kitaifa.
Yafuatayo
ni matukio mbalimbali ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili kama
yalivyofanyika sehemu mbalimbali nchini Tanzania chini ya kauli mbiu:
Funguka! Pinga ukatili wa kijinsia. Elimu salama kwa wote.
Maandamano ya amani kupinga ukatili wa kijinsia
Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa jiji la Dar es
salaam ulianza kwa maandamano ya amani ambapo maelfu walishiriki
maandamano hayo kutoka Biafra hadi Millenium towers jijini Dar es
salaam. Maandamano hayo yalifanyika tarehe 25 Novemba 2016.
Waziri Ummy Mwalimu mgeni rasmi katika maadhimisho hayo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu alikua mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho hayo
yaliyofanyika tarehe 25 Novemba 2016, jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Ummy alisema serikali ya awamu ya
tano imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba watoto wanapata
elimu salama bila aina yoyote ya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa elimu
bora bila malipo. "Lengo kuu la elimu bila
malipo ni kuhakikisha kuwa watoto wetu hususan wa kike wanapata fursa
ya kwenda shule kusoma na kufikia ndoto zao katika maisha."
Aidha
alitoa wito kwa wadau na serikali kwa ujumla kutumia nafasi zao kupinga
vitendo vyote vya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu
vilevile kwa jamii kuwa na malezi bora na kuzingatia maadili kwa watoto
na vijana wetu.
Mama Anne Makinda mgeni rasmi katika kongamano la kitaifa la Haki za Wanawake.
Aliyekuwa spika wa Bunge la Tanzania mama Anne Makinda alikuwa mgeni
rasmi katika kongamano la kwanza la kitaifa la Haki za wanawake
lililofanyika ukumbi wa Millenium Towers jijini Dar es salaam tarehe 28
Novemba 2016.
Kongamano hilo lililoratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la LSF
lilikuwa na lengo la kujadili namna mbalimbali za kuwawezesha wanawake
kisheria na kiuchumi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Jamii
imeaswa kuhusika kikamilifu katika mapambano ya kupinga ukatili dhidi
ya wanawake na watoto na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na
salama.
Kongamano hilo lilipambwa na kauli mbiu isemayo; Jitambue! Jiamini,
Simamia Haki yako.
Wageni mbalimbali wanaharakati wa Haki za binadamu walihudhuria
kongamano hilo la aina yake wakiwemo Dr. Helen Kijo Bisimba, Mary
Rusimbi, Edda Sanga na Dr. Judith Odunga.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe azindua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Challya Julius alizindua maadhimisho ya
siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika wilaya yake na kuahidi
kusimamia katika kutokomeza ukatili wa kijinsia wilayani humo. Uzinduzi
huo ulifanyika 29 Novemba 2016.
Uzinduzi huo ulienda sambamba na kutoa msaada wa kisheria kwa wahanga wa
ukatili wa kijinsia uliotolewa na wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wa
wilaya ya Rungwe wakishirikiana na shirika la WiLDAF Tanzania.
Jukwaa la Wanafunzi wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Wanafunzi
wa kidato cha 1, 3, 5 na 6 kutoka shule za sekondari za Benjamin Mkapa,
Jangwani, Tandika, Turiani na Temeke walihudhuria jukwaa lilioandaliwa
kwa ajili ya wanafunzi ili wapate fursa ya kutoa maoni juu ya mambo
mbalimbali yanayowakabili mashuleni. Jukwaa hilo lilifanyika 30 Novemba
2016 katika ukumbi wa Millenium Towers jijini Dar es salaam.
Jukwaa hilo liliandaliwa na shirika la WiLDAF Ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Funguka! Pinga Ukatili wa Kijinsia. Elimu Salama kwa wote.
Siku ya UKIMWI Duniani
Januari
mosi kila mwaka hutumika kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani.
Maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa asilimia kubwa yanatokana na vitendo
vya ukatili dhidi ya Wanawake vinavyopelekea maambukizi ya VVU kama
vile ubakaji, mila mbalimbali ambazo zimepitwa na wakati kwa mfano: -
- Ndoa za utotoni ambapo mtoto wa kike hulazimishwa kuolewa na mtu mzima
ambaye pengine ana maambukizi ya VVU.
- Mume kumlazimisha mke kufanya tendo la ndoa iwapo mume ameathirika bila kutumia kinga.
- Mjane kulazimishwa kufanya ngono na mzee anayetakasa wajane.
- Na wajane kulazimishwa kurithiwa na ndugu wa mume wake bila kujali afya ya wote wawili.
Jamii inapaswa kuacha na kukemea mila zilizopitwa na wakati ili kupunguza maambukizi ya UKIMWI.
Mdahalo wa wadau wa maendeleo kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Wadau wa maendeleo kutoka mashirika, serikali na taasisi mbalimbali
walikutana pamoja ili kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusiana na
ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia. Mdahalo huo ulifanyika Desemba 1, 2016.
Hizi ni baadhi ya nukuu kutoka katika mdahalo huo;
"Ukatili
wa kijinsia huanzia nyumbani, shuleni na kwenye jamii. Jamii ipatiwe
elimu ya kutokomeza ukatili."
"Wazazi wawe na ukaribu na watoto katika malezi na kujua mienendo ya
watoto wao."
"Hakuna mtoto anayezaliwa akiwa mtukutu ila inatokana na malezi ya
nyumbani na muda mwingine kupeleka hivyo vitu shuleni na hata kuwafanyia
watoto wengine vitendo vya kikatili."
"Ukatili wa watoto unafanywa na ndugu wa karibu wa nyumbani anaweza
akawa mjomba, dada wa nyumbani."
"Fimbo sio solution (suluhu) ya kumrekebisha mtoto, itafutwe njia
mbadala ya kumuadhibu mtoto."
Vibanda vya Filamu
Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, shirika la
TGNP Mtandao liliandaa vibanda vya filamu ili kujenga uelewa kwa jamii
na kuibua mjadala juu ya vitendo mbalimbali vya ukatili.
Wawakilishi wa Bodaboda wapata mafunzo ya ukatili wa kijinsia, waandamana kupinga ukatili.
Wawakilishi wa madereva wa bodaboda kutoka Wilaya za Ilala, Kinondoni na
Temeke mkoa wa Dar es salaam walipata mafunzo juu ya ukatili wa
kijinsia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia.
Madereva bodaboda wanahusika katika kubeba abiria mbalimbali wakiwemo
wanafunzi hivyo ni muhimu kuwapatia elimu hii ili waweze kutambua
madhara ya ukatili na kusaidia kuilinda jamii dhidi ya vitendo vya ukatili.
Aidha madereva hao waliungana na shirika la WiLDAF kuandamana kama ishara ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kauli mbiu ya maadhimisho ni FUNGUKA! PINGA UKATILI WA KIJINSIA. ELIMU SALAMA KWA WOTE.
Kauli mbiu hii inakusudia kuhamasisha jamii na taifa kwa ujumla
kuangalia ni kwa kiasi gani changamoto zilizopo katika miundombinu,
mifumo ya kibaguzi na kukosekana kwa usawa wa kijinsia, sio tu
kunachochea ukatili wa kijinsia, bali pia kunakwamisha juhudi za
serikali, asasi za kiraia na wadau mbalimbali katika kuboresha elimu na hivyo kusaidia watanzania kujikwamua katika wimbi la ujinga na umaskini.
#UkatiliSasaBasi
No comments:
Post a Comment