Na
Daniel Mbega
MKURUGENZI Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media Limited inayomiliki mtandao
maarufu wa JamiiForums, Maxence Melo, anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu, Desemba 19, 2016 kwa
ajili ya dhamana.
Taarifa zinaeleza kwamba, Melo alishindwa kutimiza sharti la dhamana
katika kesi namba 457, ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,
Mheshimiwa Mwambapa.
Mmoja wa mawakili wanaomtetea Melo, Jebra Kambole, amesema mteja wao
analetwa kesho mahakamani kwa ajili ya dhamana tu kwani kesi hiyo, pamoja na
ile ya 458 ambayo iko mbele ya Hakimu Makazi Nongwa, ziliahirishwa hadi Desemba
29, 2016.
“Kesho analetwa kwa ajili ya dhamana, unajua ilishindikana kupata dhamana
katika kesi hiyo tu baada ya kukosekana mdhamini mmoja, lakini
tulikwishakamilisha dhamana katika kesi nyingine mbili, yaani ile namba 456
iliyo mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba na ile namba 458 iliyo mbele ya Hakimu
Mkazi Mwambapa,” amesema.
Melo, alifikishwa mahakamani Ijumaa, Desemba 16, 2016 na kufunguliwa kesi
tatu zikiwa kwa mahakimu watatu tofauti na kusomewa mashtaka manne, mawili
yakiwa yanalingana, likiwemo la kumiliki mtandao wa JamiiForums ambao
haujasajiliwa nchini Tanzania.
Katika namba 457, ambayo alikosa
mdhamini, ilielezwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwambapa kwamba, katika siku na
tarehe tofauti kati ya Mei 10, 2016 na Desemba 13, 2016 katika eneo la
Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa
Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums,
wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi Tanzania linafanya upelelezi wa jinai
kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa
nia ya kuvuruga uchunguzi, alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo
alikuwa nazo, kinyume na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao
(Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka 2015.
Kesi ya kwanza, ambayo ni namba 456 yenye mashtaka kama hayo yaliyoelezwa
juu, iko mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba, ambapo upande
wa Jamhuri ulieleza kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Aprili 1,
2016 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya
Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd
ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi
Tanzania linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao
yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga uchunguzi, alikaidi
kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa nazo, kinyume na kifungu cha
22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka
2015.
Aidha, katika kesi namba 458, ambayo iko mbele ya Hakimu Nongwa, Melo
anakabiliwa na shtaka la kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini Tanzania
(domain) kinyume na kifungu cha 79(c) cha Sheria ya Mawasiliano ya
Kielektroniki na Posta Namba 3 ya mwaka 2010 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 10 na
17 (4) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Namba 428 za mwaka
2011.
Upande wa Jamhuri ulieleza katika kesi hiyo kwamba, katika siku na tarehe
tofauti kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani
ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii
Media Co. Ltd iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Kampuni (Sura ya 212
kama ilivyorejewa mwaka 2002) yenye hati ya usajili Namba 66333 amekuwa
akiendesha na kutumia tovuti inayojulikana kama jamiiforums.com ambayo
haijasajiliwa kwenye code za Tanzania (country code Top Level Domain - ccTLD),
inayofahamika kama do-tz.
No comments:
Post a Comment