Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Bw. Doto James (kushoto) na
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero
wakisaini mikataba miwili ya mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya
shilingi Bilioni 360 kwa ajili ya kuongeza Ufanisi wa Tanesco na kuiongezea
mtaji Benki ya Maendeleo ya Wakulima nchini-TADB, Makao Makuu ya Wizara ya
Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Bw. Doto James (kushoto) na
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia
Kandiero(kulia), wakibadilishana mikataba ya Mkopo wa Sh. Bilioni 360, zitakazo
kwenda katika Sekta ya Nishati ya Umeme na Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini-TADB,
tukio lililofanyika makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dare
salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu kulia) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero(wa pili kulia), wakisaini
mikataba miwili yenye thamani ya Sh. Bilioni 360 kwa ajili ya kutunisha mfuko
wa bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 na kuendeleza kilimo
kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo-AFDB, huku wakishuhudiwa na Mafisa wa
pande zote mbili. Kushoto ni Kaimu Kamishna wa
Fedha za Nje Mamelta Mutagwaba na wa pili kushoto ni Naibu Kaibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bi. Amina Hamis Shaban, Makao Makuu ya Wizara hiyo Jijini Dar es
salaam.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero (kulia), akizungumza baada ya kusaini
Mikataba miwili ya Mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya shilingi
Bilioni 360, ambapo ameshauri fedha hizo zitumike kikamilifu katika maeneo
husika ambayo ni Bajeti na kuendeleza kilimo. kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango,
jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Bw. Doto James (kushoto) akipiga makofi baada ya Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero (kulia), kuipongeza
Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za maendeleo ya Uchumi hasa katika
viwanda, baada ya kusaini mikataba miwili ya Sh. Bilioni 360, Makao Makuu ya
Wizara hiyo Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) akipeana mkono na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero (kulia), baada ya
kuagwa rasmi, katika Makao Makuu ya Wizara hiyo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) akimkabidhi zawadi ya shukrani aliyekuwa
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero
(kulia) wakati akiagwa rasmi baada ya kupewa majukumu mengine ya Ukurugenzi Mkuu
wa Benki ya AfDB kusini mwa Afrika, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango,
Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) akizungumza na baadhi ya viongozi wa Serikali wakati wa
kumuaga aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt.
Tonia Kandiero, ambapo alimshukuru kwa jitihada zake katika kusaidia
upatokanaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Barabara, nishati,
kilimo na elimu, Makao Makuu ya Wizara, Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na
Taasisi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa tayari kumuaga aliyekuwa
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero
baada ya kufanya kazi nchini kwa takribani miaka sita, Makao makuu ya Wizara ya
Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero wakifurahia uhusiano mzuri uliopo
kati ya Benki ya AfDB na Tanzania ambapo mpaka sasa miradi inayofadhiliwa na
Benki hiyo inafikia thamani ya Dola za Marekani Bilioni 2, wakati wa kuagwa kwa
Dkt. Kandiero, Makao Makuu ya Wizara, Jijini Dar es salaam.
Aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero akitoa maneno ya
shukrani mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb)
(hayupo pichani), wakati akiagwa na Waziri huyo, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha
na Mipango, jijini Dar es salaam.
(Picha zote na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini-WFM)
Na
Benny Mwaipaja-WFM, Dar es Salaam
BENKI ya Maendeleo ya
Afrika-AfDB, imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola Milioni 164,
karibu Shilingi Bilioni 360, kwaajili ya kuchangia Bajeti kuu ya Serikali
katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 pamoja na kuongeza mtaji wa Benki
ya Maendeleo ya Kilimo nchini-TADB.
Mikataba miwili imesainiwa leo
Jijini Dar es salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto
James kwa niaba ya Serikali na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
anayeondoka Dkt. Tonia Kandielo.
Mkataba wa kwanza uliosainiwa
ni kwa ajili ya kutunisha Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo Benki hiyo imetoa dola
za kimarekani milioni 70 sawa na tsh 154 bilioni ambazo zitaelekezwa kuongeza
ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini-TANESCO.
Mkataba wa pili ni kwaajili ya
kuongezea mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini-TADB wenye thamani ya
dola Milioni 94 sawa na shilingi Bilioni 204 kwa ajili ya kuiongezea uwezo
Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima ili kuongeza mnyonyoro wa
thamani kuanzia uzalishaji, uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko ya
uhakika ya mazao ya wakulima.
Uhai wa mikopo yote miwili
utakuwa ni miaka 40 ambapo serikali itaanza kuilipa baada ya miaka kumi tangu
kutolewa kwake, huku riba yake ikiwa chini ya asilimia 1.
Akizungumza baada ya kusainiwa
kwa mkopo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James,
amesema mkopo huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kukuza na kuimarisha
TANESCO na kuendeleza kilimo nchini.
“Tanzania ni nchi iliyonufaika
zaidi na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika-AFDB
ikilinganishwa na nchi nyingine yoyote iliyoko katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika” Alisema Bw.
James.
Kwa upande wake, Mwakilishi
Mkazi wa AFDB anayeondoka Dkt. Tonia Kandielo amesema kuwa hadi sasa Benki yake
imeipatia Tanzania mkopo wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2,
ambazo zimewekezwa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya
barabara, maji, nishati ya umeme, elimu na kilimo.
“Ninaamini kuwa hatua ya
kuongeza mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB itachochea maendeleo ya
kilimo nchini, na tunaahidi kuwa tutaendelea kuiwezesha zaidi siku zijazo”
Alisema Dkt. Kandielo.
Kuhusu Sekta ya Nishati, Dkt.
Kandielo amesema kuwa Benki yake imeona umuhimu wa kuliwezesha shirika hilo ili
liweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi ili kuchochea uchumi wa Taifa.
“Mikopo hii inahusiana na
vipaumbele tulivyoviweka kama Benki ambavyo viko katika malengo matano ambapo
tunataka kuwekeza katika sekta ya nishati, uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda,
kuiunganisha Afrika na kuboresha maisha ya waafrika kwa ujumla" aliongeza
Dkt. Kandielo
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha
na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amemuaga rasmi Dkt. Tonio Kandielo ambaye
amehamishiwa nchini Afrika Kusini kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo atakaye
simamia Kanda ya Kusini mwa Afrika.
Dkt. Mpango, amesifu jitihada
kubwa zilizofanywa na mwana mama huyo katika kipindi cha miaka 6 aliyokuwepo
hapa nchini ambapo ameweza kusimamia vizuri maslahi ya Tanzania katika Benki
hiyo.
Amesema kuwa katika kipindi
hicho Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta za ujenzi wa
miundombinu ya barabara, kilimo, maji na umeme, ambapo benki hiyo ilihakikisha
kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
Amemwomba Mkurugenzi Mkuu huyo
kuwezesha upatikanaji wa fedha kwaajili ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango
cha kimataifa (Standard gauge) inayohitaji fedha nyingi, kusimamia utekelezaji wa mradi wa umeme wa
kikanda unaoanzia nchini Zambia, uboreshaji wa Bandari ya Itungi na Mbambabay.
Akijibu hoja za Waziri wa Fedha
na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Dkt. Tonia Kandielo amesema kuwa anaamini
mrithi wake ataendeleza mazuri aliyoyafanya na kwamba yeye binafsi atahakikisha
anafuatilia kwa karibu miradi ambayo mikataba yake imesainiwa katika nyanja za
maboresho ya sekta ya umeme na kilimo.
No comments:
Post a Comment