Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha
wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu
walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na
vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa utumizi wa kumbi,
kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na
kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Aidha, BASATA linawakumbusha
wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku kukusanya
watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu
wa Sikukuu ya Christmas na Mwakampya ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za
sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuandaa madisko ya
watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata
sheria, kanuni na taratibu.
Aidha, baadhi ya wamiliki na
waendeshaji wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida pasi na kujali
maelekezo ya vibali vyao wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja
waliyopangiwa na BASATA.
BASATA kama mtoaji wa vibali vya
kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi
wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye
kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali
na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau
wote wa Sanaa Heli ya Christmas na Mwakampya
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment