

















Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.
Watu zaidi ya 400 wakazi wa mji wa Kahama na viunga vyake wamejitokeza
kupima VVU wakati wa mashindano ya Mahusiano Cup ambayo huusisha michezo ya mpira wa miguu na mpira wa pete.
Mashindano
hayo ambayo huandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa madini
ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi yalizinduliwa tarehe moja desemba,
yakiwa na lengo la kuhamasisha Jamii kupima afya zao na kuimarisha
uhusiano baina ya wenyeji na Mgodi wa Buzwagi.
Akizungumza
wakati wa Kuhitimisha fainali za michezo hiyo pamoja na
kampeni ya upimaji VVU katika uwanja wa mpira wa Kahama Mji, Katibu
Tawala wa Wilaya ya Kahama Timothy Ndanya amesema wao kama uongozi wa
wilaya ya Kahama wanafarijika na jitihada zinazofanywa na Kampuni ya
Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi katika harakati za
kuhakikisha Jamii inajua afya zao kwa kupima afya na kupanga maisha yao
vizuri.
Ameongeza
pia jitihada hizo zimekuwa zikionekana kupitia katika sekta
ya michezo na hii imekuwa ikijidhihirisha kupitia programu mbalimbali
za michezo ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Kampuni ya Acacia.
Akizungumzia
Mashindano ya Mahusiano Cup ya mwaka huu ambayo yamehusisha
timu nyingi zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita, Katibu Tawala huyo
amesema mashindano ya mwaka huu yamesaidia kuonyesha vipaji vingi vya
wanamichezo ambao hapo awali hawakuwa na fursa ya kuweza kuonyesha uwezo
wao kupitia michezo.
“Kwetu
sisi mmeturahisishia na kwa sababu viongozi wa vyama vya michezo
wako wako hapa, hapana shaka watakuwa wamevitambua vipaji ambavyo
vimekuwa vikionyeshwa kwa muda wote wa mashindano haya na watatafuta
namna nzuri ya kuviendeleza pamoja na kutengeneza timu imara ya
halmashauri ya Kahama Mji ambayo itakuwa ikituwakilisha katika
michezo mbalimbali” Alisema Timoth.
Kwa Upande wake kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi, George Mkanza
amesema michezo ya mwaka huu imekuwa ya mafanikio makubwa sana na kwamba Malengo yake yamefikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Mwaka
huu Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi tulikuwa na
dhamira ya kuwafikia wakazi wengi wa Kahma kwa njia ya michezo ili
kuwapatia elimu juu ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuimarisha Mahusiano
yetu na wenyeji wa Kahama, ndio maana utaona mwaka huu michezo hii
imefanyika nje ya eneo la kata ya Mwendakulima na
kuhusisha timu za tarafa yote ya Kahama Mji” Alisema Mkanza.
Akizungumzia
takwimu za upimaji VVU kwa kipindi cha wiki moja ambacho
Mashindano hayo ya Mahusiano Cup yalikuwa yakiendelea, Kaimu Meneja
Mkuu huyo wa Mgodi wa Buzwagi, amesema jumla ya watu 420 walijitokeza
kupima VVU ambapo kati ya hao Wanawake walikuwa 89 sawa na asilimia
21.1% na wanaume 321 sawa na asilimia 76.4%. Ambapo
kati ya wote waliopima watu 11 walikutwa na maambukizi sawa na
asilimia 2.6%, Wanawake 5 sawa na asilimia 1.19% na wanaume 6 sawa na
asilimia 1.42%
Michezo
ya Mahusiano Cup ya mwaka 2016 ilifanyika katika viwanja vya
Halmashauri ya Mji wa Kahama na Uwanja wa Shule ya Msingi Mwendakulima
ambapo jumla ya timu kumi na nne za mpira wa mguu zilishiri na timu sita
za mpira wa pete.
Timu
zilizoshiriki Mpira wa Mguu:- ni kata ya Nyihogo, Nyahanga, Busoka,
Kahama Mjini, Zongomela, Malunga, Mhungula, Majengo, Mwendakulima,
Ngogwa, Nyasubi, Mhongolo, Wendele, Pamoja na timu ya Mgodi wa Buzwagi,
na kwa upande wa Mpira wa Pete:- timu za Kata za Kahama Mjini ,
Mhungula, Mwendakulima, Mhongolo, Ngogwa na Zongomela
zilishiriki mashindano hayo.
Katika
michezo hiyo zaidi ya wanamichezo 400 walijitokeza kushiriki
ambapo timu za Kahama Mji pamoja na Mhungula ndizo zilizofanikiwa
kuingia fainali, ambapo katika mchezo wa fainali timu ya Mhungula
iliibuka kidedea kwa kuibamiza timu ya Kahama mji jumla ya goli tatu kwa
mbili na kujinyakulia Kombe pamoja na Shilingi milioni
moja huku mshindi wa pili timu ya Kahama Mji kuondoka na kitita cha
shilingi laki saba na nusu pamoja na kikombe.
Kwa
upande wa timu za mpira wa pete zilizofanikiwa kuingia fainali zilikuwa
ni timu za Kahama Mji na timu za Zongomela
ambapo timu ya Kahama Mji iliibuka Mshindi baada ya kuwafunga wenzao wa
kata ya Zongomela jumla ya vikapu 47 dhidi ya 22 na Hivyo kuwafanya
timu ya Kahama Mji kuwa Washindi wa Mahusiano Cup kwa upande wa timu za
netball kwa Mwaka 2016 na kujinyakulia Kombe
pamoja na Shilingi milioni moja huku mshindi wa pili timu ya Zongomela
ikiondoka na kitita cha shilingi laki saba na nusu pamoja na kikombe.
Katika
mashindano hayo hiyo timu ya Mgodi wa Buzwagi ilishika nafasi
ya tatu na kujinyakulia shilingi laki tano kwa upande wa mpira wa miguu
na timu ya Netball kutoka kata ya Mwendakuliam ilikuwa mshindi wa tatu
kwa upande wa mpira wa pete na kuondoka pia na shilingi laki tano. Huku
timu zingine zote zikiambulia kifuta jasho
cha shilingi elfu sabini kila timu.
Kabla
ya kufanyika kwa fainali hizo mapema asubuhi kampuni hiyo ya
Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi iliandaa pia Bonanza maalumu la Michezo
lililowahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani ya mji wa Kahama Bonanza
lililohusisha michezo kama vile kuvuta kamba, kufukuza kuku na mpira wa
miguu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment