Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi wa
uamuzi wake wa kuzuia biashara ya usafirishaji wa wanyamahai nje ya nchi kwa
kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa
lengo la kupanga vizuri biashara hiyo kwa faida ya serikali na wafanyabiashara wenyewe.
Ufafanuzi huo umetolewa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne
Maghembe katika kikao alichokiitisha wizarani hapo na wafanyabiashara wa wanyamahai
wa makundi ya wadudu, vyura, mijusi, ndege, nyani na tumbili ambao walitaka
kupata ufafanuzi wa hatima ya biashara yao kutoka serikalini.
Katika risala iliyosomwa na kiongozi wa wafanyabiashara hao, Adam
Rashid Warioba kwa Waziri Maghembe, aliiomba Serikali kutoa ufafanuzi wa hatma
ya biashara yao iliyofungiwa ambayo imekuwa tegemeo pekee katika kuendesha
maisha yao huku wakitaka kujua hatma ya wanyamahai waliohifadhiwa na gharama
zao walizolipia Serikalini.
Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa Serikali kufungia biashara hiyo kwa
wafanyabiashara hao, Prof. Maghembe amesema wanyamahai wengi kutoka nchini Tanzania
wamekuwa wakisafirishwa nje ya nchi bila ya kufuata utaratibu maalum ikiwemo vibali
vya kukamata na kuwasafirisha wanyama hao jambo ambalo limekuwa likiikosesha
serikali mapato mengi.
“Wapo kati yenu ambao walikuwa wanasafirisha wanyamahai kinyume cha
sheria, bila vibali vyovyote, na wanyama wa Tanzania walikuwa wakimatwa kwenye
bandari na viwanja vya ndege, ambao wanasafirishwa kinyume cha sheria, wengi
tu, na ndio maana Serikali ikasema hii biashara tusimamae kwanza tuwekwe
utaratibu ambao kila mtu ataufuata, na ambao hautaweza kututia aibu huko nje”,
alisema.
Alisema sababu nyingine iliyopelekea serikali kufunga biashara hiyo kwa
muda ni bei ndogo inayouzwa wanyama hao nje ya nchi ambayo haiwanufaishi
wafanyabiashara na Serikali ukilinganisha na thamani yake kwa kile wanachoenda
kufanyiwa, alitolea mfano tumbili ambao hufanyiwa utafiti wa madawa mbali mbali
na baadae kuuzwa mabilioni ya fedha huku tumbili huyo akiuzwa kwa dola 25 tu.
“Nimefurahi yule bwana aliyesema tumbili mmoja ni dola 25, lakini
akasema hao ndio wanafanya medical research (utafiti wa madawa)
yote duniani, sasa sisi tunapata dola 25 na wenzetu wanafanya research
(utafiti) wanatuuzia madawa yote billions of dollars (mabilioni ya
dola za kimarekani), tuweke utaratibu na ninyi mtakapokuwa mnafanya hii
biashara mpate sio lazima serikali ndio lazma ipate, mpate kilicho sawa na
thamani ya wanyama mnaowauza”, alisema Prof. Maghembe.
Aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya awamu ya tano ni
sikivu hivyo kuahidi kushuulikia changamoto walizoziwasilisha hadi kufikia
Januari 10, mwakani (2017), aliwaeleza kuwa hatma ya wanyamahai ambao
wamewahifadhi pamoja gharama za vibali walizowalipia serikalini zitashuulikiwa.
“Ambacho ninaweza kuwaambia hapa leo, kwamba tumepata hii taarifa,
tunayo ile idadi ambayo imepitiwa na wataalamu huko kwenye mazizi, tunazo zile
permit (vibali) za serikali ambazo mmepewa na leseni, vyote vile
mlivyonavyo na sisi tunavyo, tutavipitia vyooote kabisa, alafu tutaona ni namna
gani tutawainua kwa kuwafuta jasho”, alisema.
Aliongeza kuwa “Tutaangalia kila mfanyabiashara ameilipa nini serikali,
kwa wanyama hawa ambao wapo, ambao katazo lilipofanywa walikuwa nao kwenye
mazizi yao na wanyama hao tunawafanyia tathmini tukishakamilisha tutaamua sasa
wanyama hao wanapelekwa wapi, na maeneo yenyewe ni machache tu, ama kwenye
mazoo, ili waweze kutunzwa na kuendelezwa kwa vile ni vigumu kuwarudisha tena
maporini.
“Na kutokana na vibali na risiti
mbalimbali ambazo wameilipa serikali katika kuwapata hao wanyama basi
tutaviangalia na kuangalia utaratibu wa kuwarudishia wale wafanyabiashara hela
zao”.
Akizungumzia lalamiko la wafanyabiashara hao kuwa wao wamezuiliwa
kufanya biashara hiyo huku mfanyabiashara mmoja kutoka nje akiruhusiwa kufanya
biashara hiyo kwa tangazo la serikali, Prof. Maghembe anasema “Na hilo tangazo
mnalosema lina mtu amebebwa hamna ruhusa ya mtu kubebwa hapa, na mtu atayempa
huyo mtu kibali mnafahamu kitakachotokea, hakuna ruhusu, ndivyo serikali
ilivyosema”.
Mei 26, mwaka huu, akifanya majumuisho ya hotuba ya Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2016/17, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Prof. Jumanne Maghembe, alitangaza kuwa ni marufuku kusafirisha wanyamahai wote
nje ya nchi kwa miaka mitatu mfululizo.
“Kuanzia sasa (saa moja na dakika tano usiku) kwa miaka mitatu serikali
imepiga marufuku usafirishaji wa wanyamahai wote kwenda nje ya nchi, hata chawa
wa Tanzania hawataruhusiwa kusafirishwa nje, Na katika kipindi hiki cha miaka
mitatu, idara ya wanyamapori itafanya kazi ya kuishauri serikali namna gani
biashara hiyo itakavyoendeshwa”, alisema Prof. Maghembe.
Imetolewa na;
Hamza Temba
Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii
0713635204/ 0785798011
No comments:
Post a Comment