Kamishna wa Ardhi Msaidizi Nathaniel Methew akiwaeleza
waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam kuhusu kuboreshwa kwa mifumo ya
utoaji huduma kwa wananchi kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA hali iliyochangia kuongeza tija
kupitia kituo cha huduma kwa mteja kilichopo Makao Makuu ya Wizara hiyo na Katika
Ofisi zote za Kanda. Kushoto ni Msajili
wa Hati Msaidizi.
Msajili wa Hati Msaidizi
toka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Apollo Laizer akitoa
wito kwa wananchi kuzingatia sheria na kanuni wanapotaka kumiliki Ardhi ili
kuepusha migogoro ya Ardhi. Kulia ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi Nathaniel Mathew.
Baadhi ya waandishi wa
Habari wakifuatilia mkutano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
uliolenga kutoa ufafanuzi kuhusu maboresho katika kuwahudumia wananchi
kupitia kituo cha huduma kwa mteja.
Na Frank Mvungi-Maelezo
Wizara ya
Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya
Makazi imehudumia wananchi 41,932 kati
ya Novemba, 2015 hadi sasa kupitia
Kituo cha Huduma kwa Mteja.
Kauli hiyo
imetolewa leo jijini Dar es salaam na Kamishina wa Ardhi Msaidizi Bw. Nathanael
Methew wakati wa mkutano na vyombo vya habari, uliofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO),
ambapo alisema lengo la kituo hicho ni
kuongeza tija na kasi ya kuwahudumia wananchi .
“Tunahudumia
watu zaidi ya 400 kwa siku na kwa mwezi ni wateja 8,386 tangu tuanzishe
kituo cha Huduma kwa Mteja hapa
Wizarani,” alisema.
Akifafanua
Methew amesema kuwa kituo hicho kimeweza kusaidia kuondoa malalamiko mengi ya
wananchi dhidi ya Wizara katika kushughulikia kero na changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi katika sekta ya Ardhi.
Akitaja
faida za kituo hicho Methew amesema kuwa kimeongeza imani kwa wananchi na
kuondoa uwezekano wa huduma kutolewa kwa upendeleo.
Kituo hicho
pia kimepunguza kwa kiasi kikubwa muda ambao wateja wanasubiri kupata huduma.
Katika hatua
nyingine Methew amesema kuwa Wizara inao mpango wa kufungua vituo vya huduma
kwa wateja kwenye ofisi zote za Ardhi za Kanda.
Naye Msajili
wa hati msaidizi Bw.Apollo Laizer alitoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria na
kanuni wanapotaka kumiliki ardhi ili kuepuka migogoro inayohusu sekta hiyo.
Aliongeza
kwamba kituo hicho, kinatoa huduma za
utawala wa ardhi,upimaji na Ramani,Mipango Miji na Vijiji,Maendeleo ya
Nyumba,Huduma za Usajili wa Hati,
nyaraka mbalimbali na malalamiko ya wateja.
No comments:
Post a Comment