Kaimu
Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Bi. Ruth Minja akitoa ufafanuzi kwa wahariri wa vyombo vya Habari kuhusu matokeo
ya Utafiti wa Watu wenye uwezo wa kufanya Kazi leo jijini Dar es salaam.
Matokeo hayo yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija ya utendaji kazi katika
shughuli zinazofanywa na makundi mbalimbali ili kubaini mchango wake katika
kukuza Pato la Taifa.
Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari waliohudhuria ufafanuzi kwa wahariri
wa vyombo vya Habari kuhusu matokeo ya Utafiti wa Watu wenye uwezo wa kufanya 2014
Kazi leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa – Dar es
salaam.
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) imesema kuwa takwimu za
matokeo ya utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa Mwaka 2014 zitatumika
kufanya maboresho ya Mipango na Sera mbalimbali za kukuza ajira na kupunguza
umasikini nchini.
Matokeo ya utafiti huo
yameonesha kuwa asilimia 70.9 ya muda wa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi kwa
siku hutumika kwenye shughuli zisizo za uzalishaji ikilinganishwa na asilimia
18.5 inayotumika kwenye shughuli za kiuchumi.
Akizungumza na
wahariri wa vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam Kaimu Meneja wa Idara ya
Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja amesema kuwa matokeo hayo
yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija ya utendaji kazi katika shughuli zinazofanywa
na makundi mbalimbali ili kubaini mchango wake katika kukuza Pato la Taifa.
Amesema kwa mujibu wa utafiti huo Tanzania ina nguvu
kazi ya Taifa ya watu milioni 22.3 wanaume wakiwa milioni 11 na wanawake wakiwa
milioni 11.2 huku idadi ya watanzania walio nje ya nguvu kazi ya Taifa
wakifikia milioni 3.4.
Amefafanua kuwa idadi
ya watanzania walio kwenye ajira ni milioni 20 ikilinganishwa na watu milioni
2.2 ambao hawako kwenye ajira huku akibainisha kwamba kiwango cha nguvu kazi
iliyo katika uzalishaji wa bidhaa na huduma za kiuchumi na nguvu kazi iliyo
tayari kujihusisha na uzalishaji mali kimepungua kutoka asilimia 89.6 mwaka
2006 hadi asilimia 86.7 ya mwaka 2014.
Kwa mujibu wa utafiti
amesema kiwango cha watu wenye umri wa kufanya kazi walio na ajira kwa upande
wa wanaume kwa mwaka 2006 kilifikia asilimia 80.8 ikilinganishwa na asilimia
82.1 za mwaka 2014 huku kiwango hicho hicho kwa upande wa wanawake kwa mwaka
2014 kikifikia 73.8 kutoka 77.6 za mwaka 2006.
“ Kiwango cha watu
wenye umri wa kufanya kazi walio na ajira kwa ujumla kimepungua, hii inaonesha
kuwa, kiwango cha uchumi kuzalisha ajira kimepungua kidogo kutoka asilimia 79.2
mwaka 2006 hadi asilimia 77.8 mwaka 2014” Amesema.
Kuhusu masaa ya
kufanya kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea Bi. Ruth Minja amesema
kuwa kati ya mwaka 2006 hadi 2014 kumekuwa na ongezeko la masaa ambayo watu
hufanya kazi kwa makundi yote ya ajira akifafanua kuwa watu wanaofanya kazi kwa
malipo na waliojiajiri wamekuwa wakifanya kazi zaidi ya saa 50 kwa wiki kuliko
hali nyingine za ajira.
“ Napenda kuwaeleza
kuwa takwimu hizi zitasaidia kuboresha sera ya ajira na programu nyingine ili
kuwe na uwiano kati ya saa za watu wanaofanya kazi, uzalishaji na malipo
wanayopewa” Amesisitiza.
Aidha, amefafanua
kuwa kwa upande wa ukosefu wa ajira kwa muda mrefu kwa watu wenye umri wa miaka
15 au zaidi kote nchini wananwake wana kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira
kuliko wanaume kwa miaka yote ya utafiti uliofanywa na Ofisi hiyo toka mwaka
2006 hadi 2014.
Amesisitiza kuwa ipo
haja kwa Serikali na wadau mbalimbali kushughulikia kiwango cha watu wasio na
kazi na wale ambao hawako tayari kufanya kazi yoyote ya kiuchumi kutokana na
ongezeko lake kuwa kubwa kutokana na athari yake kwa uchumi wa taifa.
“ Kiashiria hiki
katika utafiti tulioufanya kinabainisha kuwa kiwango cha watu ambao hawakuwa na
kazi wala hawakuwa tayari kufanya kazi yoyote ya kiuchumi kimeongezeka kutoka
ailimia 10.4 za mwaka 2006 hadi 17.2 za mwaka 2014 “ Amesisitiza.
Ameeleza kuwa kufuatia
kiashiria hicho wanawake wana kiwango kikubwa zaidi kuliko wanaume kwa kuwa wao
hujishughulisha na shughuli za nyumbani ambazo sio za kiuchumi zikiwemo za
kufua nguo, kupika na malezi ya watoto.
No comments:
Post a Comment