Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Mhe Dkt.
Abdallah Possi akiwasilisha hoja za masuala ya Watu wenye
Ulemavu wakati wa Mkutano wa Bunge wa kujadili Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha
2016/17 kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,
Vijana na Ajira) Mhe. Antony Mavunde tarehe 25 Aprili, 2016.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na
Ajira) Mhe. Antony Mavunde akiwasilisha hoja zinazohusu masuala ya Kazi na Ajira wakati wa
mkutano wa Bunge wa Kujadili Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha
2016/17 Bungeni Dodoma tarehe 25 Aprili, 2016.
(Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Mwandishi Wetu
26/04/2016
Serikali imeahidi kuboresha Makazi ya watu wenye ulemavu na
wenye mahitaji maalum ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha
yao ya kila siku.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye
Ulemavu) Mhe. Dkt Abdallah Possi wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Bunge
wa kujadili Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 Bungeni mjini
Dodoma.
Naibu Waziri aliwaeleza Wabunge umuhimu wa Serikali kuboresha
makazi ya Watu wenye Ulemavu na wenye mahitaji maalum kwa mujibu wa matakwa ya
Sheria ya watu wenye Ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 inayoeleza haki za watu
wenye Ulemavu kuboreshewa maeneo muhimu ikiwemo elimu, ajira, fursa sawa na
miundombinu.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikiasha Watu wenye Ulemavu
wanashiriki katika shughuli mbalimbali kwa kuwawekea mazingira rafiki
yanayowasiaida kutekeleza majukumu yao kulingana na hali zao” Alisema
Mhe.Possi.
Aidha, Serikali imefanya jitihada za awali kwa kuyatembelea
makazi ya watu wenye ulemavu yakiwemo makazi ya Nunge yaliyopo wilaya ya
Kigamboni mkoani Dar es salaam, Sarame Mkoani Manyara, Kituo cha Wagonjwa
wa Ukoma cha Msufini mkoani Tanga pamoja na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na
kubaini umuhimu wa kuyaangalia maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kutatua
changamoto za uvamizi wa makazi ya watu wenye mahitaji maalum.
“Makazi ya watu wenye ulemavu na wale mahitaji maalum yana
changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa majengo, kukosa vifaa, uhaba wa wahudumu,
changamoto za kifedha na uvamizi wa mara kwa mara” Alisema Naibu Waziri.
Naibu Waziri Possi alisisitiza kuwa hadi sasa Wizara hiyo
imeshakubaliana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuangalia
hatua za kuzuia uvamizi katika Makazi ya Watu wenye Ulemavu na wenye Mahitaji
maalum ili kuimarisha usalama wao.
Msingi wa hoja iliyojibiwa na Naibu Waziri imetokana na michango
iliyotolewa na wabunge kuhusu masuala ya Watu wenye Ulemavu kuitaka Serikali
kuhakikisha inaboresha mazingira ya watu wenye ulemavu.
Maeneo yanayoboreshwa na kutekelezwa ni pamoja na
kuwaboreshea namna ya wanavyotakiwa kupata elimu bora, kukomesha mauaji ya
wenye ualbino, suala la kodi na Makazi ya watu wenye ulemavu na wenye mahitaji
maalum wakati wa kuchangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka
wa fedha 2016/17.
No comments:
Post a Comment