Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kuongezeka kidogo kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Mei 2016 jana jijini Dar es salaam.Mfumuko wa Bei mwezi Machi 2016 umepungua hadi asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.6 iliyokuwepo Februari 2016.
Waandishi wa Habari wakiwa kazini, wakati Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikitangaza Mfumuko wa Bei Mwezi Machi 2016 jana.
Picha na Aron Msigwa-MAELEZO.
Na Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Machi 2016 na kusema kuwa umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.6.iliyokuwepo mwezi Februari, 2016.
Hii inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwezi Machi 2016 imepungua kidogo ikilinganishwa na kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma iliyokuwepo mwezi Februari mwaka huu.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Mwezi Machi, 2016 leo jijini Dar es salaam amesema kuwa kupungua kwa mfumuko huo kumesababishwa na kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Takwimu zilizokusanywa katika mikoa yote ya Tanzania Bara Machi 2016 kwa mujibu wa bei za bidhaa zilizoainishwa kupima mfumuko wa bei zinaonyesha kuwa bidhaa zisizo za vyakula katika soko zikiwemo Gesi, dizeli na mafuta ya taa zimechangia kupungua kwa mfumuko huo.
Amesema kuwa pamoja na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa hizo mwezi Machi mwaka huu baadhi ya bidhaa za vyakula zikiwemo za mchele, Mahindi, vyakula kwenye Migahawa na mkaa zimeonesha kuongezeka katika soko.
Kuhusu Fahirisi za Bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi hapa Tanzania kwa mwezi Machi, Kwesigabo amesema kuwa zimeongezeka hadi kufikia 101.93 kutoka 101:44 za mwezi Februari.
Amesema baadhi ya bidhaa za vyakula za vyakula zikiwemo unga wa muhogo, matunda, maharagwe na samaki zimechangia kuongezeka kwa Fahirisi hizo na kuongeza kuwa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni Mavazi ya wanawake, mkaa na kuni.
Kwa upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Machi , 2016 umefikia shilingi 98 na senti 11 ikilinganishwa na uwezo wa shilingi 98na senti 58 wa mwezi Februari 2016.
“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Machi 2016 umepungua, hii ina maana kuwa sasa mtu kuongeza ziada ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa na zile alizokuwa na uwezo wa kuzinunua mwezi Februari"
Kwa upande wa mfumuko wa Bei kwa nchi za Afrika Mashariki mwezi Machi, 2016, Kwesigabo amesema una mwelekeo unaofanana; Kenya umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 6.45 kutoka 6.84 huku Uganda ukifikia asilimia 6.2 kutoka asilimia 7.0 za mwezi Februari.
No comments:
Post a Comment