Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akichangia Hotuba ya
Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma na kusisitiza kuwa
Serikali inaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wanahabari nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Philip Mpango (aliyesimama) akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu
25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma na
kusisitiza Wizara yake inavyochangia masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Dkt. Possy Abdallah
akichangia Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma
na kusisitiza juu ya Serikali inavyosimamia suala la watu wenye ulemavu nchini.
Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
Walemavu Jenista Muhagama na kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Anthony
Mavunde.
Wabunge wakifuatilia mjadala
wa Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
Na
Eleuteri Mangi-MAELEZO
Serikali inaendelea kufanya kazi
kwa ushirikiano na wanahabari nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa
mbalimbali zinazofanywa na Serikali yao katika nyanja za kijamii, kisiasa,
kiuchumi na kiutamaduni ili kuhakikisha Watanzania wanafikia maendeleo yao na
taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye alipokuwa akichangia Hotuba ya
Ofisi ya Waziri Mkuu 25/04/2016 jioni bungeni mjini Dodoma.
“Waandishi wa habari wapo huru
kuuliza maswali kwa Wabunge na kuandika habari kupitia vyombo vyao na kuwapatia
wananchi taarifa mbalimbali zinazoendelea bungeni” alisema Waziri Nape.
Kuhusu idadi ya vyombo vya habari
nchini, Waziri Nape amesema kuwa Tanzania ni nchi yenye vyombo vingi vya habari
yakiwemo magazeti, redio na televisheni ambavyo ni ishara wazi kuwa vyombo
hivyo vipo huru kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya tasnia ya
habari pamoja na katiba, Sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Waziri huyo alisema kuwa Tanzania
sio nchi ya kwanza kutokurusha matangazo ya bunge moja kwa moja (live),
utaratibu huo unafuatwa na Mabunge yote ya jumuiya ya Madola.
Waziri Nape amesema kuwa bado
Serikali inakusudia kuboresha mazingira ya waandishi wa habari ili waweze
kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa wanapotimiza majukumu yao ya kiundishi
wa habari.
Aidha, amewashukuru wabunge kwa
uzalendo wao wa kubaki ndani ya bunge na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo
ya nchi yao kwa manufaa ya wananchi wanaowawakilisha.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Gorge Masaju amewashukuru wabunge kutimiza haki yao ya Kikatiba kuingia
Bungeni na kushiriki mijadala mbalimbali kulingana na ratiba iliyopo
Kwa mujibu wa ibara ya 63 (2), Bunge itakuwa ndicho chombo
kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya
wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo
vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kuhusu matangazo ya Bunge
kurushwa moja kwa moja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Masaju alisema kuwa
Watanzania wanaendelea kupata taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari
nchini.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ibara 18. (2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa
wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa
maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Akitoa ufafanuzi wa ibara hiyo Masaju
alisema kuwa haki ya kupewa taarifa, siyo haki ya kuonekana na vile vile maamuzi
ya Bunge hayafanywi kwa muonekano, bali hufanywa kwa majadiliano ya Wabunge
wakiwa Bungeni.
Bunge litaendelea na vikao vyake
Jumatano Aprili 27, baada ya kuahirishwa kwa mapumziko ya maadhimisho ya Sherehe
za miaka 52 ya Muungano wa Tanzania na ambapo mwaka huu Watanzania wametakiwa kuiadhimisha
wakiwa majumbani au wakiwa katika shughuli zao binafsi.
Mapema mwezi huu Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alielekeza fedha zilizopangwa
kutumika katika maadhimisho hayo ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 2 za
Tanzania zitumike kupanua barabara ya Mwanza Airport katika eneo linaloanzia
Ghana Quarters hadi uwanja wa ndege wa Mwanza ili kupunguza adha ya msongamono wa
magari katika barabara hiyo Jijini humo.
No comments:
Post a Comment