Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 26 April 2016

MAKAMBA: HOJA ZA MUUNGANO NA HATUA ZA UTATUZI

Waziri January Makamba

TAARIFA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) KUHUSU UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA MUUNGANO 

HOJA ZA MUUNGANO NA HATUA ZA UTATUZI

1. UTANGULIZI
Katika kuhakikisha kuwa changamoto za Muungano zinatatuliwa, Serikali ilianzisha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Maagizo hayo yalitolewa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2006 na kuwataka Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi kukutana na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazoukabili Muungano wetu. Katika kipindi hicho Ofisi ya Makamu wa Rais iliratibu vikao viwili (2) kati ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tarehe 22 Mei, 2006, Dar es Salaam na tarehe 21 Novemba, 2006, Zanzibar.

Hata hivyo, mwezi Februari 2008, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya marekebisho ya kiutendaji serikalini ambapo Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kushughulikia masuala ya Muungano iliwekwa chini ya Uongozi na Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuzingatia utaratibu huo, kikao cha kwanza chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais kilifanyika tarehe 15 Mei 2008 Dar es Salaam, na vilivyofuata vilikuwa ni: tarehe 11Oktoba, 2008, Zanzibar; tarehe 19 Mei, 2009, Dar es Salaam; tarehe 2 Juni, 2010, Zanzibar; tarehe 28Januari, 2012, Dar es Salaam; tarehe 13 Januari, 2013, Zanzibar na tarehe 23 Juni, 2013, Dodoma.


2. KAMATI YA PAMOJA YA SMT NA SMZ YA KUSHUGHULIKIA MUUNGANO

Kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 jumla ya hoja kumi na tano (15) ziliwasilishwa na kujadiliwa na Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ. Kati ya hizo, hoja kumi na mbili (12) zimepatiwa ufumbuzi na hoja tatu (3) zipo katika hatua mbalimbali ya kutafutiwa ufumbuzi. 

2.1. CHANGAMOTO ZILIZOPATIWA UFUMBUZI

2.1.1. Utekelezaji wa Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora
Hoja:Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sura Namba 391 inayosimamiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilikuwa haitekelezwi Zanzibar kwa kuwa haikuwa suala la Muungano na pia haimshirikishi Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwenye dhamana ya mambo ya Haki za Binadamu.

Hatua: Baada ya majadiliano katika vikao vya kamati ya Pamoja, suala hilo limepatiwa ufumbuzi kwani Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ‘Written Laws Miscellaneous Amendments’, Namba 8 ya mwaka 2006. Sasa sheria hiyo ni ya Muungano na Tume inafanya kazi pande zote mbili za Muungano.

Kufuatia maridhiano hayo, Hati ya makubaliano ilisainiwa na Mawaziri husika kutoka Serikali zote mbili katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika tarehe 2 Juni, 2010, Zanzibar.

2.1.2. Utekelezaji wa Merchant Shipping Act katika Jamhuri ya Muungano na Uwezo wa Zanzibar Kujiunga na International Maritime Organisation(IMO)

Kwa mujibu wa sheria na taratibu za ‘IMO’ Zanzibar haiwezi kujiunga na ‘IMO’ kwani mwanachama lazima awe Dola. Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utaifa ni mmoja na kwamba, pamoja na kuwa na serikali mbili, utaifa huu unawakilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Hoja: Zanzibar ilikuwa na sheria yake ya usafiri baharini “Maritime Transport Act, 2006” ambayo imekuwa ikitumika kwa masuala yote yanayohusu uchukuzi na usalama wa njia ya majini katika mikataba yote ya SMZ chini ya (Zanzibar Maritime Administration). Aidha, ilikuwa na mpango wa kuanzisha chombo chake cha kusimamia masuala ya usafiri majini. Sheria ya ‘Merchant Shipping Act’ ya mwaka 2003 imekuwa ikitumika katika masuala yote yanayohusu uchukuzi na usalama wa njia ya majini kwa upande wa Tanzania Bara na katika mikataba yote ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hali hii ilizusha utata wakati Zanzibar ilipoomba uanachama kwenye taasisi ya International Maritime Organisation (IMO).

Hatua: Ingawa uanachama wa ‘IMO’ ni wa kitaifa, baada ya mashauriano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ‘IMO’, imekubalika Zanzibar kuwa na Mamlaka yake ya usafiri majini (Zanzibar Maritime Administration) ambayo itatekeleza baadhi ya majukumu kulingana na mikataba ya kimataifa. Majukumu yanayoweza kutekelezwa na ZMA ni yale yaliyoko ndani ya Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa watu baharini ( Safety of life at Sea – SOLAS), ambayo kiutaratibu utekelezaji wa majukumu hayo huweza kusimamiwa na Taasisi nyingine kwa niaba ya Nchi mwanachama wa IMO.

Aidha, majukumu yaliyobainishwa na IMO yasiyoweza kukasimiwa ni: Mafunzo ya Mabaharia; Utafutaji na Uokoaji baharini; Ukaguzi wa meli za kigeni zinazotumia bandari ya Tanzania; na Ulinzi wa majini na bandarini.

Hoja hii imepatiwa ufumbuzi na Hati ya makubaliano imesainiwa na Mawaziri husika kutoka Serikali zote mbili katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichofanyika tarehe 2 Juni 2010, Zanzibar.

2.1.3. Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu 

Ukanda wa uchumi wa bahari kuu unasimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia sheria Na. 1 ya Mamlaka ya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari kuu. 
Hoja:Sheria ya Mamlaka ya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari kuu ilikuwa haitekelezwi Zanzibar kutokana na kutozihusisha taasisi za SMZ zinazoshughulikia masuala ya Uvuvi katika Bahari Kuu katika utekelezaji wake. 

Hatua: Baada ya majadiliano, Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwezi Februari, 2007 kupitia Sheria Na. 4 ya mwaka 2007 na kuzitambua taasisi zinazohusika na matumizi ya Bahari Kuu kwa upande wa Zanzibar na kuzijumuisha katika Kamati ya utendaji ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu hivyo, kuiwezesha mamlaka kuanza kazi zake rasmi mwaka 2010. Hatua nyingine muhimu sambamba na marekebisho ya sheria hiyo ni: kufunguliwa kwa ‘Deposit Account’ ambayo mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu yatawekwa; kufikiwa kwa makubaliano ya kugawana mapato hayo; na pia mgao wa wafanyakazi wa mamlaka kwa pande zote za Muungano. 

Kwa sasa Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu ni moja, na Makao Makuu yake yako katika kijiji cha Fumba Zanzibar. Mamlaka hiyo ina majukumu ya kutoa leseni za uvuvi katika bahari kuu, kudhibiti viwango vya uvuvi, kusimamia rasilimali ya uvuvi na hifadhi ya mazingira ya bahari na uendelezaji wa rasilimali za uvuvi katika bahari kuu.

Hata hivyo, Sheria hiyo bado haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi, hivyo Sekta husika zimekubaliana utaratibu wa muda ili shughuli za mamlaka ziendeshwe katika utaratibu huo wa mpito hadi hapo Sheria hiyo itakaporidhiwa na Baraza la Wawakilishi.

2.1.4. Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki 
Hoja:Nafasi ya Zanzibar kuwasilisha miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya kujumuishwa katika miradi ya kikanda inayotekelezwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hatua: Katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inashiriki kikamilifu na kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya yaAfrika Mashariki, iliwasilisha miradi minane ya maendeleo kwa ajili ya kujumuishwa katika Miradi ya Kikanda inayotekelezwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Miradi minne ya kikanda kati ya minane ilipewa kipaumbele kwa ajili ya kuandaliwa maandiko ya miradi, usanifu na tathmini ya gharama tayari kwa kuombewa fedha za utekelezaji. Miradi iliyowasilishwa kwa Sekretarieti ya Jumuiya kwa ajili ya kutafutiwa fedha kwa Wadau wa Maendeleo na Wawekezaji ni; ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba; Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Maruhubi; Mradi wa Ujenzi wa Chelezo (Dry Dock Construction) na Mradi wa Kivuko (Roll on Roll off – RoRo) kati ya bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Pemba, Tanga na Mombasa. 


Aidha, kwa miradi mingine ambayo ni ya kisekta imekubalika itashughulikiwa na sekta husika, miradi hiyo ni: Mradi wa Ukuzaji wa zao la Taifa na karantini ya Wanyama na Programu ya Kuifanya Zanzibar kuwa eneo huru la milipuko ya maradhi ya Mifugo (Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na Wizara ya Kilimo na Maliasili - SMZ); Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa njia ya upepo (Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati – SMZ); Programu ya Kilimo na Chakula (Wizara ya Kilimo na Maliasili – SMZ) na Mradi wa Uratibu wa Magonjwa ya Mifugo Ukanda wa Zanzibar (Wizara ya Mifugo na Uvuvi – SMZ).

2.1.5. Mgawanyo wa Mapato 
• Mgawanyo wa Mapato Yatokanayo na Misaada Kutoka Nje

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipata misaada mbalimbali kutoka kwa washirika wa maendeleo na nchi wahisani kwa ajili ya kutekeleza programu za maendeleo. Hoja:Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokupata mgao stahiki wa mikopo ya kibajeti inayotolewa na wahisani katika General Budget Support (GBS).

Hatua: Mazungumzo yaliyofanyika baina ya SMT na SMZ imeridhiwa kwamba fomula ya asilimia 4.5 itumike katika kuhakikisha SMZ inapata fungu lake. Hivyo, kuanzia mwaka wa fedha 2009/2010 Zanzibar inanufaika na gawio hilo la asilimia 4.5 ya Misaada ya Kibajeti (General Budget Support – GBS). 

• Misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF

Kulikuwa na makubaliano ya awali na IMF kuhusu matumizi ya fedha za MDRI (Multilateral Debt Relief Initiative) zitokanazo na misamaha ya mikopo ya IMF kwamba, Zanzibar itatumia fedha hizo kununua vifaa vya kutengenezea barabara, kilimo, n.k. 

Hoja: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilihitajikununua pia magari kwa ajili ya matumizi yake kupitia fedha za MDRI suala ambalo halikuwepo katika makubaliano ya awali baina ya Tanzania na IMF.

Hatua: Katika kulishughulikia hili, Wizara ya Fedha SMT ilifanya mawasiliano na IMF kuangalia uwezekano wa Zanzibar kujumuisha ununuzi wa magari kati ya vitu vinavyoweza kupatikana kutoka katika msamaha huo. Maombi hayo yalikubaliwa na suala hili limeshapatiwa ufumbuzi kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishapata fedha za misamaha hiyo na tayari ilishanunua vifaa vya kujengea barabara, vifaa vya hospitali, vifaa vya kilimo na magari kwa ajili ya matumizi ya Serikali.

TANBIHI: Katika hoja hii ya Mgawanyo wa Mapato, vipengele viwili vinaendelea kutafutiwa ufumbuzi ambavyo ni Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na Mgawanyo wa mapato yatokanayo na Faida ya Benki Kuu.(Angalia katika kipengele cha hoja zilizo katika hatua mbalimbali za utatuzi).

2.1.6. Kodi Nyinginezo: PAYE na Withholding Tax

Hoja: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hainufaiki ipasavyo na kodi ya mapato yatokanayo na mishahara ya wafanyakazi wa taasisi za Muungano waliopo Zanzibar (PAYE) pamoja na kodi ya kampuni na mashirika yanayofanya kazi Zanzibar (Withholding Tax). 

Hatua: Kutokana na hali hiyo, pande zote mbili za Muungano zimekubaliana kuwa, Sheria ya Kodi irekebishwe ili mapato yanayokusanywa kutokana na mishahara ya wafanyakazi, kampuni au mashirika kwa upande wa SMZ yabaki Zanzibar na yale yanayokusanywa na SMT upande wa Tanzania Bara yabaki Tanzania Bara. Aidha, pande zote mbili za Muungano zimekubaliana SMZ ipate asilimia 4.5 ya sehemu ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye kodi ya mishahara ya wafanyakazi (PAYE) kama utaratibu wa muda na fedha hizo kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina wa SMZ wakati utaratibu wa kurekebisha sheria unaendelea.


2.1.7. Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa Ndani na Nje ya Nchi

Utaratibu uliokuwepo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhusiana na suala la mikopo ya ndani na nje ya Nchi ni kuwa, SMT hupokea mapendekezo ya miradi kutoka SMZ na kuitafutia fedha miradi husika, Ingawa SMT huingia mikataba ya mikopo husika, SMZ ina wajibu wa kulipa madeni husika pamoja na riba kwa SMT. Aidha, kwa upande wa kukopa ndani ya Nchi, ilikuwa ni kwa kutumia dhamana ya SMT.

Hoja: Uangaliwe utaratibu utakaowezesha SMZ kukopa katika soko la ndani bila dhamana ya SMT na SMT isilazimike kulipa madeni hayo iwapo SMZ itashindwa kulipa. 

Hatua: Katika kulishughulikia hili, Wizara zinazoshughulikia masuala ya fedha SMT na SMZ ziliandaa utaratibu na muongozo wa kuendesha suala hili. Baada ya mashauriano suala la Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa ndani na nje ya Nchi limepatiwa ufumbuzi. Kwa sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweza kukopa ndani ya nchi bila kikwazo chochote. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweza kukopa nje ya nchi chini ya udhamini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MOU) kuhusu hoja hii imeandaliwa na endapo itaridhiwa na sekta husika pamoja na Wanasheria Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasainiwa katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ.

2.1.8. Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa Kodi mara mbili

Hoja: Kuwepo kwa tofauti ya ukadiriaji wa viwango vya thamani za bidhaa, na kodi ya forodha baina ya ofisi za TRA zilizoko Tanzania Bara na zile zilizoko Zanzibar kutokana na mifumo tofauti ya ukadiriaji. Tofauti hii ilisababisha kufanywa kwa makadirio mapya ya kodi, ambayo ni ya viwango vya juu, kwa bidhaa zitokazo Zanzibar zinazoingia soko la Tanzania Bara. Hali hii ilileta malalamiko kwa wafanyabiashara wa Zanzibar, ambao nao wanatumia kipengele cha sheria ya kodi kinachosema kwamba; “Bidhaa zinazoingizwa nchini na kukamilisha taratibu zote za kiforodha kupitia kituo chochote rasmi cha forodha zihesabike kuwa zimeingizwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, na kwamba hakuna haja ya kufanya upya makadirio kwa bidhaa zinazoletwa Tanzania Bara. 

Hatua: Katika kulishughulikia suala hili, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilitengeneza mfumo mpya wa ukadiriaji (Import- Export Valuation Database) ambao unathaminisha sawa bidhaa kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Mfumo huo umeanza kutumika tarehe 25 Februari, 2011 katika vituo vyote vya forodha nchini na ulipaswa kutumika katika vituo vyote vya forodha vilivyopo Zanzibar. Hata hivyo, mfumo huo bado haujakubalika na kutumika kikamilifu kwa upande wa Zanzibar.

Kutokana na kutokukubalika kwa mfumo huo upande wa Zanzibar, Serikali zetu zimekubaliana kuwa, TRA ifanye tathmini ya mfumo mpya wa kufanya ukadiriaji/uthaminishaji (Import-Export Valuation Data base) ili kubaini faida na mapungufu. Aidha, pande mbili zimekubaliana utaratibu unaotumika sasa wa tathmini uendelee katika kipindi cha mpito.

2.1.9. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa SMT

Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya majimbo ya uchaguzi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Hoja: Mfuko wa maendeleo ya Jimbo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukumhusisha mjumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Kamati ya Usimamizi wa Mfuko ili kuweza kujua matumizi ya fedha na mipango ya maendeleo ya jimbo. 

Hatua: Katika kurekebisha utata uiojitokeza kwa majimbo ya Zanzibar, SMZ imeamua kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa lengo sawa na lile la Mfuko wa Maendeleo ya jimbo kwa Wabunge wa SMT.

Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MOU) kuhusu hoja hii imeandaliwa na endapo itaridhiwa na sekta husika pamoja na Wanasheria Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasainiwa katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ.

2.1.10. Ongezeko la Gharama za Umeme 

Hoja: Mnamo mwezi wa Januari 2008, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipandisha bei za umeme kwa wateja wa TANESCO ikiwemo Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO), kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na usambazaji wa umeme. Bei iliongezeka kwa asilimia 168 badala ya asilimia 21.7. Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya TANESCO NA ZECO suala hilo lilipatiwa ufumbuzi. Vilevile, mwaka 2011, bei zaumeme pamoja na “Demand Charge” ziliongezekatena. Kupanda kwa gharama hizo kulileta malalamiko kwa watumiaji wa umeme kwa upande wa Zanzibar kutokana na kutotolewa kikamilifu sababu za ongezeko hilo. 

Katika kuzitafutia ufumbuzi hoja zilizobakia ZECO iliwasilisha mapendekezo ya kupunguziwa bei ya umeme ya Tarriff 3 kwa asilimia 40.


Katika kuzitafutia ufumbuzi hoja zilizobakia ZECO iliwasilisha mapendekezo ya kupunguziwa bei ya umeme ya Tarriff 3 kwa asilimia 40. Baada ya majadiliano TANESCO na ZECO waliwasilisha mapendekezo kwa SMT, ya ZECO kupunguziwa bei ya umeme wa Tarrif 3 kwa asilimia 31. Gharama hizo ni kwenye maeneo ya gharama za “Own generation and Transmission”, gharama za ununuzi wa umeme (Purchased electricity), gharama za usambazaji (Distribution), gharama za uchakavu (Depreciation) na gharama za miundombinu (Infrastructure).

Hatua: Baada ya mjadala wa kitaalamu na wa kina, makubaliano ya kufanya marekebisho ya viwango vya bei yalifikiwa na kwamba TANESCO na ZECO wanatakiwa kuongeza uwazi katika gharama za uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Hata hivyo, taarifa iliyopo ni kuwa, mpaka kufikia Februari, 2016 ZECO ilikuwa ikidaiwa na TANESCO shilingi bilioni 85 na kwamba inatakiwa itolewe taarifa juu ya hatua iliyofikiwa ya kulipwa deni hilo kwa kufuata taratibu zinazotakiwa za ulipaji wa madeni.

2.1.11. Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano 

Nafasi za ajira kwa Wazanzibar katika taasisi za Muungano ni mojawapo ya masuala ambayo yamejadiliwa katika vikao vya mashauriano. 

Hoja: Kupungua kiwango cha ushindani katika soko la ajira kwa wazanzibari kunatokana na tofauti ya mitaala ya elimu ya msingi na Sekondari kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Aidha, hoja nyingine ilikuwa ni kuendeleza Ari na Dhamira ya Muungano katika kufanya uteuzi wa nafasi mbalimbali katika Taasisi za Muungano.

Hatua: Kamati ya kukuza mitaala iliundwa ikiwa na wajumbe kutoka pande zote za Muungano. Baada ya kulinganisha mihutasari yote ya ngazi zote za Elimu (Msingi na Vyuo) ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar, pamoja na majadiliano ya muda mrefu, ilionekana kuwa tatizo sio tofauti ya mitaala bali ni nafasi za watumishi kwa Tanzania Zanzibar kwa Taasisi za Muungano.

Hivyo imekubalika kuwa, yafanyike marekebisho ya Sheria na Kanuni. Aidha, uwepo mkakati wa kiserikali wa kuhamasisha watumishi wa SMZ na Wazanzibar kuomba ajira zinazotangazwa na SMT au Taasisi za Muungano; kuhamasisha Taasisi za Muungano kuwa na Ofisi Zanzibar na Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma kuhakikisha kuwa utaratibu wa kuendesha usaili unafanyika pia Zanzibar. 

Vilevile, kwa nafasi zinazohitaji uteuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hushauriana pindi nafasi hizo zinapojitokeza ili kuwa na uwiano baina ya pande mbili za Muungano. Kuhusu nafasi za Watumishi wa kawaida kwenye taasisi za Muungano, utaratibu wa muda wa mgao wa ajira umekubalika kutumika na tayari umesambazwa kwa wadau.

2.1.12. Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Kimataifa

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ndiyo yenye wajibu wa kuratibu na kusimamia masuala yote ya Kimataifa yaliyo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hoja: Wizara ya mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuipa nafasi ndogo Zanzibar katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi kwenye Taasisi za Kimataifa. 

Hatua: Katika kushughulikia suala hilo, SMT na SMZ zimetayarisha mwongozo kuhusu ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya Kimataifa. Mwongozo huo umezingatia maeneo ya ziara za viongozi wa kitaifa; mikutano ya kimataifa; nafasi za masomo ya elimu ya juu nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada au mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali kutoka nje ya nchi. 

Vile vile kwa masuala yasiyo ya Muungano, Mwongozo huo umeainisha namna ambavyo Serikali zetu mbili zinashirikiana kwenye masuala ya kimataifa. Wizara zinazoshughulikia masuala yasiyo ya Muungano zinazoshabihiana zinatakiwa kuwasiliana na kushirikiana kuandaa taarifa za pamoja kuhusu sekta husika kuanzia hatua za awali. Taarifa hizo za pamoja hubeba mahitaji ya pande zote mbili kwa masuala mbalimbali.

Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MOU) kuhusu hoja hii imeandaliwa na endapo itaridhiwa na sekta husika pamoja na Wanasheria Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasainiwa katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ.

2.2. CHANGAMOTO ZILIZOPO KATIKA HATUA ZA MBALIMBALI ZA KUTAFUTIWA UFUMBUZI 

2.2.1. Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asili

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ni suala la Muungano.

Hoja: Namna ya kugawana mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia itakapopatikana. 

Hatua: Serikali zetu baada ya kujadiliana, ziliamua kumtumia mshauri mwelekezi AUPEC wa Uingereza ili atoe ushauri wa kitaalam kuhusu mgawanyo wa mapato ya rasilimali ya aina hiyo kwa nchi zilizoungana. 

Kampuni ya AUPEC ilikamilisha kazi hiyo na kuwasilisha mapendekezo kwa Serikali zetu mbili ambazo zinasubiri maelekezo kutoka ngazi za juu za uongozi ili kupatiwa ufumbuzi. Hata hivyo, hoja nyingine ilijitokeza kuwa suala la mafuta na gesi asilia liondoshwe katika orodha ya mambo ya Muungano.

Baada ya majadiliano baina ya viongozi wa SMT na SMZ, Pande zote mbili zimekubaliana kuliondoa suala la utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asili katika orodha ya mambo ya Muungano. Aidha, iliundwa timu ya wataalamu ikiongozwa na Wanasheria Wakuu wa SMT na SMZ ili kuandaa Utaratibu wa Mapendekezo ya Sera na Sheria zitakazoruhusu SMZ iendelee na matayarisho ya Utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia.

2.2.2. Taarifa ya Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha

Tume ya Pamoja ya Fedha ilifanya tafiti mbalimbali na kutoa mapendekezo kwa Serikali zote mbili (SMT na SMZ) mwaka 2006. Mapendekezo hayo yanajumuisha vigezo vya kuchangia gharama na kugawana mapato ya Muungano. 

Hoja: Serikali kutolea maamuzi mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha iliyowasilishwa serikalini tangu 2006 na kuwasilishwa tena 2010.

Hatua: Wizara ya Fedha SMT ilishaandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha na ulishajadiliwa na Makatibu Wakuu (IMTC) na baadae kuwasilishwa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri. SMZ imekamilisha zoezi la kupitia mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha juu ya uchangiaji wa gharama na mgawanyo wa mapato ya Muungano kutoka ngazi ya Wizara hadi Baraza la Mapinduzi. 

2.2.3. Mgawanyo wa Mapato

• Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki

Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki ilianzishwa Desemba, 1919 kufuatia Uingereza kutawala nchi za Afrika ya Mashariki kutoka kwa wakoloni wa kijerumani baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia. Bodi hii ilikuwa na jukumu la kutoa na kudhibiti usambazaji wa sarafu ya uingereza katika kipindi hicho kwenye makoloni yake ya Afrika Mashariki.

Mwaka 1920, Tanganyika iliingizwa kwenye Bodi hiyo baada ya kuwekwa chini ya himaya ya Uingereza na uliokuwa Umoja wa Mataifa (League of Nations).Tarehe 1 Januari, 1936, Zanzibar ilijiunga kwenye Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki.

Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 50, utawala wa kikoloni ulianza kufikia mwisho kufuatia nchi nyingi za Kiafrika kupata uhuru. Hali hii ilisababisha kuanza kujitokeza kwa dalili za kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki. Tangazo la kuanzishwa kwa Benki Kuu za nchi za Kenya, Tanzania na Uganda lilitolewa mwezi Juni, 1965. Mwaka 1966 Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki ilikoma kufanya kazi.

Kufuatia maamuzi ya kuivunja Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki na kuanzishwa kwa Benki Kuu kwa kila nchi zilizokuwa wanachama, Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1965 ilipitishwa na Bunge la Tanzania mwezi Desemba 1965. Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa tarehe 14 Juni, 1966.

Hoja: Zijulikane hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika bodi ya Sarafu ambazo ziligawanywa kwa nchi wanachama kabla ya bodi hiyo kuvunjika mnamo mwaka 1966.

Hatua: Katika majadiliano ya kamati imekubalika hoja hii isubiri Mawaziri wa Fedha SMT na SMZ kukutana na kupitia nyaraka za siri kuhusu Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki 

• Mgawanyo wa mapato yatokanayo na Faida ya Benki Kuu

Kabla ya kuvunjika kwa bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1966; nchi wanachama zilishauriwa kuanzisha benki kuu zao ili ziweze kusimamia na masuala ya sarafu na fedha kwa nchi hizo. Benki kuu ya Tanzania ilizinduliwa mnamo tarehe 14 Juni, 1966 na Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hoja: Mgao wa mapato yatokanayo na faida ya benki kuu ufanyike kwa kuzingatia kiwango cha hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.

Hatua: Hoja hii pia imekubalika isubiri Mawaziri wa Fedha kupitia nyaraka za siri kuhusu hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizokuwa katika bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.

2.2.4. Usajili wa Vyombo vya Moto
Hoja:Kumekuwa na changamoto juu ya matumizi ya vyombo vya moto vinavyosajiliwa upande mmoja wa Muungano kutumika upande mwingine. Hivyo, sheria ziwianishwe ili kuondosha changamoto hiyo.

Hatua: Baada ya majadiliano ya Serikali zote mbili, imeonekana Sheria za Usajili wa Magari ziwianishwe ili gari likitoka upande mmoja wa Muungano kwenda upande mwingine, ijulikane kuwa imesajiliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kanzidata (Database) inayojumuisha taarifa kuhusu usajili wa magari ziimarishwe na kuwekwa bayana.

Kwa upande wa Zanzibar mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya Usafiri nambari 7 ya mwaka 2003 na kanuni zake yamewasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ. Kwa upande wa Tanzania Bara Sheria zinazohusiana na vyombo vya moto mapendekezo yake yameingizwa kwenye sheria mpya ya Usalama Barabarani ambayo ipo katika mchakato wa kutungwa.

Imewasilishwa leo,

25 Aprili 2016

No comments:

Post a Comment