Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Na Fidelis Butahe na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Iko dhana kuwa ili Tanzania ipige hatua kimaendeleo inahitaji kiongozi anayethubutu kufanya uamuzi mgumu hasa kuwawajibisha viongozi wabadhirifu na wazembe, lakini Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba amekwenda mbali zaidi; anasema dawa ni kufanya uamuzi wa kidikteta.
Makamba alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Mbunge huyo ambaye hivi karibuni alitangaza nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, ametoa kauli hiyo wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi huo huku tayari watu mbalimbali, hasa kutoka chama tawala cha CCM wakiwa wameshaanza kujinadi.
“Moja ya vitu vitakavyozuia rushwa ni adhabu kali ambayo itaonekana. Kwa nini madikteta wanawaua watu hadharani? Wanachojaribu kukionyesha ni kwamba kama siku moja mtu akijaribu kuwapindua atapelekwa uwanjani na kupigwa risasi hadharani. Lengo ni kuwatia watu hofu,” alisema.
Alisema, “Moja ya namna ya kupambana na rushwa ni kuwatia watu hofu, kwamba ukikamatwa yatakayokukuta ni kama yanayowakuta wenzako.”
Alisema ili kupambana na rushwa ni lazima kuwekwe mbinu za kivita na kwamba kama hilo lisipofanyika ni sawa na kupoteza muda.
“Serikali itakuwa inakusanya mapato na kupanga mambo yake, lakini asilimia 50 ya mambo hayo yanarudi mikononi mwa watu,” alisema.
Makamba alisema mmomonyoko wa maadili ni moja ya sababu inayofanya nchi ichelewe kupata maendeleo.
“Kuna wizi na ubadhilifu mkubwa siyo tu kwa viongozi wa kisiasa, hasa kwa watendaji na watumishi wa kada za kati na chini. Watu wanawatizama wabunge na waziri pekee wakati wapo wahasibu wa wizara na halmashauri,” alisema.
Maadili
Alisema suala la maadili lipo katika sura mbili, ya kwanza ikiwa ni adhabu za kijamii na pili ni adhabu za kisheria.
“Katika adhabu za kijamii, ni lazima kujengeke utamaduni kwenye jamii wa kuwatenga, kuwachukia watu ambao wanapata kipato kisicho halali. Katika adhabu za kisheria, cha kufanya ni kuanzisha mahakama maalumu na kubadilisha sheria na kuyaweka kwa pamoja makosa ya rushwa na ubadhirifu kama makosa ya uhujumu uchumi,” alisema.
Mbunge huyo kijana alisema kwamba kitendo cha daraja linalotakiwa kujengwa kwa Sh800 milioni, lakini likajengwa kwa Sh200 milioni ni sawa na uhujumu uchumi na kusisitiza kuwa lazima adhabu ziongezeke.
“Kuna udhaifu wa kitaasisi katika kuchunguza na kuhukumu makosa ya rushwa. Kesi zinakaa miaka mingi bila kuisha na kumbuka kuwa wenye makosa hayo wana fedha na uwezo wa kutafuta mawakili wazuri, “ alisema, Aliongeza,
“Tunatakiwa kuweka tafsiri mpya ya nini hasa maana ya uhujumu uchumi na kuyapandisha daraja makosa hayo ili watakaobainika wafungwe miaka 30 jela au kufungwa maisha. Hizi taasisi za kuchunguza na kuhukumu makosa ya rushwa tunatakiwa kuzipanga upya.”
Alisema jambo jingine ni kuwa na mahakama maalumu za kusikiliza na kutoa uamuzi wa kesi za uhujumu uchumi.
“Kama mfumo wa uchaguzi unaingiza viongozi kwa rushwa au viongozi waliowahi kula rushwa, tusahau kabisa nchi hii kuondokana na rushwa. Hapo ni pa kupafanyia kazi sana,” alisisitiza.
Alisema licha ya kuwa nchi ina Sheria ya Matumzi ya Fedha za Uchaguzi, lakini imekosa usimamizi na kufafanua kwamba ni vyema sasa kuwa na taasisi mahususi kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa sheria hiyo.
“Kingine ni ujasiri wa kuwafuta uongozi na kuwapiga marufuku wagombea wanaogawa fedha ili kupata madaraka,” alisema.
Urais uchaguzi 2015
Akizungumzia nafasi yake ya kuwa rais wa Tanzania na mchakato wa CCM katika kuteua jina moja la mtu anayefaa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho alisema, “ Taasisi ya kujipanga ni CCM ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha inapambana na matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi na nafasi tulizo nazo kutozitumia kutafuta madaraka.”
Alisema watu wanaokamatwa wakitumia fedha kupata madaraka wanatakiwa kukatwa kabisa na chama hicho kuwania nafasi hiyo.
“Kiongozi anayetumia fedha kununua uongozi hawezi kupambana na rushwa hawezi kuleta mabadiliko ya aina yoyote katika nchi hii,” alisema.
Alisema chama hicho kinatakiwa kujihadhari na watu wa aina hiyo kwa sababu Uchaguzi Mkuu ujao ni muhimu kuliko chaguzi zote za miaka ya nyuma kwa sababu ni uchaguzi ambao utaamua mwelekeo wa Tanzania.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment