Kiongozi wa Kundi la Kudansi la Wakali Sisi lililoshinda katika Shindano la Dansi mia mia hivi karibuni Yasin Haji (Kulia) akiongea na wadau wa Sanaa waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kushoto ni Afisa Sanaa kutoka BASATA, Ernest Biseko.
Kundi la Wakali Sisi likionesha vitu vyeo kwenye Jukwaa la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii.
Mdau wa Sanaa kutoka Kikundi cha Sanaa za Majukwaani cha Binti Leo Lena Jackson akizungumza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii. Kushoto kwake ni mkongwe wa Sanaa za Maonesho nchini, Baraka Mpelemba maarufu kwa jina la Jangala na Mwenyekiti wa Chama cha Sanaa za Maonesho Nkwama Bhallanga.
Wadau wa Sanaa wakifuatilia burudani iliyokuwa ikitolewa na Kundi la Wakali Sisi kwenye Jukwaa la Sanaa mapema wiki hii.
Na
Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wameaswa
kuzingatia muda wanapohitajika kufanya onesho au kazi yoyote ya jamii ili
kuepuka kudharaulika na kuonekana watu wa hovyo na wasiyojali muda.
Rai hiyo imetolewa na Afisa
Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ernest Biseko wakati
akihitimisha Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki ambapo Kikundi cha Wakali
Sisi kilichoshinda kwenye onesho la dansi mia mia kilitoa burudani.
“Hakuna kitu muhimu na cha
msingi kwa msanii kama kuzingatia muda. Wasanii tumekuwa tukilalamikiwa sana kuchelewa
kwenye maonesho au kwenye shughuli za kijamii ambazo zinatutaka tuwahi. Hii
haipendezi” alisema Biseko.
Aliongeza kwamba, wadau
wengi wa Sanaa hawafurahishwi hata kidogo wanapoona msanii anafika kwa
kuchelewa kwenye shughuli hali ambayo imekuwa ikiwafanya wachukie na kuchukua
maamuzi ya kufanya vurugu.
Mdau mwingine wa Sanaa
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sanaa za Maonesho nchini Nkwama Bhalanga alisema
kuwa, wasanii wamekuwa wakidharaulika na kuonekana wa hovyo-hovyo kutokana na
kutokuzingatia muda hali ambayo inawafanya washindwe hata kufanya vizuri
jukwaani kutokana na muda mfupi wa maandalizi.
“Msanii lazima afike kwenye
tukio walau saa moja kabla ya onesho ili azoee mazingira lakini pia afahamu
wapi pa kubadilishia mavazi, kupumzika na kuoga baada ya onesho lake”
alisisitiza Bhallanga.
Awali katika Jukwaa hilo,
Kikundi cha kudansi cha Wakali Sisi ambacho wiki kadhaa zilizopita kiliibuka
kidedea kwenye onesho la Dansi Miamia kilitoa burudani ya kuvutia kwa wadau wa
Sanaa.
No comments:
Post a Comment