Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza na waandishi wa habari wa Zanzibar kwenye ofisi ndogo za mashirika ya Umoja wa Mataifa visiwani Zanzibar kuhusiana na mafanikio ya mradi wa kusaidia maendeleo nchini Tanzania (UNDAP) ulioanza mwaka 2011 na sasa ukiwa ukingoni. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues na kushoto ni Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Zaidi ya watoto 3000 waliokuwa wakikabiliwa na utapiamlo nchini Zanzibar sasa wapo katika hali nzuri baada ya Umoja wa Mataifa (UN)kwa kushirikiana na wadau wengine kufanikisha programu ya kusaidia kukabili utapiamlo mkali kwa watoto hao.
kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na waandishi wa habari uliofanyika hivi karibuni ambapo UN ilielezea mafanikio ya mradi wa kusaidia maendeleo nchini Tanzania (UNDAP) ulioanza mwaka 2011 na sasa ukiwa ukingoni.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez alisema kwamba Umoja huo ukiadhimisha miaka 69 ya uwepo wake imefurahishwa na maendeleo yaliyopatikana katika maeneo ambayo ilikuwa imejikita kusaidia kukabili umaskini,kuhakikisha utawala bora na kusaidia jamii.
Alisema pamoja na kuendeleza na juhudi za kukabiliana na utapiamlo katika visiwa vya Pemba pia Umoja huo umefurahishwa na hatua zilizofikia katika kukabiliana na vifo vya mama na mtoto na kusema ni wajibu kuhakikisha watoto hawana matatizo ya utapiamlo kwani wao ndio msingi wa taifa la sasa na lijalo.
Alisema hata hivyo upo umuhimu wa kuendelea na washirika wengine wa maendeleo kuona kwamba tatizo la utapiamlo la visiwa vya Pemba kwa watoto linamalizwa.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akielezea kufurahishwa kwake na Serikali Tanzania kwa kupigia hatua katika kutoa ajira nyingi kwa walimu kwenye mkutano huo. Kushoto ni Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.
Alisema pamoja na mafanikio hayo Umoja wa Mataifa unaendelea na ujenzi wa uwezo kwa baraza la wawakilishi ili kuhakikisha kwamba baraza hilo linawezesha kuwepo kwa sheria nzuri na bora na zinazotekelezeka ambazo hazikwazi kukua kwa demokrasia na ustawi wa jamii.
Aidha alisema kwa kuzingatia kwamba mwaka huu mwishoni kuna uchaguzi wa serikali za mitaa na pia uchaguzi mkuu mwakani pamoja na kura ya maoni ya katiba, Umoja huo unaendelea kufanyakazi na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar kwa kuiwezesha kitaalamu kuweza kufikisha elimu ya uraia kwa wananchi.
Aidha katika masuala ya utawala bora Umoja wa Mataifa unashirikiana na taasisi za sheria kwa ajili ya kufanya mabadiliko katika mfumo wa sheria za watoto ili kuwepo na usalama mkubwa kwa watoto hasa kutokana na utamaduni uliopo visiwani kwa sasa.
Aidha alisema kwamba yamepatikana mafanikio makubwa katika sekta ya tiba na kuzuia maambukizi ya Ukimwi na kuondokana na unyanyapaa.
Mwandishi wa gazeti la Mwananchi Zanzibar, Talib Ussi akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Aliwahimiza waandishi wa habari kuwa daraja la kuelezea mafanikio na pia changamoto zinazotokana na program za Umoja wa mataifa zilizolenga kusaidia maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
Alisema matokeo ya program ya kusaidia maendeleo ya Tanzania (UNDAP) ndiyo yatakayotumika kutengeneza UNDAP 2 ambayo inatarajiwa kuanza katikati ya mwaka 2016.
Katika mkutano huo ambapo waandishi walipata nafasi kubwa ya kuuliza masuala yanayohusu shughuli za Umoja wa Mataifa Zanzibar, Bara na duniani kwa ujumla Alvaro alizungumzia pia umuhimu wa Umoja wa Mataifa katika dunia inayobadilika.
Alisema pamoja na madhumuni ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, baada ya vita kuu ya dunia ya pili mwaka 1945 ya usalama na kujenga uchumi baada ya kuharibiwa na vita yapo palepale, mabadiliko katika utendaji kwa lengo hilo hilo la usalama na maendeleo ni dhahiri.
Alisema mathalani malengo ya millennia (MDGs) ambayo yalisanifiwa kwa lengo la kuleta maendeleo duniani katika demokrasia, utawala bora na ustawi wa jamii, bado yanatakiwa kuimarishwa kupitia mpango mpya wa maendeleo SDGs wenye lengo la kutokomeza umaskini uliotopea duniani ifikapo mwaka 2030.
Afisa Habari wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama akifafanua jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na mafanikio ya mradi wa kusaidia maendeleo nchini Tanzania (UNDAP) ulioanza mwaka 2011 na sasa ukiwa ukingoni.
Alisema ni matumaini yake kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana na UN katika kuhakikisha kwamba mafanikio katika MDGs yanaendelezwa na pia kukamilisha yale ambayo hayakufikiwa kwa lengo la kutokomeza umaskini uliotopea ifikapo mwaka 2030.
Alisema mafanikio ya UNDAP kwenye utawala bora, ustawi wa jamii na uondoaji umaskini na ukuaji wa uchumi nchini Tanzania, ni matokeo ya ushirikiano kati yake ya mamlaka mbalimbali nchini Tanzania na kwamba UN itaendelea kushirikiana na mamlaka hizo kuhakikisha maendeleo ya kuwezesha amani na usalama na ukuaji wa uchumi yanapatikana.
Naye Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama amesema lengo la kukutana na waandishi wa habari wa Zanzibar lilikuwa kuangalia mafanikio na namna ambavyo program za Umoja wa Mataifa katika visiwa vya Zanzibar zinafanyakazi.
Alisema kwamba shughuli za Umoja wa Mataifa visiwani humo zinaweza tu kujulikana kwa wananchi kwa kupitia waandishi wa habari ambao wanakuwa wanajua Umoja huo unafanya nini na wapi.
Mkutano kati ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa na waandishi wa habari wa Zanzibar ukiendelea.
Mwandishi wa habari wa TBC, Kulthum Ally, akiuliza swali kuhusiana namna Umoja wa Mataifa unavyoweza kuwasaidia Wanawake wa Zanzibar kupata nafasi za uongozi sawa na wanaume.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (waliokaa katikati), Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues (kulia) pamoja na Meneja wa Baraza la Habari Zanzibar, Suleiman Omar (kushoto) katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment