Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Licha ya taarifa mbalimbali kuonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wameajiriwa na sekta ya kilimo, hali ya sekta hiyo bado si ya kuvutia.
Wakulima wanasumbuliwa na changamoto nyingi, baadhi yake ni kulima chini ya kiwango kwa sababu si wataalamu wengi wa kilimo wanaowatembelea wakulima.
Hali kama hiyo iko kwenye kilimo cha mpunga, kiasi cha kusababisha wakulima kupata mpunga kidogo ukilinganisha na eneo wanalolima, miundo mbinu mibovu na ukosefu wa pembejeo.
Mbali na hayo sababu nyingine inayowakwamisha wakulima ni kukosa masoko ya uhakika ya mazao yao.
Matumizi ya teknolojia katika kilimo, inatajwa kuwa ni sababu kubwa kwani wengi wao wanalima kwa kusubiri mvua badala ya kujifunza namna ya kuhifadhi maji ya mvua.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji mpunga ukanda wa Afrika Mashariki, kwa kiwango cha tani milioni 1.18 ikiwa ni karibu asilimia 65 ya uzalishaji wote Afrika Mashariki, ikifuatiwa na Kenya na Uganda.
Tanzania ina wakulima zaidi ya 500, 000 wa mpunga, lakini wengi wao ni wadogo na kutokana na kukosa elimu na pembejeo wanalima mpunga usiokuwa na ubora.
Washauri wa masuala ya uchumi wanasema kinachohitajika ni kwa wadau mbalimbali wa kilimo kushirikiana na wakulima na Serikali katika kuimarisha kilimo.
Walichukulia mfano wa Shirika la Competitive African Rice Initiative (CARI) ambalo limeanzisha ushirikiano na tasisi ya Kilimo Trust na wadau wengine kwa kuwakusanya wakulima wadogo 30,000 wa mpunga na kuwafundisha namna ya kuboresha kilimo hicho.
Mbali na Tanzania kampeni hiyo ya kukuza uzalishaji wa zao hilo imehusisha nchi za Nigeria, Burkina Faso na Ghana.
Dk Mary Shetto, kiongozi wa kampeni hiyo iliyozinduliwa Jijini Dar es Salaam na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassani Mwinyi hivi karibuni anasema lengo la kampeni hiyo ni kuboresha zao la mpunga.
“Tunataka kuona kiwango cha mpunga unaozalishwa nchini kinaongezeka mara mbili au hata zaidi, hii inawezekana ikiwa tutatumia mbegu bora, teknolojia za kisasa na kuwasaidia wakulima masoko,” anasema.
Anataja lengo jingine kuwa ni kuwaelekeza wadau mahali pa kuwekeza kwa kuwakutanisha na wakulima na wasindikaji ambao kwa namna moja ama nyingine watanufaika na njia hiyo.
Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo, anasema Tanzania na Afrika kwa jumla zinatakiwa zijivunie bidhaa zinazopatikana kwenye nchi zao badala ya kuagiza za bei rahisi kutoka nje ya nchi.
Anafafanua kuwa pamoja na mchele kuwa mwingi na kubaki kwenye maghala, bado unaagizwa mwingine kutoka nje ambao wakati mwingine hauna ubora kama wa ndani.
“Changamoto iliyopo ni kwamba hatukubali kuwa tunaweza kufanikiwa kwa kutumia vya kwetu, bado watu wanaagiza mchele ambao baadhi yake hauna ubora kama wa kwetu,” anasema Mwinyi.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, anasema hapo awali walikuwa wananunua mahindi na mtama kutoka kwa wakulima, lakini hivi sasa wameanza pia kununua mpunga, na tayari wamekusanya tani 30, 000.
Chiza anasema wameanza kujenga maghala kwa ajili ya kuhifadhi mpunga, huku akifanya juhudi za kuhakikisha sekta binafsi inanunua ziada. Anasema amekwenda Kenya na Sudan Kusini huku akifanya mazungumzo na nchi za Kiarabu kwa lengo la kupata soko.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment