Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 27 October 2014

TAMKO LA SIKIKA KUHUSU UKOSEFU WA DAWA NA VIFAA TIBA KATIKA HOSPITALI, VITUO VYA AFYA NA ZAHANATI ZA UMMA NCHINI.


Sikika imesikitishwa na taarifa za hivi karibuni zinazoeleza kuwa na uhaba wa dawa na vifaa 
tiba muhimu katika vituo vya kutolea huduma vya umma nchini. Upungufu huu unasemekana kuathiri zaidi wananchi wasio na bima za afya.


Matatizo yanayosababishwa na uhaba wa dawa ni makubwa, kwani sio tu yanatishia uhakika wa huduma kwa mgonjwa anapokuwa katika kituo cha huduma za afya lakini pia 
yanapunguza ari ya kufanya kazi kwa watoa huduma. Aidha, matatizo haya pia yanaathiri 
ustawi wa jamii na mfumo wa huduma za afya nchini. Hali hii imeathiri wananchi wengi hasa wale wasio katika mfumo wa bima za afya na wale wenye bima zenye wigo mdogo. 
Nchini Tanzania, zaidi ya 80% ya wananchi hawako katika mfumo wowote wa bima za afya 
na inapotokea uhaba wa dawa na vifaa tiba wananchi hawa wamekuwa wakiathirika zaidi 
kwani inawalazimu kununua dawa kwa gharama kubwa na wakati mwingine hukosa kabisa. 
Hali hiyo huathiri utaratibu wa matibabu yao na kusababisha matabaka kati ya wale wasio 
nacho na walio nacho kwani walio nacho wamekuwa wakipata huduma za afya.
Uhaba wa dawa na vifaa tiba muhimu unaoendelea kwa sasa unasababishwa na ukosefu wa 
fedha pamoja na mlundikano wa madeni wa baadhi ya vituo vya huduma za afya, hususani 
hospitali kwa Bohari Kuu ya Dawa ya Taifa (MSD) ambao umepelekea MSD kusimamisha 
kutoa huduma katika vituo hivyo mpaka pale madeni hayo yatakapolipwa. MSD imefikia 
hatua hii ili kulinda mtaji wake ambao umekuwa ukizidi kutetereka kutokana na madeni 
yanayozidi kulimbikizwa kutoka serikalini pamoja na vituo vya kutolea huduma.
Baadhi ya vituo vilivyokumbwa na kadhia ya kukosa huduma MSD ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, hospitali za wilaya za Kiteto, 
Mpwapwa na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Sikika pamoja na vyombo vya habari, Wizara ya Afya na 
Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa na MSD zaidi ya Tsh Bilioni 90 (Ikiwa ni gharama ya 
ugomboaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa kutoka miradi misonge).
Aidha baadhi ya vituo vyenye madeni MSD ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili 
(8bn) hospitali ya wilaya ya Kiteto (38Mil) na nyinginezo.
Ongezeko la deni kwa MSD limekua likiathiri ufanisi wa bohari hiyo kutokana na ukweli 
kuwa MSD haifanyi kazi kwa faida na mtaji wa kujiendesha yenyewe umekuwa ukipungua 
siku hadi siku na hivyo kupelekea MSD kushindwa kufanya manunuzi kwa wakati, 
kusambaza na kuwa na akiba ya kutosha ya dawa na vifaa tiba. 
Kukua kwa deni la MSD kunasababishwa na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na makadirio ya 
mahitaji, upungufu wa pesa inayotolewa na serikali kuu tofauti na bajeti zinazopitishwa 
pamoja na ukosefu wa usimamizi na vipaumbele juu ya matumizi ya fedha zinazotokana na 
uchangiaji (cost sharing).
Pamoja na kwamba wananchi wengi huchangia pesa kutoka mfukoni, rekodi za afya 
zinaonesha kuwa, mchango wake katika vyanzo vya mapato ni mdogo. Hii inachangiwa na 
ukosefu wa taarifa sahihi za makusanyo na matumizi kutoka katika ngazi za halmashauri na 
vituo vya huduma za afya zinazoonesha kuwa miongozo ya ukusanyaji na matumizi ya fedha 
hizi haufuatwi.
Hivyo Sikika inapendekeza yafuatayo:
● Serikali itimize ahadi yake ya kutoa fedha zote za dawa na vifaa tiba muhimu na 
zitolewe kwa wakati sahihi.
● Serikali ipitie upya na kutekeleza miongozo ambayo itatoa mwelekeo juu ya 
ukusanyaji na matumizi ya fedha za uchangiaji hasa fedha za papo kwa papo.
Mwongozo uliopo unasema kwamba 67% ya ukusanyaji zitumike kwa ajili ya dawa 
muhimu na 15% kwa vifaa tiba na vitendanishi lakini ni halmashauri chache sana 
zinazofuata mwongozo huu.
● Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iongeze idadi ya watu katika 
mfuko wa bima ya afya ili kuongeza mapato. Hii itawezesha kulipia huduma hata 
kwa wale wachache watakaoshindwa kujiunga na mifuko ya bima za afya.
● Wizara ya Afya kupitia Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) iboreshe mifuko 
ya CHF na TIKA ili kuwawezesha wananchi kupata huduma nchi nzima.
● Vituo vya kutolea huduma za afya na Halmashauri vinapaswa kuhakikisha kuwa 
makusanyo ya fedha za uchangiaji yanatumika kwa mujibu wa miongozo, na kila 
wanapofanya manunuzi ya dawa nje ya MSD wahakikishe wanapata thamani halali 
ya pesa. 
● MSD itimize mahitaji ya dawa kwa vituo kwa asilimia 100. Hii itavisaidia vituo 
kuendelea kutoa huduma wakati wa uhaba kwani watakuwa wanatumia akiba waliyonayo.

IMESAINIWA:
Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz

No comments:

Post a Comment