Taarifa kwa Vyombo Vya
Habari, 30 Octoba 2014
Serikali isikwepe kulipa malimbikizo ya madeni MSD
kuokoa maisha ya Watanzania!
Sikika imesikitishwa na tamko lililotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, kuhusiana na kushindwa kwa vituo vya huduma za afya kununua dawa MSD
kutokana na kuongezeka kwa deni. Ni wazi kuwa waziri hajalipa tatizo hili uzito
unaotakiwa na kutambua kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza kupoteza maisha
kutokana na tatizo hili.
Sikika inatambua kuwa, mapato yatokanayo na uchangiaji katika huduma
za afya ni moja tu ya vyanzo vinavyotumika katika kuongeza upatikanaji wa dawa
na vifaa tiba nchini. Na pia inatambua kuwa chanzo hiki pekee
hakiwezi kuziba pengo kubwa la ufinyu wa bajeti ya dawa na vifaa tiba muhimu ambao
hauendani na mahitaji halisi. Kwa mfano, makadirio ya mahitaji ya dawa nchini
kwa mwaka wa fedha 2014/15 ni shilingi bilioni 500 lakini bajeti iliyopangwa na
kupitishwa ni shilingi bilioni 70.5 ambayo inakidhi mahitaji kwa asilimia 14 tu!
Sikika
inapenda kuikumbusha Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kuwa, takribani asilimia
75 ya wagonjwa wanaopata huduma katika
hospitali za Manispaa wapo katika kundi la msamaha wa huduma za afya. Kundi
hili linahusisha wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee, watu wenye
magonjwa sugu, watu wasiojiweza pamoja na watu wenye ulemavu. Hii inamaanisha
kuwa Serikali inategemea asilimia 25 tu ya wagonjwa wanaoweza kuchangia
huduma kama chanzo kikuu cha fedha za dawa zitokanazo na
uchangiaji. Serikali inatakiwa kuwajibika katika hili na sio kuwatupia mzigo
wananchi wachache.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii atambue kuwa, kuzitaka hospitali kulipa deni la MSD
kwa kutumia fedha za uchangiaji badala ya kutumia fedha hizo kununua dawa
kutokana na ufinyu wa bajeti, ni chanzo cha kuzifanya hospitali hizo
kuendelea kukopa zaidi na hivyo
kuendelea kukuza tatizo badala ya kutafuta suluhu. Tunamkumbusha kwamba hili ni
tatizo linalotokana mfululizo wa upangaji wa bajeti finyu kwa makusudi. Baadhi
ya hospitali hizi zimekuwa zikitumia fedha za uchangiaji kununua dawa lakini
bado zina madeni. Kwa hiyo, agizo la Waziri halitakuwa na tija katika kutatua
tatizo hili kwa sasa.
Hii sio mara ya kwanza kwa Wizara ya Afya kuzitaka hospitali kupeleka MSD
asilimia 50 ya mapato yao uchangiaji. Agizo hili limekuwa likijirudia tangu
mwaka 2012 bila ya kuwa na usimamizi katika utekelezaji na ufuatiliaji. Kwa
mfano, mwezi Julai 2014, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii aliziagiza hospitali
zote kupeleka MSD asilimia 50 ya mapato yao. Kwa kuwa agizo hili limekuwa likishindwa
kutatua tatizo la upatikanaji wa dawa, tulitarajia mbinu mbadala kutoka
serikalini.
Sikika ingependa pia kujua ni jinsi gani hospitali ya Taifa, za rufaa
na maalumu ambazo zinachangia asilimia kubwa ya deni (67%) katika kundi la
madeni ya vituo vya huduma za afya zitalipa deni hilo, kwani agizo la waziri lililenga
hospitali za wilaya na mikoa pekee. Vile vile, tungependa
kujua Wizara imeweka mipango gani katika kulipa deni lake ambalo ni zaidi ya
asilimia 70 ya deni lote ambalo MSD wanadai. Deni hilo la Wizara linatokana na
gharama za kugomboa, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za miradi misonge (vertical programs).
Mbali na hilo, tamko la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Umma la
tarehe 27 Oktoba 2014 linaeleza kuwa, Serikali imekuwa ikilipa Deni la MSD kwa
awamu. Hata hivyo, Waziri hakuweka wazi kwamba pamoja na kulipa kwa awamu, deni
limekuwa likiongezeka kwa sababu serikali inalipa kiwango kidogo na kukopa
kiwango kikubwa. Kwa mfano, mwaka 2013 deni lilikuwa kiasi cha Tsh. bilioni 76.4
lakini kufikia Septemba 2014 deni limekuwa na kufikia kiasi cha Tsh. bilioni 102
ingawa serikali ilifanya malipo ya Tsh. bilioni 10 .
Sikika ingependa
kupata ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mh.
Mwigulu Nchemba ambaye hivi karibuni alinukuliwa na baadhi ya magazeti akisema
kuwa kiasi cha fedha zilizotolewa kwa ajili ya dawa katika mwaka 2013/14
ilikuwa Tsh. bilioni 47 lakini ni Tsh. bilioni 7 tu ndizo zilitumika katika
kununua dawa. Sikika, pamoja na watanzania wote, ingependa kujua ni wapi fedha
hizi zimepelekwa na ni kwa sababu zipi hususan katika kipindi hiki cha uhaba wa dawa
na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya.
Sikika pia ingependa
kutoa ufafanuzi kwa umma kwamba misaada iliyositishwa na wafadhili ni kwenye
bajeti ya kuu tu (General Budget support)
na si kwenye mfuko wa pamoja wa sekta ya afya (Health Basket Fund). Kwa kipindi cha Julai-Septemba 2014, zaidi ya
Tsh bilioni 20 zilitolewa na wafadhili kwa ajili ya kusaidia halmashauri zote
nchini ambapo kwa kawaida, theluthi moja ya fedha hizo inapaswa kutumika kwa
ajili ya manununzi ya dawa na vifaa tiba muhimu.
Sikika inatambua
juhudi za serikali kujumuisha sekta ya afya katika mpango wa matokeo makubwa
sasa (BRN), ambao kwa kiasi unaweza kuchangia kupunguza uhaba sugu wa dawa na vifaa tiba katika vituo
vya huduma za afya vya umma. Hata hivyo, mpango huo utaanza kutekelezwa rasmi
mwaka wa fedha 2015/16, hivyo hauwezi kutatua tatizo la sasa la dawa. Waziri
atambue kwamba wagonjwa wanateseka na pengine baadhi kufariki kwa sababu ya
ukosefu huu wa dawa na vifaa tiba.
Mwisho, Sikika
inaitaka Wizara ya afya na Ustawi wa Jamii kuchukua hatua za haraka katika
kutatua tatizo hili sugu la ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya
huduma za afya vya umma. Uhaba wa dawa unawanyima wananchi kupata haki ya huduma
bora za afya ambazo huweza kusababisha vifo. Serikali inapaswa kulipa deni la
MSD na kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa dharura na haraka. Sio
haki kwa serikali yoyote kuacha wananchi wake wakiteseka ama kupoteza maisha
kutokanana sababu zinazoweza kuzuilika.
Mr. Irenei Kiria,
Executive Director of
Sikika,
P. O. Box 12183 Dar es
Salaam,
Tel: +255 222
666355/57, Fax: 2668015, Email: info@sikika.or.tz, Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Website: www.sikika.or.tz
No comments:
Post a Comment