Nahodha Lee Joon-seok
Waendesha mashitaka wa Korea Kusini wameomba adhabu ya kifo dhidi ya nahodha wa kivuko cha Sewol, ambacho kilizama mwezi April na kuua zaidi ya watu 300.
Waendesha mashitaka wamesema Lee Joon-seok, ambaye anashitakiwa kwa mauaji ya kutokusudia, alishindwa kutekeleza jukumu lake.
Wito wa waendesha mashitaka hao umekuja wakati wakikamilisha hoja zao katika kesi ilianza kusikilizwa mwezi Juni 2014.
Tukio la kuzama kwa kivuko cha Sewol kuliibua kilio nchini kote Korea Kusini, na shutuma nzito kwa serikali kwa kushindwa kusimamia shughuli za uokoaji.
Wengi wa waliokufa wakati kivuko hicho kilipozama walikuwa vijana wakiwa katika ziara ya masomo.
Waendesha mashitaka wamesema Kepteni Lee "aliondoka katika meli hiyo bila kuonyesha juhudi zozote za kuwaokoa abiria", shirika la AFP limeripoti.. "alitoa visingizio na kudanganya. Hajaonyesha kukiri kosa... Na kwa hiyo tunaomba adhabu ya kifo," wamesema.
Kepteni Lee anashitakiwa kwa kosa la kuua pasipo kukusudia kupitia uzembe wa makusudi.
Wakati wote wa kesi, Kepteni Lee mara kwa mara aliiambia mahakama kuwa alichanganyikiwa na hakuwa katika hali ya kawaida wakati ajali ilipotokea.
Waendesha mashitaka wamependekeza kifungo cha miaka kati ya 15-30 kwa wafanyakazi wengine 11 wa kivuko hicho ambao wameshitakiwa kwa makosa madogo wakati kesi imefikia mwisho katika mji wa kusini wa Gwangju.
Kivuko cha Sewol kilikuwa na abiria 476 kilipopinduka tarehe 6 April katika pwani ya kusini ya Korea Kusini.
Watu 172 ndio walionusurika katika ajali hiyo, kwa Kepteni Lee na wafanyakazi wake kuwa miongoni mwa watu wa kwanza waliokimbilia katika maboti ya kujiokoa.
Kulikuwa na kilio cha umma baada ya abiria walio nusurika kutoa ushahidi kwamba waliambiwa na wafanyakazi wa meli hiyo kubakia walipo hata wakati wanaona meli ikianza kuzama.
CREDIT: BBC/SWAHILI
No comments:
Post a Comment