| Katika picha ya pamoja (Picha zote kwa hisani ya BongoLeaks Blog)
Na Daniel Mbega, Iringa
MRATIBU wa Mradi wa Kuboresha
Mtandao wa Maeneneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (Spanest), Godwell Ole
Meing’ataki, amesema ujangili ni ujambazi na kwamba unapaswa udhibitiwe kama
ilivyo kwa uhalifu wa ujambazi ikiwa kweli kuna dhamira ya dhati ya
kuutokomeza.
Akizungumza
katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maandamano ya Tembo na Faru duniani,
ambayo kimkoa yamefanyika mjini Iringa leo hii, Ole Meing’ataki amesema
ujangili wa tembo na faru haupaswi kufumbiwa macho na akatoa rai kwa vyombo vya
dola na Watanzania kwa ujumla kuunganisha nguvu kuwashughulikia wahusika.
“Wahusika
wa ujangili ni Watanzania wenzetu, ndugu zetu na majirani zetu, baadhi
yawezekana wananchi wanawajua, hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha
vitendo hivi vinakomeshwa ili maliasili hizi, ambazo ni urithi wa bure kutoka
kwe Mungu, ziweze kuwanufaisha wananchi wote,” alisema.
Akaongeza:
“Pembe za ndovu na faru hazipatikani mijini, haziuzwi Iringa wala Dar es
Salaam, zinapatika porini – vijijini, na wahusika wote wanatumia barabara zetu,
bandari zetu na hata viwanja vyetu vya ndege kusafirisha, lakini wanashirikiana
na Watanzania wenzetu kwa ubinafsi tu.”
Ole Meing’ataki
amesema, vijana walioko vijijini, ambao mara nyingi ndio wanaohusika na uuaji
wa tembo na faru, wanapaswa kupatiwa elimu na kutambua madhara ya ujangili na
kujua umuhimu wa maliasili hizi kuwanufaisha wote, hivyo Spanest kwa
kushirikiana na wadau wengine wataendelea na program zao za kutoa elimu
vijijini ili maliasili hizo zilindwe kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunatambua
kwamba kuna tatizo la ajira nchini na duniani kwa ujumla, lakini ujangili usiwe
mbadala wa ajira hizo kwa sababu kadiri wanyama hawa adhimu wanavyouawa Taifa
linapoteza rasilimali na mapato kwani hatutaweza kupata wageni ambao ndio
wanaotuingizia fedha za kigeni,” amesema.
Spanest ni
mradi wa kuimarisha utalii nchini ambao uko chini ya udhamini wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mfuko wa Kimataifa (GF) pamoja na Shirika
la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) ambapo linafanya shughuli zake katika
mikoa mitatu ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania – Iringa, Njombe na Mbeya.
Maandamano
na maadhimisho hayo yameandaliwa na kuratibiwa na shirika binafsi la Wildlife
Connection lenye makao yake makuu Tungamalenga wilayani Iringa, ambapo limeshirikisha
wadau mbalimbali wa maliasili na utalii mkoani humo.
Mkuu wa
Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amesema lengo la maandamano hayo ni
kuujulisha umma juu ya tatizo la mauaji yanayowakabili wanyama hao ambao ni
muhimu katika uhifadhi na utalii.
Katika hotuba
yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi, Adam Swai, Dk.
Ishengoma amesema faida ya wanyamapori nchini ni kubwa hasa kupitia sekta ya
utalii ambayo inachangia takriban 17% ya pato la Taifa na kuingiza zaidi ya 21%
ya fedha za kigeni.
“Mkoa wa
Iringa una bahati ya kuwa na hifadhi za taifa zenye tembo wengi hasa Ruaha na
Udzungwa, hivyo maandamano haya yanafanyika kwa kutambua hali halisi ya
ujangili katika hifadhi hizi na pia kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau
mbalimbali pamoja na wananchi katika kukabiliana na ujangili,” amsema.
Amewapongeza
wadau wanaojishughulisha na utalii, uhifadhi na utafiti kama vile Wildlife
Conservation Society, Carnivore Project, HALI Project, Southern Tanzania
Elephant Research Project, WWF, PAMS Foundation, Friends of Ruaha na wengineo
kwa jitihada kubwa wanazozifanya na kuwataka waendelee vivyo hivyo.
Aidha,
aliwapongeza Wildlife Connection walioandaa na kuratibu maandamano hayo akisema
hiyo imewapa nafasi ya kuungana na jumuiya ya kimataifa katika kupiga vita
ujangili wa tembo na faru.
Awali,
Naibu Mkurugenzi wa shirika la Wildlife Connection, Julius Mbuta, alisema pamoja
na jitihada zinazofanywa na serikali katika kutokomeza ujangili, lakini mapambano
dhidi ya ujangili yanapaswa kuhusisha wadau wote wakiwemo wananchi wa kawaida.
“Sisi
katika kupambana na ujangili tumekuwa tukiwaelimisha wananchi hasa wanaozunguka
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuhusu umuhimu wa kuwatunza wanyama hao ambao ni tunu
kutoka kwa Mungu na wanatuletea faida kubwa kama taifa,” alisema. “Tunafanya
hivyo kwa kushirikiana na uongozi wa Hifadhi ya Jamii ya Mbomipa na tumeanzisha
maktaba mbili katika eneo hilo ili wanafunzi wapate fursa ya kujisomea na
kujifunza umuhimu wa kuhifadhi maliasili.”
Ameongeza kwamba,
katika kukabiliana na migogoro ya wananchi na wanyama, hasa tembo, wanaovamia
makazi na mashamba, wameanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki ambapo hutandaza
mizinga mipakani ili kuwazuia tembo wasivamie mashamba na makazi.
“Tumeunda
kikundi cha watu watano na tumeanza na mizinga 120. Kwa kuwa tembo anaogopa nyuki,
tunaamini ufugaji huu wa nyuki utasaidia kuwauia tembo wasilete uharibifu kwa
jamii, lakini wakati huo huo wanajamii wakipata faida katika mradi huo,”
alisema.
Mbunge wa
Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii, amesema suala la kulinda maliasili ni la kila Mtanzania
kwa mujibu wa Katiba na akawataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika
kupambana na kuwafichua majangili wote.
Amesema maliasili
zinakuza uchumi wa taifa na kwamba mapambano dhidi ya ujangili hayapaswi kuchukuliwa
kisiasa kwa kuwa yatadidimiza uchumi.
“Siasa
haiwezi kutenganishwa na uchumi, maliasili hizi ndizo zinazokuza uchumi wetu
kwa kuleta fedha nyingi za kigeni, leo hii kama tusingekuwa na tembo kamwe hawa
Wazungu wasingeweza kuja kwetu, lazima tushikamane pamoja kuutokomeza ujangili,”
alisema.
Hata hivyo,
pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na ujangili,
amesema nivyema elimu ikatolewa kwa Watanzania wote huku wananchi wa vijijini
wakipewa kipaumbele kwani ndio wahusika na washirika wakubwa.
“Wanaoua
tembo ni Watanzania wenzetu – hata kama wanatumwa na Wachina. Hakuna Mchina
hata mmoja anayekwenda porini kuua tembo wetu, vijana wetu ndio wanaoshika magobore,
hivyo lazima elimu ikatolewa kwao kujua umuhimu wa kuwatunza wanyama hawa,”
alisema.
Aidha,
aliitaka serikali kutekeleza Azimio la Kimataifa kuhusu Mpango wa Kulinda Tembo
lililotolewa jijini London, Uingereza mwezi Februari 2014 ambalo liliagiza
ufanyike ukaguzi wa wazi wa meno ya tembo na kutambua meno yaliyopatikana
kihalali na kinyume cha sheria, kisha kuyateketeza hadharani yale
yaliyopatikana kiharamu kama wanavyofanya China, Hong Kong na Vietnam.
“Iliagizwa
pia kwamba, shehena zote za meno ya tembo kuanzia gramu 500 lazima zipimwe
vinasaba (DNA) pindi zinapokamatwa ili kujua wapi zilikotokea na hivyo kuongeza
udhibiti, jambo ambalo halijafanyika mpaka sasa,” alisema.
Naye Muikolojia
wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Paul Banga, amesema Mfumo- Hifadhi ya Taifa Ruaha
ni sehemu ya mfumo
ikolojia wa Rungwa-Kizigo –Muhesi ambao unachukua eneo la kilometa za mraba
45,000 na hifadhi yenyewe – ambayo ndiyo kubwa zaidi Tanzania na Afrika
Mashariki kwa ujumla – ina kilometa za mraba 20,226.
Hifadhi
hiyo ni ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Hifadhi ya Kafue ya Zambia. Ukubwa
wa Hifadhi ya Ruaha ni zaidi ya 2/3 (theluthi mbili) kwa ukubwa wa nchi ya
Ubelgiji ambayo eneo lake la mraba ni kilometa za mraba 30,528! Rwanda yenye
eneo la ukubwa wa kilometa za maraba 26,338 na Burundi (27,834km2) zinaizidi
kidogo hifadhi hii wakati ambapo ina karibu ukubwa sawa na Jimbo la New Jersey
la Marekani, ambalo eneo lake ni kiliometa za mraba 22,608.
Banga amesema
idadi ya tembo katika hifadhi hiyo inaendelea kupungua kila mwaka ambapo kwa
takwimu za mwaka 2013, wanyama hao wamebaki takriban 25,000 kutoka idadi ya
awali ya 31,000.
“Ingawa
ndiyo hifadhi ya pili Afrika kwa kuwa na tembo wengi, lakini idadi inapungua
sana na hali inatisha,” alisema.
|
No comments:
Post a Comment