Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 4 October 2014

KUNA HAJA YA KUINGIA ‘MKATABA WA AMANI’ NA MAJANGILI WA TEMBO NA FARU!


Mizoga ya Faru na Tembo iliyouawa na majangili

“NISEME nini, niseme nini? Sina la kusema! Walipewa madaraka, wakalala usingizi, walipewa madaraka, wakayatumia vibaya… sasa Tembo wanateketea…”

Naam. Nimeamua nianze na kibwagizo cha wimbo wa nguli wa Bongo Beats, marehemu Ramazan Mtoro Ongalla, maarufu kama Dk. Remmy Ongalla, usemao ‘Niseme Nini?’ alioutoa mwaka 1991 akiwa na bendi yake ya Super Matimila.
Nakumbuka wimbo huu ulipotoka kwa mara ya kwanza ulipigwa ‘BAN’ ya nguvu na Serikali ya Awamu ya Pili usisikike redioni, wakati huo Radio Tanzania (RTD) pekee, kwa madai kwamba ulikuwa ‘ukiwasimanga’ viongozi wa serikali.

Ni katika kipindi ambacho Rais Alhaj Ali Hassan Mwinyi alikuwa ametoa ruksa, rasilimali za taifa nazo hazikubaki salama kwa sababu wapo baadhi ya maofisa wa serikali wa ngazi za juu waliotumia fursa hiyo kujinufaisha.
Nyara za Serikali zilihamishwa kinyemela kupelekwa nje ukiwemo udongo ambao ulisafirishwa kupelekwa Arabuni kwa ajili ya kutengenezea bustani kutokana na maeneo mengi ya huko kuwa ya jangwa.
Dk. Remmy alipotoa wimbo huo hakuwa amekurupuka, alikuwa anaona, kama Watanzania wengine walivyokuwa wanaona lakini walikosa mahali pa kusemea kutokana na kutokuwepo ‘uhuru wa habari’ na hata uhuru wa kujieleza unaotajwa kwenye Katiba yenye viraka haukujulikana.
Kwahiyo, hata serikali ilipopiga ‘ban’ wimbo huo hakuna aliyepiga kelele japokuwa wengi walishangilia kuona jamaa ‘wameumbuliwa’. Remmy akauhariri wimbo huo na kuurekodi tena, hivyo unaosikika sasa siyo ule niliousikia kwa mara ya kwanza nikiwa Pugu sekondari pamoja na akina Dk. Kitila Mkumbo.
Leo hii tumeazimisha Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Mauaji ya Tembo na Faru lakini ni miaka 23 baadaye, ambapo zimeibuka taarifa kuhusiana na vigogo wengi, wakiwemo wafanyabiashara na makada wa vyama, kuhusika katika biashara ya meno ya tembo.
Vigogo hawa wamejiimarisha, wana fedha, wanaweza kununua silaha za kivita ili kuwapopoa tembo. Kwa kifupi, hawa jamaa ni madaktari bingwa wa meno ya tembo. Wanang'oa bila ganzi na hawajali hasara ambayo taifa linapata.
Soko lao huko Mashariki ya Mbali, hususan China, linazidi kupanuka na wanaingiza maelfu kwa mamilioni ya dola.
Kwa vile maofisa wa serikali katika idara nyeti zinazohusiana na ulinzi wa maliasili zetu pamoja na zile zinazoruhusu mizigo isafirishwe nje ya nchi wametopea kwenye rushwa, hawa majangili wanaendelea kutanua kwa kadiri watakavyo, hakuna wa kuwazuia.
Na kwa bahati mbaya, kama inavyoelezwa na vyombo vya usalama vya kimataifa, fedha zinazopatikana kwenye bishara hiyo 'haramu' ya meno ya tembo ndizo zinazofadhili harakati chafu katika nchi mbalimbali duniani, Tanzania ikiwa miongoni mwao.
Vikundi vya kigaidi vinapata fedha za aina hii ili vijiendeshe! Tembo wa Afrika (Loxodonta africana spp) wanazidi kuteketea.
Ni kwa msingi huo basi, wanajamii wenzangu, nimekuja na hoja au maoni au mapendekezo, kwamba ili tuwaokoe tembo wetu, pamoja na wanyamapori wengine wanaopopolewa na hawa majangili, Tuingie Mkataba wa Amani na Majangili hawa!
Tanzania ndiyo inayoongoza kwa sasa kwa ujangili wa tembo kuliko nchi yoyote Afrika. Wahusika, yawezekana kabisa, wanajulikana na 'tunawakumbatia'.
Sasa vita hii ya ujangili inaweza kumalizwa ama kwa kuingia mkataba wa amani na majangili kama suluhu ya kumaliza tatizo kwa vile juhudi zote za kimataifa zinaonekana kukwama.
Mbinu zote zilizopo zinaonekana za kizamani: udhibiti mkubwa wa biashara hiyo ya meno ya tembo, utaifishaji na kuharibu shehena inayokamatwa, uwekezaji mkubwa katika jitihada za kudhibiti ujangili, adhabu kali - ikiwemo kifo katika nchi nyingine kwa majangili, mawakala wao na hata wanunuzi.
Mbinu za kawaida hazijafanikiwa huko nyuma, zinaonekana hata sasa haziwezi kufanikiwa kwa kiwango kikubwa, na yawezekana zisifanikiwe hapo baadaye.
Pengine, mkataba wa amani unaweza kusaidia, kinyume chake tutajikuta tukibaki na picha kwenye vitabu kwamba tulikuwa na mnyama mmoja anaitwa tembo, ambaye alifanya binadamu wengi kujenga nyumba za 'mgongo wa tembo' - ziwe za nyasi au bati!
Nawasilisha wadau.

NB: Makala haya yamehaririwa, lakini niliwahi kuyatoka kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wa Mabadiliko, Juni 20, 2013.

No comments:

Post a Comment