Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 5 October 2014

HALIMA MDEE ALIPOTIWA MBARONI NA POLISI


Mwenyekiti wa BAWACHA, Halima Mdee akisukumwa kuingia ndani ya 'Difenda' pamoja na wanachama wengine. PICHA|RAFAEL LUBAVA/THE CITIZEN 
Viongozi tisa akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee, wamekamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay baada ya kufanya maandamano yasiyo halali.

Viongozi hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho (Jumatatu) kwa ajili ya kusomewa mashitaka.

Kukamatwa kwao kulikuja muda mfupi baada ya maandamano yao yaliyoanzia kwenye ofisi za baraza hilo, Kinondoni, jijini Dar es Salaam kuelekea Ikulu kwa lengo la kumwomba Rais Jakaya Kikwete asitie saini Rasimu inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK).


Hata hivyo, maandamano hayo yalizingirwa na polisi na wote hao kukamatwa pindi walipofika eneo la makaburi ya Kinondoni, maarufu kama makaburi ya FM.

Viongozi wengine waliokamatwa na vyeo vyao kwenye mabado ni Martha Charles (Katibu wa Mdee), Rose Mushi (Diwani Viti Maalum Kinondoni), Edward Simbeye (Mratibu wa Uhamasishaji Baraza la Vijana Chadema,Taifa) na Sophia Phanuel (mlinzi wa Chadema).

Wengine ambao vyeo vyao havijapatikana ni Eauty Mmari, Anna Linjewelle, Remina Peter na Mwanne Kassim.

MAANDAMANOMaandamano hayo yaliyoanza saa 4.00 asubuhi yakitokea katika ofisi za baraza hilo kuelekea Ikulu, yalikolezwa na mabango yaliyosomeka "Rais usipochukua hatua wananchi tutalazimisha uchukue hatua",  lingine lilisomeka "Katiba siyo mali ya CCM" na "Hakuna Katiba isiyolinda rasilimali za taifa" .

Hata hivyo, mita chache tu kutoka ofisini hapo maeneo ya makaburi ya FM Kinondoni,  kikosi maalum cha polisi kilichokuwa kimetanda eneo hilo kwa ajili ya kudhibiti maandamano hayo, kiliwatawanya kwa kuwamwagia maji ya kuwasha.

Kufuatia kitendo hicho, Mdee ambaye alikuwa akiongoza maandamano hayo pamoja na viongozi wenzake, walitawanyika kila mmoja na njia yake.

Katika purukushani hizo, Mdee na wenzake kadhaa walikimbilia katika nyumba iliyokuwa mita chache kutoka makao makuu ya Chadema kwa ajili ya kujificha.
Hata hivyo, polisi waliokuwa wamevalia magwanda walivamia nyumba hiyo na kuwatoa.

NIPASHE Jumapili lilishuhudia  jeshi hilo likitekeleza kazi yake kwa kumtandika virungu Mdee na wenzake hadi walipopanda gari lao aina ya Defender lililokuwa limeegeshwa eneo hilo tayari kuwafikisha kituo cha polisi.

Pamoja na kuwapiga virungu waandamanaji hao, gazeti hili lilishuhudia uharibifu uliofanywa kwenye kibanda kilichokuwa nje ya nyumba waliyokuwa wamejificha viongozi kwa kuvunjwa na polisi hao.

MKUTANOKabla ya viongozi hao kukutana na adha hiyo,  walifanya mkutano na waandishi wa habari, ambapo mwenyekiti huyo aliwaeleza kuwa maandamano hayo yameruhusiwa na Rais Kikwete.

Alisema Rais Kikwete amewaalika Ikulu na wanashangaa kwa nini polisi wanawaingilia.

“Tulitoa taarifa siku tatu nyuma, lakini polisi wametujibu jana jioni (juzi), Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Sulemain Kova ametoa sababu kuwa maandamano hayapo kisheria,’ alisema.

Mdee alisema kuwa, lengo la maandamano ni kupinga Katiba inayopendekezwa na BMK ambapo vipengele muhimu vimeondolewa.

DEFENDER  ZATANDAGazeti hili lilishuhudia magari ya polisi aina ya defender yakiwa yametanda eneo hilo majira ya saa 2:00 asubuhi huku askari polisi waliokuwa na silaha aina mbalimbali wakiwa wanazunguka mitaa ya Kinondoni na jirani na ofisi za baraza hilo.

Baadhi ya magari ya polisi yaliyoonekana kurandaranda maeneo hayo ni pamoja na PT 1686 na KX 06 E.

MWITIKIO
Hata hivyo,  mwitikio wa wanachama katika maandamano hayo haukuwa mkubwa, huku baadhi ya wananchi wakionekana kukaa pembeni kushuhudia kitakachotokea.

OYSTERBAY POLISIBaada ya viongozi hao tisa kufikishwa kituoni hapo, baadhi ya wafuasi walifika na kusababisha purukushani kati yao na polisi.

Gazeti hili lilishuhudia eneo la kuingilia kituoni hapo likiwa limefungwa kamba maalum ili kuzuia watu au magari kuingia ndani ya kituo hicho huku polisi wenye silaha za moto wakiwa wameweka ulinzi.

Wafuasi hao waliingia kituoni hapo wakiwa na magari tofauti ambapo walishuka na kuanza kujibizana na polisi.

Kufuatia hali hiyo, defender lililokuwa limebeba maji ya washawasha liliwasili kujiweka tayari na hatua yoyote ambayo ingejitokeza.

Askari aliyetambuliwa kwa jina moja la Tille alitoa maagizo kwa wafuasi hao waondoke eneo hilo, huku akiwafuata waandishi wa habari waliokuwa wamejitenga na kundi hilo na kuwataka waelekee  walikotaka wana-Chadema waende.

Hata hivyo, kitendo hicho kilipingwa na askari mwingine ambaye alisema waandishi wa habari wanafanya kazi pamoja nao, hivyo sio vyema kuelekea huko kwa kuwa ni eneo hatari.

Baada ya wafuasi hao kutii amri hiyo walikaa upande wa pili wa barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kuimba nyimbo mbalimbali huku wakiigiza jinsi askari wanavyotembea wakiwa kwenye gwaride.

Katibu wa Chadema Mkoa Kinondoni, Henry Kileo, alitoka ofisi za kituo hicho na kuwaeleza wafuasi hao kuwa, mpaka muda huo (saa 7:40 mchana), Mdee na wenzake walikuwa wamekataa kuhojiwa hadi mawakili au ndugu wa karibu watakapofika kituoni hapo. Hatimaye wakili Peter Kibatara, aliwasili kituoni hapo.

POLISI WAONGEANaibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Simon Siro, alithibitisha kukamatwa kwa viongozi tisa na kueleza kuwa baada ya mahojiano waliachiwa kwa dhamana.

Aidha alisema watafikishwa mahakamani kesho kwa kosa la kufanya maandamano yasio halali.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment