Unaweza kuwatambua hawa? Kushoto kabisa mwenye gitaa ni Felix Pepe Manuaku Waku, anafuatiwa na N'Yoka Longo Mvula na kulia ni bwana mdogo Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba 'Papa Wemba'.
N'Yoka Longo (wa pili kushoto) na Pepe Manuaku Waku wakiwa na mchezaji mahiri wa AS Vita Club na timu ya taifa ya Zaire (Les Leopards) wakati huo Emmanuel Kakoko Etepe. Kushoto ni mwandishi akiwahoji.
Na Daniel Mbega
KAMA siyo kutoka ubavuni mwake, basi bendi
nyingi, kama si zote zinazotamba nchini Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia) kwa
sasa, zimeasisiwa na wanamuziki ama waliotoka ndani ya bendi hii au katika
bendi zilizoanzishwa na wakali waliopata kuipigia.
Naam. Hiyo ndiyo Zaiko Langa Langa, bendi kongwe
nchini Congo kwa sasa ambayo bado inaendelea kudunda licha ya wimbi kubwa la
kuhamwa na wanamuziki mahiri pamoja na ushindani uliopo hivi sasa.
Kimsingi twaweza kusema Zaiko Langa Langa ni chuo
cha muziki katika Congo, kwa sababu bendi nyingi zinazotamba hivi sasa, ambazo
zimeanzishwa kuanzia miaka ile ya 1970, ni matunda yake.
Ukitaja wanamuziki nyota wa nchini Congo kuanzia
Papa Wemba, Bozi Boziana, Dindo Yogo, Evoloko Ley Ley ‘Joker’, Defao Matumona,
Koffi Olomide, na wengineo wote lazima utapata chimbuko lao kutoka kwenye shina
la Zaiko Langa Langa, ambayo mpaka sasa bado ingali inaongozwa na mkongwe
N’Yoka Longo Mvula.
Bendi nyingi kama Isifi Lokole, Yoka Lokole, Viva
la Musica, Langa Langa Stars, Zaiko Familia Dei, Choc Stars, Le Anti Choc, Le
Grand Zaiko Wawa, Quartie Latin na nyinginezo nyingi zimetoka kwenye chimbuko
la Zaiko ambayo sasa inajulikana kama Zaiko Langa Langa Nkolo Mboka, yaani
‘Wakuu wa Mji’.
Siyo ajabu kuona leo hii kuna idadi kubwa ya
bendi zilizotokea ubavuni mwa Zaiko Langa Langa zikijiita ‘Ukoo wa Langa Langa’
(Clan Langa Langa). Bendi hizo ni Isifi Lokole iliyoanzishwa na Papa Wemba,
Bozi Boziana, Evoloko Jocker na Mavuela Somo; Yoka Lokole iliyoanzishwa na Papa
Wemba, Bozi Boziana na Mavuela Somo; Grand Zaïko Wa Wa iliyoanzishwa na Felix
‘Pepe’ Manuaku Waku aliyeungana na Shimita El Diego na Djo Poster; Viva La
Musica iliyoanzishwa na Papa Wemba akiwa na Emeneya Mubiala na Theodore Djangi
Dindo Yogo; Choc Stars iliyoanzishwa na Bozi Boziana, Tshimpaka Roxy na
kuungana na akina Ben Nyamabo, Carlito Lassa, na Defao Matumona; L'Orchestre
Anti-Choc iliyoanzishwa na Bozi Boziana akiungana na Deyesse Mukangi, Jolie
Detta, Dodoli, Walingonda, Fifi Mofude, na wengineo; Langa Langa Stars
iliyoanzishwa na Verckys Kiamuangana Mateta, Evoloko Jocker, Bozi Boziana,
Tshimpaka Roxy, Emeneya Mabiala na Djo Mali; Zaiko Langa Langa Familia Dei ya
Lengi Lenga, Ilo Pablo, Bimi Ombale, Beniko Popolipo, Petit Poisson, na Djimi
Yaba; Zaïko Langa Langa Nkolo Mboka yenyewe chini ya N'Yoka Longo, Meridjo,
Oncle Bapius, Zamuangana, Nono Atalaku, Mbuta Matima, Malage de Lugendo, Adamo
Ekula, Baroza, na Shiro Shiro; Zaiko Universel ya Meridjo na Oncle Bapius
Muaka; Langa Langa Rénové ya Evoloko Jocker; Basilique Loningisa iliyoanzishwa
na Bimi Ombale; Etumba na Ngwaka Aye iliyokuwa chini ya Dindo Yogo; Les Quatros
de Langa Langa ukiwa ni muungano wa Papa Wemba, Evoloko, Bozi Boziana na Gina
Efonge; Les Stars de Zaiko (sasa inaitwa Zaikas Kolo Mboka) ikiwa chini ya
Adamo Ekula, Petit Poisson, Tshanda na Papy Cocaine; na Clan Petrole ambapo
nyimbo nyingi zimerekodiwa kupitia majina ya makundi tajwa hapo juu
yanayowakilisha Ukoo wa Langa Langa.
KUZALIWA KWAKE
Watu wengi wamekuwa wakikosea historia ya Zaiko
Langa Langa, kwamba ilianzishwa mwaka 1970. Hii siyo kweli kabisa.
Bendi hii mwaka huu imetimiza miaka 45 tangu
kuanzishwa kwake. Ilianzishwa rasmi Desemba 24, 1969 jijini Kinshasa
ikijulikana kama Orchestra Zaiko, ambayo ni kifupi cha maneno ya Kilingala ya
Zaire ya bankoko (Zaire ya babu zetu). Neno Langa Langa lina utata kidogo:
kwenye wavuti ya bendi linamaanisha
‘utukufu’, lakini nilipata kuongea na N’Yoka Longo jijini Dar es Salaam wakati
fulani akasema maana ya Langa Langa ni ‘Maji Maji’ (kwa maana nyingine
walichukua jina la Mto Zaire). Hivyo kirefu chake ama tafsiri yake halisi ni
Zaire ya mababu zetu ni ya maji maji!
Wakati huo muziki wa Congo ulitawaliwa zaidi na
bendi za African Jazz ya Joseph Athanase Tchamala Kabaselleh ‘Le Grand Kalle’,
African Fiesta ya Nicolas Kassanda wa Mikalay maarufu kama Dk. Nico, Tout
Puisant Orchestre Kinnie Jazz (TP OK Jazz) ya L’Okanga La Ndju Pene Luambo
Luanzo Makiadi Franco na hata African Fiesta National ya Pascal-Emmanuel
Sinamoyi Tabu, almaarufu Tabu-Rey Rochereau, aliyoianzisha baada ya kutengana
na Dk. Nico na mwaka 1970 akaibadili jina na kuiita Orchestre Afrisa
Intanatinale.
Waanzilishi wa Zaiko Langa Langa walikuwa
wanamuziki ambao baadhi walikuwa wanapigia bendi ndogo ndogo tu za mitaani na
wengine walikuwa wanafunzi. Hawa si wengine bali ni mpiga conga maarufu D.V.
Moanda, ambaye jina lake halisi ni Vital Moanda-di Veta (Alifariki mwaka 1984
jijini Kinshasa), Marcelin Delo, Henry Mongombe, Olemi Eshar-Eshar dem'belina,
Andre Bita, Mavuela ‘Somo’ Simeon, Evoloko Lay Lay ‘Joker’, Teddy Sukami, Oncle
Bapius aliyekuwa akipiga bass, Zamuangana Enock le meilleur, baba ya wapiga
solo wa kizazi kipya Congo Felix Manuaku Waku (pia alijulikana zaidi kama Pépé
Fely), na N'Yoka Longo Mvula, anayelikana kama Jossart, ama Vieux Mbombas,
lakini maarufu zaidi kama N’Yoka Longo, ambaye asili yake ni Angola. Hawa
walikuwa wakipiga soukous. Katika upande wa pop, muziki uliokuwa ukifungua
pazia katika shoo zote za bendi hiyo, kulikuwa na Bimi Ombale, Mbuta Matima
Zephirin na Mashakado Mbuta.
Moanda, Mongombe, Marcelin, Waku, N’Yoka Longo na
Andre Bita walitokea kwenye bendi ya mtaani iliyojulikana kama Bel Guide
National. Wote hawa walikuwa wanafunzi wakitokea katika familia za matajiri
jijini Kinshasa.
Baadaye mwaka huo bendi hiyo ikamchukua bwana
mdogo mwenye miaka 19, ambaye alikuwa anaimba kwaya kanisani. Huyu si mwingine
bali ni Jules Shungu Wembadia Pene Kikumba, maarufu kama Papa Wemba.
Itaendelea...


No comments:
Post a Comment