Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 21 October 2014

ALI AMEIR MOHAMED ATAKA RAIS AJAYE AWE KAMA MKAPA

Ali Ameir Mohamed
Na Theodatus Muchunguzi
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, amesema mtu sahihi anayepaswa kuwa rais ajaye wa Tanzania anatakiwa kuwa na sifa zilizoainishwa na CCM wakati wa kumpata aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, huku akimmininia sifa kwamba alikuwa kiongozi makini.

 
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake Donge, visiwani Zanzibar, Ameir ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Habari, alisema Mkapa alikuwa na sifa zilizoainishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 1995, anazoamini kwamba bado zinahitajika katika uchaguzi ujao na zaidi ya hayo, vilevile (Mkapa) alikuwa ni makini, mchapakazi na asiye na ubinafsi.
 
Ameir alizitaja baadhi ya sifa zilizoainishwa na CCM wakati Mkapa alipopata nafasi ya kugombea na mwishowe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni, elimu ya chuo kikuu, uwezo wa kuongoza na uzoefu wa kutosha.
 
“Tena sifa hizo za Chama Cha Mapinduzi zilipowekwa na mimi nilikuwapo… kwa hiyo sipingani nazo. Bado naona zinafaa,” alisema Ameir, akiongeza kuwa ni sifa hizo, ikiwamo ya elimu ya chuo kikuu, ndizo zilizochangia kumuondoa Augustine Mrema aliyeihama CCM na kujiunga na chama kikuu cha upinzani wakati huo cha NCCR-Mageuzi. Hivi sasa Mrema ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP). 
 
Ameir alimsifu Mkapa, akisema anamfahamu vizuri rais huyo wa awamu ya tatu kwa vile alifanya naye kazi wakati walipokuwa waandishi wa habari na baadaye kuteuliwa naye kuwa waziri katika serikali yake.
 
“Unajua Mzee Mkapa ni mtu makini, mtu ambaye hapendi majungu. Usije ukampelekea jungu. Na mimi nimegundua toka tuko gazeti la Uhuru. Kama hujamzoea utamuona kama mtu anayeringa hivi… lakini nimemgundua mtu yeyote anaweza kumwingia,” alisema.
 
“Ni msomi, ni very serious person, principled (ni mtu makini, mwenye kufuata kanuni) na ni mzalendo. Ni kiongozi makini na kama utamuelewa, atakuwa rafiki yako mkubwa,” alisema Ameir.
 
UMRI WA URAIS
Kuhusu umri wa urais, Ameir alipendekeza uanzie miaka 40 kwani ana amini kuwa huo ndiyo umri mzuri zaidi kwa sababu akili (ya mtu) tayari inakuwa imekomaa na anajua kuwa amepewa dhamana ya kulitumikia taifa.
 
Alisema rais ni mtu mkubwa kwa kuwa ndiye mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu na hivyo kama (rais) bado ana mambo ya ujana, ni hatari kwa nchi.
 
“Mimi vijana watanisamehe… wanaweza kunishangaa kwamba hili dingi ni conservative (huyu mzee ni mhafidhina). Lakini miaka 40 ni umri mzuri,” alisema na kuongeza:
“Siyo lengo langu kuwazuia vijana kuwa marais. Lakini lengo langu ni (kuona) kuwa rais akiwa na umri angalau miaka 40, huwa hababaishwi kwa sababu ujana una mambo yake. Mtanisamehe vijana.”
 
“Rais ni mtu mkubwa sana. Ndiye Amiri Jeshi Mkuu, watu wote, hata mkuu wa majeshi anampigia saluti. Mkipata mtu ambaye hajatulia vizuri, mnaweza kupata matatizo.”
 
Alitolea mfano kwa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akisema alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza,  alikuwa kijana mdogo lakini aliweza kuongoza kwa kuwa alipendekezwa na kusimamiwa na  jeshi na kwamba kwa sasa amekomaa na hivyo amekuwa rais mtendaji.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment