Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 4 January 2014

ZITTO KABWE AIVURUGA CHADEMA


















MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeahirisha hadi Jumatatu kusikiliza shauri lililofunguliwa mahakamani hapo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Katika shauri hilo, Zitto aliitaka mahakama kuizuia Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujadili uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Hata hivyo mara baada ya uamuzi huo kutolewa jana, ziliibuka vurugu ambapo wafuasi Chadema walitwangana makonde nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, hadi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kilipoingilia kati na kuwatawanya.

Wafuasi hao walitwangana makonde jioni wakati maombi ya Zitto yalipomalizika kusikilizwa, ambapo baadhi ya kundi linalompinga lilifanya vurugu na kumkashfu mbunge huyo asubuhi kabla ya kesi hiyo kuanza.
"Fisadi wewe, umenunuliwa na CCM, mtu mmoja tu unatupotezea muda hapa mahakamani.” Hayo yalikuwa maneno ya wafuasi wa chama hicho katika makochi ya mahakama ambako, Zitto alikuwa amekaa na wakili wake.
Askari walifanikiwa kumtoa Zitto katika eneo hilo na kumweka katika chumba maalumu hadi mchana, wakati maombi yake yalipoanza kusikilizwa ambapo walimuingiza mahakamani kupitia mlango wa majaji, mlango ambao ulitumika pia kumtoa baada ya kesi hiyo kuahirishwa jana jioni.
Nje ya Mahakama Kuu, wafuasi wa makundi hayo mawili walikuwa na mabango, ambapo wafuasi wanaodaiwa kuunga mkono uongozi wa Chadema mabango yao yaliandikwa: “Zitto CCM”, huku wafuasi wa Zitto walibeba mabango yenye ujumbe uliosomeka: “Zitto kama Mandela”.
Wafuasi hao walioshinda mahakamani hapo huku kila kundi likishangilia kwa kutamka walichokiandika, walipigana hadi askari waliokuwa wakiimarisha ulinzi walipowaamua na kuwatawanya.
Kutokana na vurugu hizo, wakili wa Zitto, Albert Msando na wenzake wanne waliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa askari hadi walipokuwa wameegesha magari.
Kwa upande wake, Zitto alitolewa kwa kutumia mlango mkubwa wa nyuma unaotumiwa na majaji na kupanda katika gari lisilojulikana, lengo likiwa kuwakwepa wafuasi hao kwa ajili ya usalama wake.
Hata hivyo wafuasi hao walitaka kumpiga askari kanzu wakidai anawarekodi, huku mmoja wa wanachama hao alipojaribu kumtetea askari huyo alivamiwa na kupigwa hadi kuchaniwa shati.
Zitto alifungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Willbrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakapomalizika mahakamani hapo.
Katika kesi ya msingi, Zitto anaiomba mahakama iamuru kamati kuu na chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.
Aidha anaomba mahakama imwamuru, Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa.
Maombi hayo yanasikilizwa mbele ya Jaji John Utamwa, ambapo wakili wa Zitto, Albert Msando aliiomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama kutojadili suala la uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akiwasilisha hoja zake wakili Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika chama, uliotolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 12 mwaka jana.
Wakili alidai endapo amri hiyo haitatolewa na Kamati Kuu ikamvua uanachama, Zitto atapata athari kubwa kuliko chama chenyewe kwa kuwa atapoteza nafasi yake ya ubunge na kushindwa kuwatumikia wananchi waliomchagua.
Si hilo tu, mwanasheria huyo alisema athari nyingine ni kwamba iwapo atafukuzwa uanachama, Zitto atapoteza nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Alisisitiza kuwa, Zitto haizuii Chadema kufanyakazi zake za kisiasa kama wao wanavyodai katika hati ya kiapo kinzani, bali anaomba Kamati Kuu isijadili suala lake la uanachama mpaka uamuzi utakapotolewa.
Akijibu hoja hizo Wakili wa Chadema, Tundu Lissu alidai kuwa katika kutoa zuio la muda mahakama inatakiwa iangalie maslahi ya walio wengi na si faida ya watu wachache.
Alidai katika hati ya kiapo, Zitto anadai hakuna tarehe ya kikao cha Baraza Kuu la chama kilichopangwa, pia asipokata rufaa hatotendewa haki na atapata madhara lakini dawa ya woga na hofu yake ni kuomba mahakama iamuru kikao cha Baraza Kuu kifanyike na siyo kuomba zuio.
Lissu alidai kuvuliwa uanachama kwa Zitto hakutakuwa na athari kubwa kama anavyodai, athari ataipata yeye kwa kukosa posho na mishahara.
Hata hivyo, Jaji Utwama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili aliamua kutoa uamuzi wa kuzuia au kutozuia kamati hiyo kujadili uanachama wa Zitto hadi Jumatatu.

CHANZO: Mtanzania

No comments:

Post a Comment