TUSIUMIZE VICHWA BURE
MRITHI WA RAIS KIKWETE HUYU HAPA
Na Mwandishi Maalum
Mwenendo
wa upepo wa kisiasa ni vigumu kuwa na utabiri wa kuaminika kutokana na ukweli
kuwa wakati wowote hubadilika na kugeuza mwelekeo. Hali hii inatokana na ukweli
ambao hauzuiliki unaotokana na hali ya kimaumbile ya binadamu ya kuwa daima ya
hamu ya kutaka mabadiliko hata bila ya kujua atafaidikaje na mabadiliko hayo.
Ni kwa
silika hii baadhi ya watanzania hasa vijana wasiojua nchi ilikotoka, imefikia
wapi na inataraji nini sasa na kwa mustakbali, waliweka matumaini yao kwenye
vyama vya upinzani kama njia ya kufikia mapinduzi ya hali zao hasa za kiuchumi
kwa dhana kuwa hali ngumu ya uchumi waliyonayo inasababishwa na chama tawala
CCM.
Matumaini
ya
wenye nadharia ya kuhitaji mabadiliko kwa mujibu kisilika ya kibinadamu
tu, na ambao wengi wao ni vijana wadogo, wameweka tumaini
lao kwenye vyama vya upinzani hususan chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), ambacho katika chaguzi zilizopita kilifanya vizuri
ukilinganisha na
vyama vingine vya upinzani.
Hata
hivyo matumaini hayo yamefifia katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja
uliopita, baada ya kuzuka malumbano makubwa na kutoaminiana baina ya viongozi
wa ngazi ya juu wa chama hicho.
Katika
kipindi cha mwaka mzima wa 2013 viongozi wa Chadema wamejishughulisha zaidi na
mapambano ya ndani badala ya kuimarisha chama, kitendo ambacho kimekidhoofisha
na kukirejesha nyuma lakini pia kuwakatisha tamaa watanzaniajuu ya uwezekano wa
chama hicho kukiangusha Chama tawala katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Hali ya mapambano ndani ya chama hiki kikuu
cha upinzani kumekinufaisha chama cha Mapinduzi ambacho watendaji wake wakuu
walitumia mwanya huo kukiimarisha chama chao na kuwajengea wananchi dhana ya
kupuuza upinzani huku serikali ikishadidisha kusimamia miradi ya maendeleo ambayo
ni mtaji wenye nguvu kisiasa mbele ya jamii.
Kitendo cha
kutuhumiwa Mbunge wa Kigoma kaskazini Zitto Kabwe na wenzake kuwa wasaliti wa
chama hicho kwa kutumiwa na CCM, kitaendeleza dhana mbili endelevu zilizo muhimu
na zinazohitaji tafakuri.
Kwanza ni
kuwa, kuna udhaifu mkubwa ndani ya uongozi wa Chadema ngazi ya Taifa kwa kiasi
kwamba CCM imeweza kupenya na kuingia ndani na kufaulu kujenga dhana ya
kutoaminiana na kuusambaratisha uongozi.
Pili,
Chadema watapaswa kufahamu kuwa ikiwa vyanzo vyao vya uchunguzi vimebaini kuwa
CCM ilijipenyeza ndani yao kwa kiasi kinachoelezwa, ni wazi pia bado ndani ya
Chadema kuna CCM wengine ambao wana jukumu la kuendeleza wimbi la kutoaminiana
na hivyo hali ya mambo bado si shwari.
Kwa
ujumla katika uwanja wa siasa za vyama vingi bado CCM inatawala kwa kigezo cha
ukweli kuwa inamiliki serikali na vyombo vyake na hakuna shaka kuwa vyombo
hivyo kwa pamoja vitaendelea kuhakikisha vinailinda Ikulu kuangukia mikononi mwa
wapinzani na njia mojawapo ni kuwasambaratisha wapinzani kama walivyofanya kwa NCCR-Mageuzi.
NCCR-MAGEUZI
ni chama kilichokuwa na nguvu kubwa lakini kama ambavyo kila mmoja wetu
anafahamu hadi leo chama hicho kinachechemea
baada ya kutokea machafuko ya ndani kama haya tunayoyaona sasa ya Chadema ambayo
kuna kila dalili inayoonyesha virusi vya ugonjwa huu kiasili vinategenezwa na
CCM.
Chama cha
Wananchi (CUF) kama vyama vingine vya upinzani kinaendelea kushuka chati baada
ya kuwa na magomvi ya ndani ambayo tunaweza kuyaita ni maradhi ya wapinzani.
Chama hiki katika sura yake halisi kinaonyesha uhai wake uko mikononi mwa mtu
binafsi.
Ukiondoa
visiwani Zanzibar ambako Maalim Seif Shariff Hamad ni mwanasiasa nyota anayeng'ara
kwa siasa za upinzani visiwani humo, CUF hakina mvuto wa kisiasa popote
Tanzania Bara na kila uchaguzi mkuu wa Rais unapofanyika Chama hicho huzidi
kupoteza umaarufu wake na kudidimia.
Kwa upande
wa demokrasia ndani ya vyama vyote viwili vikuu vya upinzani CUF na Chadema
havina demokrasia ya kweli ndani yake ukilinganisha na CCM. Mfano mdogo ni huu
kwamba haihitajiki mkutano mkuu ndani ya Chadema wala CUF kumtambua nani atakuwa
mgombea wa kiti cha Urais kwa Bara au Visiwani na anayejaribu kuhoji jambo hilo
hapana shaka atafukuzwa si tu uongozi bali hata uanachama wa chama chenyewe.
Sasa kama
nilivyotanguliza kusema awali upepo wa kisiasa hubadilika, lakini hadi sasa
kuelekea uchaguzi Mkuu wa Rais wa mwaka 2015 hakuna matumaini yanayoonyesha
kuwa mrithi wa Dk Jakaya Kiwete atatokea chama cha upinzani, bali bado upepo unaashiria
kuendelea utawala wa CCM.
Kuwapo
kwa wanasiasa wengi wenye kujikweza kwenye dhana ya sifa za kugombea nafasi
hiyo, kunakiweka chama cha Mapinduzi katika wakati mgumu kutokana na makundi yaliyomo
ndani kugombea nafasi hiyo muhimu katika taifa.
Ukweli
wenyewe ni kuwa Rais JK ana wakati mgumu sana katika shughuli ya kuutua mzigo
wa uongozi wa Chama chake kwa sababu huenda chama hicho kikasambaratika kabisa
au kikapata ushindi kiduchu utakaokipa serikali dhaifu yenye kutegemea
maridhiano na upinzani endapo vita ya kugombea urithi wa kiti cha rais ndani ya
CCM haitodhibitiwa.
Ndani ya
CCM kuna hazina kubwa ya viongozi wenye maadili na uwezo mkubwa kiuongozi
lakini wamekuwa kimya na hawaoni busara ya kujitokeza na kujitangaza kufaa kwao
kwa sababu maadili mema hayamfundishi mtu mwadilifu kujitukuza na kujinaki kwa
kujipa sifa mwenyewe.
Pengine
wapenzi wa wanasiasa wa kambi mbali mbali hawawezi kufurahia uchambuzi huu,
lakini ni ukweli usioepukika kuwa Edward Lowassa kwa sasa anatambulika kuwa
ndiye mwana-CCM aliyejipanga na kufanikiwa kuwarubuni wana-CCM wengi kuamini
kuwa yeye ndiye rais ajaye.
Lowassa anafahamika
kama mwanasiasa hodari, mwenye haiba na shakhsiya, hutambulika pia kama mtu
mwenye maamuzi na uwezo mkubwa wa kusimamia maamuzi yake. Mwandishi wa
uchambuzi huu ni mmoja wa watu ambao wasingependa Lowassa ashike nafasi ya
Urais, lakini chuki na utashi wake binafsi hauna nguvu ya kuzuia ukweli
kusimama mahala pake.
Lowassa
ameshikilia turufu kutokana na uwezo wake mkubwa kifedha ambao ameutumia bila
ajizi kuugawa kwa mahitaji ya kijamii hususan kupitia taasisi za kidini na kumfanya
Lowassa kukubalika zaidi Makanisani.
Lakini hata
hivyo Lowassa bado hajamaliza tofauti zake na Waislamu wanaomtazama kama mdini
kutokana na kusaini mkataba (Memorandum
of understanding) baina ya Serikali na Wakristo unaoipa jamii hiyo fursa ya
kufaidika na fedha kutoka serikalini.
Lowassa ambaye alijiuzulu nafasi ya waziri mkuu kutokana na kashfa
ya kampuni iliyodaiwa kuwa hewa ya kufua umeme ya Richmond, licha ya kugawa
mamilioni ya fedha kila anapoalikwa bila ukomo, amekuwa akikanusha kuwa yeye si
tajiri na kwamba nyuma yake wako watu ambao anawaita marafiki wanaochangia
mamilioni hayo.
Jambo ambalo wengi wanajiuliza bila kupata jibu kuhusu suala la
fedha anazogawa Lowassa ni je, hawa
marafiki zake wanaojitolea mamilioni haya wana nia gani katika utoaji wao?
Marafiki hawa wema kiasi hicho ni watanzania au ni raia wa kigeni? Nini
madhumuni yao katika kumjenga Lowassa kupitia njia ya kumwaga mapesa?
Wanategemea kupata nini kwa Lowassa akishaingia Ikulu? Akiwa Ikulu
Lowassa anategemea kuwa na hiyari juu ya wafadhili wake hao? Wafadhali hao
hawawezi kuwa na kauli yoyote juu ya mfadhiliwa? Je haiwezi kuwa watu hawa wana
nia ya kumfanya Lowassa akubalike ili baadae ajikute kuwa rais wakala wa
wawezeshaji wake?
Uchunguzi wa uhakika wa mwandishi wa dodoso hili unaonyesha kuwa
uongozi wa CCM katika mikoa mingi unamuunga mkono Lowassa kwa kiwango kwamba
kuna tetesi kuwa kuna baadhi ya viongozi kimkoa wanapata posho zao ama kwa
Lowassa mwenyewe au kwa watu wanaodhaniwa kuwa wapenzi wake.
Kwa kuzingatia udhaifu wa vyama vya upinzani, na dhana kuwa mgombea
wa CCM ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuwa rais, na kwa namna Lowassa
alivyojipanga ndani ya chama, na ukweli kuwa endapo jina la Lowassa litaingizwa
katika mkutano mkuu hakuna wa kumshinda, basi hapana shaka Lowassa ana nafasi ya
kuwa mrithi wa Rais Jakaya Kikwete.
Hii si maana yake kuwa Edward Lowassa ndiye pekee mwana-CCM
anayefaa kwa nafasi hiyo. Wapo wengine wanaotajwa tajwa na ambao wana sifa bila
dosari za wazi japo hawana mamilioni ya kumwaga akiwemo Benard Membe, Dk Hussein Mwinyi, Dk Emmanuel Nchimbi na Dk Asha
Rose Migiro.
Wengine ambao wanatajwa kuwa wanafaa ni pamoja na Dk Harison
Mwakyembe, Anne Makinda, Dk John Magufuli, na pia kuna wengine kama Samuel
Sitta na waziri mkuu mstaafu Fredirick Sumaye.
Kwa kadiri ya mjadala huu utakavyoendelea jambo kubwa la msingi linaloweza
kutokea ni CCM kusambaratika baada ya jina la Lowassa kuondolewa katika
kinyang'anyiro cha urais na Lowassa naye akajibu kwa kuamua kujiondoa ndani ya
chama hicho.
Endapo jambo hilo litatokea CCM
itagawanyika vipande ambavyo ama vitawapa nguvu wapinzani kuchukua nchi au CCM
kupata ushindi kiduchu utakaokifanya kuwa na rais atakayekuwa na wabunge
wachache na hivyo kuongoza serikali dhaifu.
Naomba nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha wanaogombea nafasi
ya urais na wapambe wao kuwa mbali na kampeni zao wenyewe wasije wakasahau
kuzihusisha jitihada zao na matakwa ya Rais Kikwete kama kiongozi wa nchi,
lakini pia Kikwete kama mtu mwenye shakhsiya na mvuto maalum wenye nguvu na
ushawishi wake binafsi.
Lakini kubwa kuliko yote msilolijua wagombea masikini na matajiri, ni
hilo la kuwa Rais wa Tanzania atakayemrithi Jakaya Kikwete ni huyo hapa, "Mgombea
ambaye ataungwa mkono na Jakaya mwenyewe iwe wakati huo kikatiba anaruhusiwa
kumfanyia kampeni au haruhusiwi.
Nafahamu kuwa wako watakaosema ya kuwa hata viongozi waliomtangulia
JK walishindwa kuwaweka warithi waliowataka wao kwa kuwa walikinzana na upepo
wa kisiasa. Lakini upepo wa kisiasa unaotoa ishara ya kubadilishana uongozi
baina ya Rais Kikwete na mrithi wake uko wazi kuwa miongoni mwa watu
anaowafikiria yeye basi mmoja wao ndiye atakayemrithi. Kama wengine walishindwa kuna kila uwezekano
JK hatoshindwa. Kwa hiyo usisumbuke na kuumiza kichwa chako bure atakayeungwa
mkono na Kikwete mwenyewe ndiye rais ajaye.
<WANABIDII>
No comments:
Post a Comment