Ndugu Viongozi wote mliopo hapa,
Ndugu Waandishi wa Habari.
Awali ya yote napenda kuwakaribisha katika mkutano huu ambao nitaelezea Mafanikio ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne.
Ukiacha Idara za Utawala, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaundwa na Idara kuu tano ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Idara ya Huduma kwa Jamii. Pia katika Wizara yetu tuna Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.
Majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kuhifadhi na kuwarekebisha wafungwa, kutoa huduma za zimamoto na uokoaji, kudhibiti uingiaji na utokaji nchini kwa raia na wageni, kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Huduma kwa Jamii na kuandaa na kutoa Vitambulisho vya Taifa.
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne, Wizara yetu imefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuiwezesha nchi yetu kuwa na amani na utulivu. Kwa wastani tunaweza kusema kuwa nchi yetu imekuwa na usalama ambao umewawezesha wananchi na wageni kuendelea kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi, licha ya matukio ya hapa na pale, ambayo Wizara inaendelea kuyachukulia hatua na kuyatafutia ufumbuzi.
Jeshi la Polisi:
Wizara yetu, kwa kupitia Jeshi la Polisi, imeweza kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vimeanza kukithiri hapa nchini. Vitendo hivyo ni pamoja na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha, wizi katika mabenki, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino na makosa mengine ya kijinai. Kwa mfano, kwa juhudi zilizofanywa na Wizara yetu, makosa ya kuwania mali (unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi katika mabenki, uvunjaji, wizi wa mifugo n.k) yalipungua kutoka 53,268 mwaka 2005 hadi 45,470 mwaka 2013. Mengine yaliyopungua ni mauaji ya albino kutoka 20 mwaka 2008 hadi moja mwaka 2013. Watuhumiwa waliohusika katika matukio haya walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kwa ujumla kutokana na juhudi zinazofanywa na Wizara, makosa makubwa ya jinai yamekuwa yakipungua kwa wastani wa asilimia sita (6) kila mwaka.
Katika juhudi za kuongeza nguvu kazi, idadi ya askari na askari wanafunzi katika Jeshi la Polisi imeongezwa kutoka 26,000 mwaka 2006/2007 hadi 44,000 kufikia Desemba, 2013.
Nyumba mpya 491 kwa ajili ya askari Polisi zimejengwa kote nchini yakiwemo maghorofa 84 yaliyojengwa Dar es Salaam, matatu Zanzibar na mengine matatu, Pemba. Pamoja na kuendelea na ujenzi katika maeneo mengine nchini, Jeshi la Polisi limesaini makubaliano ya awali ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 350 za kuishi askari katika mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni mara mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Mara Group utakaposainiwa. Aidha kwa msaada wa Serikali ya Marekani, Chuo cha Polisi Wanamaji kimejengwa mjini Mwanza.
Kwa upande wa vitendea kazi, magari mapya 373 na pikipiki 1,128 zimenunuliwa. Boti 10, magari 97 na pikipiki 484 zimepatikana kutoka kwa wafadhili na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuimarisha operesheni za Jeshi la Polisi.
Jeshi la Magereza:
Katika kuimarisha shughuli za utunzaji na urekebishaji wafungwa, Wizara kupitia Jeshi la Magereza imefanikiwa kukarabati majengo na miundombinu ya magereza, likiwemo Gereza lenye ulinzi mkali la Butimba, na ukarabati wa majengo mengine ya ofisi za Utawala umefanyika katika magereza ya Uyui, Lilungu, Maweni, Isanga, Keko na Ukonga. Ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa mabweni ya wafungwa umefanywa katika magereza 24 nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa usalama wa wafungwa unaimarishwa.
Aidha, ujenzi wa jengo la ghorofa la kuishi familia 16 za askari katika Gereza la Mahabusu Iringa umekamilika. Ujenzi wa nyumba za maofisa na askari unaendelea katika magereza 17 nchini. Pia nyumba nne (4) pamoja majengo na mengine matatu (3) yamenunuliwa kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) wilayani Lushoto mkoani Tanga kwa ajili ya matumizi ya Jeshi. Aidha ukamilishaji wa nyumba zilizojengwa kwa njia ya ubunifu unaendelea katika magereza 11 nchini.
Ili kutoa nafasi zaidi kwa wafungwa wanaopokelewa magerezani, idadi ya nafasi za kuwalaza wafungwa zimeongezwa kutoka 22,699 mwaka 2005 hadi nafasi 29,552 mwaka 2011.
Jeshi la Magereza pia limeanzisha na kutekeleza jukumu la kuwapeleka mahabusu kwenda Mahakamani na kurudi gerezani kwa kutumia mabasi ya kisasa. Zoezi hili lilianza rasmi tarehe 19 Mei, 2008 kwa mahabusu waliopo mkoa wa Dar es Salaam na wale wa mkoa wa Pwani. Kwa sasa zoezi hili limeendelezwa katika mikoa ya Arusha na baadhi ya wilaya za mkoa wa Dodoma, na litaendelea kutekelezwa kwa awamu nchi nzima.
Mafunzo mbalimbali yameendeshwa ndani ya Jeshi la Magereza na watumishi 5,889 walihitimu kozi mbalimbali hadi mwishoni mwa mwaka 2013.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji:
Katika kukabiliana na majanga ya moto, Wizara kwa kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji imeweza kupunguza majanga ya moto kwa kiasi kikubwa. Pia ofisi za Zimamoto na Uokoaji zimeanzishwa katika mikoa yote nchini na zinaongozwa na Makamanda wa Zimamoto wa Mkoa. Aidha vituo vipya vya Zimamoto na Uokoaji vimejengwa katika maeneo ya Lugalo, wilaya ya Kinondoni na Mchicha, wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, na vituo vidogo katika maeneo ya Karatu, wilayani Karatu mkoani Manyara na Same, wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Jumla ya magari ya kuzima moto 25 yamenunuliwa na askari 379 na watumishi raia 28 wameajiriwa. Ili kuongeza zaidi nguvu kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetoa kibali cha kuajiri askari 800 katika mwaka wa fedha 2013/2014 na kazi hiyo imeshaanza.
Idara ya Uhamiaji:
Kwa kupitia Idara ya Uhamiaji, Wizara imefanikiwa kutoa Pasi za Kusafiria za kawaida 534,855, za kiutumishi 4,035, za ki-balozi 2,172, na za Afrika Mashariki 13,220. Aidha katika kipindi cha mwezi Januari, 2006 hadi Desemba, 2013, imeweza kuwahudumia wageni 6,469,876 walioingia nchini na 6,395,167 waliotoka nchini. Pia imeweza kutoa vibali 322,603 vya ukaazi na kutoa vibali vya uraia wa Tanzania kwa wageni 1,392. Wahamiaji haramu 65,675 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria. Kati ya wahamiaji hao haramu, 31,203 walipatikana wakati wa Operesheni Kimbunga, iliyotekelezwa kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka 2013. Aidha jumla ya raia wa Tanzania 2,770 waliokuwa wamezamia nchi za nje walirejeshwa na kupokelewa nchini.
Kutokana na shughuli mbalimbali zilizofanywa na Idara ya Uhamiaji, makusanyo ya maduhuli ya serikali yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 14.2 mwaka 2006/2007 hadi bilioni 83.4 mwaka 2013/2014. Ongezeko hili kubwa lilitokana na juhudi zilizofanya na Serikali kuboresha mifumo ya makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
Ili kuboresha huduma, jumla ya magari 192 yalipatikana, 93 kati ya hayo ikiwa ni misaada ya wafadhili. Idara pia ilinunua pikipiki 206 na boti 2 ambazo hutumika katika misako na doria katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa:
Wizara kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vy Taifa imezindua Mfumo wa Usajili na Utambuzi wa watu nchini na Vitambulisho vya Taifa vimeanza kutolewa mwezi Februari, 2013 kwa watumishi wa Serikali 290,000 walioko Dar es Salaam na Zanzibar. Aidha, zoezi la kusajili wananchi limeanza katika mikoa ya Dar es Salaam ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya wananchi 2,159,822 wamesajiliwa jiji la Dar es Salaam na wengine 220,000 katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Lengo ni kuendeleza kwa awamu zoezi hili nchi nzima.
Idara ya Huduma kwa Jamii:
Idara ya Huduma kwa jamii inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Huduma kwa Jamii ambayo inahusiana na utekelezaji wa adhabu mbadala ya vifungo magerezani. Tangu mwaka 2006 hadi 2013, Wizara kupitia Idara hii imeweza kufikisha huduma zake katika mikoa 17 kati ya 25 ya Tanzania Bara. Jumla ya wafungwa 6,444, kati yao wanaume 5,940 na wanawake 504, wamefaidika na adhabu mbadala ya vifungo magerezani, ambapo jumla ya wafungwa 5,193 wamemaliza adhabu zao za kutumikia jamii.
Kutokana na utekelezaji wa Sheria hii, Serikali imekuwa ikiokoa kiasi cha shilingi 3,500 kila siku kwa kila mfungwa anayepangiwa kufanya kazi za jamii badala ya kufungwa gerezani.
Kwa upande wa kutoa elimu kwa wadau muhimu, Wizara kupitia Idara ya Huduma kwa Jamii imeweza kuendesha Mafunzo mbalimbali kwa wadau hao ambao ni Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Wasajili wa Mahakama, Maafisa Usalama wa Taifa, Maafisa Magereza, Polisi, Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri katika mikoa 17 inayohusika.
Maboresho ya Miundo ya Idara za Wizara;
Jeshi la Polisi:
Wizara imefanya maboresho ya Muundo wa Jeshi la Polisi ambapo nafasi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi imeundwa na Divisheni za Jeshi hilo zimeongezwa kutoka nne hadi nane, ambazo zote zinaongozwa na Makamishna kama ifuatavyo:
Kabla ya hapo kulikuwa na Makamishna wanne tu wa:
Maboresho haya yanategemewa kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa Jeshi la Polisi.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji:
Vikosi vyote vya Zimamoto na Uokoaji sasa vimewekwa chini ya Komandi moja ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Kabla ya hapo kulikuwa na vikosi chini ya Mamlaka mbalimbali, kama vile Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Mamlaka ya Bandari, na Mamlaka za Halmashauri za Miji na Majiji ambapo vikosi hivi vilikuwa na Komandi zinazojitegemea.
CHANGAMOTO:
Pamoja na mafanikio tuliyopata bado kuna changamoto mbalimbali zinazokabili utendaji wa shughuli za Wizara. Changamoto hizo ni pamoja na:
1) Ongezeko la kasi la mahitaji ya huduma ya ulinzi na usalama wa raia ikilinganishwa na rasilimali na vitendea kazi vilivyopo.
2) Kubadilika kwa mbinu za kutenda uhalifu.
3) Ongezeko la makosa makubwa na madogo yanayofanywa kwa njia ya mtandao (cyber crime).
4) Ufinyu wa bajeti ambao unakwamisha utekelezaji wa baadhi ya majukumu na miradi ya maendeleo, kama vile shughuli za ujenzi wa ofisi na makazi ya watumishi na askari, ununuzi wa vifaa na dhana mbalimbali za kazi na uhaba wa watumishi.
5) Ujenzi holela katika maeneo ya mijini, ambao unachangia kukwamisha juhudi za kuboresha huduma za zimamoto na uokoaji.
6) Kujengeka kwa tabia ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kufanya vitendo vya uhalifu.
MALENGO NA MASUALA YANAYOENDELEA KUFANYIWA KAZI:
i. Kuwa na Sera ya Kitaifa ya Usalama wa Raia. Rasimu ya Sera hii inaendelea kufanyiwa kazi na inategemewa kukamilika hivi karibuni..
ii. Kupunguza msongamano magerezani. Kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya adhabu mbadala ya kifungo, kama vile Vifungo vya Nje, Adhabu ya Huduma kwa Jamii na Parole, na kushirikiana kikamilifu na wadau wengine kuhakikisha kuwa usikilizwaji wa kesi zinazowasilishwa unaharakishwa.
iii. Kuwa na Sheria ya Taifa ya Uhamiaji – Waraka wa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Taifa ya Uhamiaji umepelekwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kupata maoni kabla ya kuendelea na utaratibu wa kuuwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri.
iv. Kuwa na Sera ya Taifa ya Uhamiaji na Uraia – Rasimu ya Sera hii pia imepelekwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata maoni ili kufikia muafaka wa kuikamilisha.
v. Matumizi ya Uhamiaji Mtandao – Maandalizi yameanza kwa ajili ya kutoa huduma zote za kiuhamiaji kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Hadi sasa upembuzi yakinifu wa mfumo huo umekamilika na mchakato wa kumtafuta mzabuni wa kutekeleza kazi hiyo umeanza.
vi. Kujenga vituo vitano (5) vya Zimamoto katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam – Lengo ni kuzipeleka karibu kwa wananchi huduma za Zimamoto na Uokoaji.
vii. Kushirikiana na Mipango Miji – Kuhakikisha kuwa miji yetu mikubwa na midogo inapangwa vizuri ili kurahisisha huduma za Zimamoto na Uokoaji.
viii. Kujenga Ofisi za Utambuzi na Usajili wa watu (2014/2015) – Wizara kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ina mpango wa kujenga Ofisi za Utambuzi katika wilaya 45 za Tanzania Bara na tano (5) za Zanzibar ili kuharakisha zoezi la utambuzi na usajili wa watu kwa ajili ya kuandaa Vitambulisho vya Taifa.
Hata hivyo, ni lazima kueleza kuwa mafanikio ya Wizara yetu kwa kiasi kikubwa yamepatikana kutokana na ushirikiano wa wananchi na wadau wengine ambao kila mara wamekuwa wakitoa michango yao ya hali na mali. Ili kuendelea kupata mafanikio na kutekeleza mipango yetu ya baadaye kwa ufanisi zaidi, Wizara yetu itategemea ushirikiano wa wananchi kupitia mikakati yetu mbalimbali kama ile ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi na mingineyo.
Kwa kupitia mkutano huu napenda kutoa shukrani za dhati kwa wananchi na wadau wengine wote ambao mara zote wamekuwa wakisaidiana na Wizara yetu kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na amani na utulivu na naomba ushirikiano huu uimarishwe zaidi katika siku zijazo.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment