Bw. Nape Moses Nnauye
Mara baada ya kuundwa kwa Sekretarieti
ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg.
Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka mwaka jana, Sekretarieti hiyo
imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani kukutana na wananchi
kusikiliza kero zao,kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na
kuimarisha Chama mikoani. Utaratibu huu ni agizo la mkutano mkuu wa
Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma. Nanukuu
azimio hilo;
“ Chama Cha Mapinduzi lazima kiwe karibu
na wananchi, kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa
wanyonge” Moja ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
Kwa hiyo msingi wa kwanza wa ziara hizo
ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambacho ndicho kikao cha juu
kabisa cha Chama. Msingi wa pili ni ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa
dhamana na kuingia mkataba na wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2010/2015, hivyo inayowajibu wa kukagua utekelezaji wa ilani
hiyo.
Na bila shaka wote tumeshuhudia jinsi
ziara hizo zilivyoinua uhai wa Chama nchi nzima na kuongeza kasi ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kutatua kero mbalimbali za wananchi
kwenye maeneo yao, kiasi cha kuongeza imani ya wananchi kwa CCM.
Tumeshuhudia makundi mbalimbali ndani ya
jamii yakija kueleza changamoto zao ndani ya Chama. Makundi hayo ni
pamoja na makundi ya wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanafunzi na
wafanyakazi hasa walimu. Huu ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao
kwa CCM.
Katika mwendelezo wa ziara hizo mwishoni
mwa mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti
walifanya ziara ya siku 26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe.
Pamoja na mambo mengine wananchi walilalamikia baadhi ya watendaji wa
serikali hasa baadhi ya mawaziri wakiamini kuwa yapo mapungufu kadhaa
yanayotokea kwenye wizara zao.
CCM kama lilivyo agizo la Mkutano mkuu
la kuwasemea wananchi tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu,
baadhi ya mawaziri hao waliitwa na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM
mwezi Disemba 2013.
Utaratibu wa watendaji wa serikali
kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye vikao
vya Chama sio mgeni na wala haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa kwenye
wilaya, wakuu wa mikoa hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu mpya.
Baada ya mahojiano hayo Kamati Kuu ya
CCM ilitoa ushauri kwa serikali wa namna ya kurekebisha mapungufu
yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye
mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe, CCM ililiacha suala hili kwake
aangalie njia ipi bora ya kuondoa mapungufu tuliyoyaeleza.
Na kwenye taarifa yetu kwa vyombo vya
habari baada ya kikao hicho tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze
mawaziri husika isipokuwa wanaweza kufanya mabadiliko katika
mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na mabadiliko katika kushughulikia
mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
Hivi karibuni Rais amefanya mabadiliko
kidogo kwenye baraza lake la mawaziri na kuwarudisha baadhi ya mawaziri
waliolalamikiwa na wananchi na wabunge, ambao malalamiko hayo yaliungwa
mkono na CCM. Ni kupitia malalamiko hayo ndipo lilipozaliwa jina la
mawaziri mizigo. Baada ya uteuzi huo kukaibuka mjadala mkubwa nchini
wakihoji kulikoni Rais kaamua kutowatimua mawaziri hao.
Kwanza haikua hoja ya CCM kuwafukuza
mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu husika.
Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo lakini sio njia pekee.
Hivyo basi CCM tunaamini kuwa kurudishwa kwao wamepewa fursa ya
kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa niaba ya wananchi. Tunaamini
mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu wao na kuhakikisha
wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa serikali.
Ifahamike kuwa Chama Cha Mapinduzi
hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine
watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu
wao vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa
Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa
CCM itakua ni kujinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.
Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa
serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi
wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani
CCM tutakuwa wakali sana kwenye mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua
tunajihujumu wenyewe.
Tutatumia vizuri wingi wa wabunge wetu
bungeni na wingi wa madiwani wetu kwenye halmashauri kuisimamia vizuri
serikali. Hivyo kuanzia sasa kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu
itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya vibaya itaongezeka mara dufu
kwa kila ngazi.
Tunawaomba watanzania kwa ujumla tuwape
muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema
pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa
kweli ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yetu.
CCM inawatakia kila lakheri kwenye
kutimiza wajibu wao. Tuna matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja
hawataisaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba hawatayaangusha
matumaini ya wananchi kwa serikali yao.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
23/01/2014
No comments:
Post a Comment