Kama mojawapo ya mikakati ya baadhi ya watu wanaotaka kuhamisha
mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya
chama, hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe
amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa
nafasi yake ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza;
Tuhuma hizo ni pamoja na;
1.Kwamba
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka kwa
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kiasi cha sh.Milioni 40
ili Mwenyekiti Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.
2. Mwaka 2008, eti Mbunge Mkono
alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa, sh. Milioni 20 kwa ajili ya
uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama mkopo na
akalipwa.
3. Mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mbunge
Mkono eti alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa sh. Milioni 200 kwa ajili
ya kampeni za mgombea urais.
4.
Mwaka huo huo wakati wa uchaguzi mkuu, eti Mwenyekiti wa Chama Taifa,
alipokea sh. Milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni.
Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda kusema yafuatayo;
1.
Hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo. Ni uongo na uzushi
uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka
kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM
na kwamba chama hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya
Watanzania katika kupigania haki zao na kupinga kila aina ya ufisadi,
kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani, ambacho
kimepoteza ushawishi kwa wananchi.
2. Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala.
3.
Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kuuambia umma wa Watanzania wote,
hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko
nchini kwamba,Mwenyekiti wa Chama Taifa, ameshawasiliana na mawakili
walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
4. Kwa uhakika tunapenda kuiambia
jamii ya Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa
CHADEMA na wapenda mabadiliko wote nchini, kwamba; Chama wala Mwenyekiti
wa Chama Taifa, mahali popote na wakati wowote, hajawahi kupokea msaada
wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.
5. Tungependa kuwaambia waliozusha
tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda kutunza heshima kidogo waliyobakiza
katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo wa tuhuma za utovu wa
maadili na usaliti dhidi ya CHADEMA, badala ya kugeuka kuwa mabingwa wa
kupika uongo, wajibu masuala ya msingi yanayowaandamana kuhusu mikakati
yao ya kuhujumu CHADEMA na viongozi wake, ambayo iwapo chama
kisingeibaini na kuchukua hatua za kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto
na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala,
kwa kuiondoa CCM madarakani.
6. Taarifa kuhusu baadhi ya tuhuma
katika mkakati huo ambazo zimemlenga Mwenyekiti wa Chama Taifa, kwa
kuhusisha shughuli zake binafsi za uwekezaji, zitajibiwa kupitia taasisi
husika.
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA
No comments:
Post a Comment