Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne
Mtaturu akiwasilisha mtazamo wa namna ambavyo anataka Wilaya hiyo iwe.
Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa
Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakifatilia mafunzo
kutoka kwa wawasilishaji.
Afisa Utumishi wa Wilaya ya Ikungi
Evodius Buberwa akifafanua na kutofautisha majukumu ya watendaji wote ngazi ya
Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne
Mtaturu akisisitiza umuhimu wa kuchangia maabara kwa ajili ya kuwanusuru
wanafunzi wanaotaka kusoma masomo ya sayansi lakini kikwaza inakuwa maabara.
Kutoka Kushoto ni Mustafa Mtopo Kaimu Ofisa Usalama wa Taifa Wilaya ya Ikungi, Fortunatus Ndalama, Mshauri wa Mgambo
Wilaya ya Ikungi, Dijovson Ntangeki Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Mkuu
wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka, na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi Milton
Nkyalu wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji waliotoka ofisi ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya ikungi Rustika Turuka aliyesimama akizungumza na Wakuu wa Idara na
vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji
wakati wa kikao hicho cha kazi.
Afisa Utumishi wa Wilaya ya Ikungi
Ahmed Mussa akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi
Dijovson Ntangeki akielezea ratiba ilivyo ya mafunzo hayo.
Na Mathias Canal,
Singida
Wakuu wa Idara na
vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa
vijiji 101 vilivyopo Wilayani Ikungi Mkoani Singida hii leo wamepatiwa mafunzo
ya kutambua mipaka ya majukumu yao kiutendaji katika kikao cha kazi
kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Ikungi.
Mafunzo hayo
yameandaliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na kubainika
kuwa asilimia kubwa ya watendaji hususani wenyeviti wa vijiji na vitongoji
wamekuwa wakiingilia katika majukumu ya kiutendaji.
Akifungua mafunzo hayo
yaliyodumu kwa zaidi ya masaa matano yaliyojikita zaidi kutoa ufafanuzi juu ya
majukumu ya watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji, Mkuu
wa Wilaya hiyo Miraji Jumanne Mtaturu amebainisha
kuwa pamoja na mafunzo kwa ajili ya ufahamu wa majukumu ya watendaji hao lakini
amesema kuwa Wilaya ya Ikungi ipo nyuma kielimu kutokana na shule kuwa mbali na
maeneo ya watu, wanafunzi wa kike kuachishwa shule na kuolewa, baadhi ya
viongozi na wataalamu kutotimiza wajibu wao na wakati mwingine uzembe wa baadhi
ya watumishi wa serikali katika kutatua kadhia za wananchi.
Pamoja na hayo pia DC Mtaturu amesema kuwa kuna baaadhi ya
maeneo kuna shule ambazo zina majengo mazuri na Hosteli kwa ajili ya wanafunzi
lakini wazazi wanakataa kuwapeleka wanafunzi shuleni ikiwa ni pamoja na shule
ya Sekondari Mkinya iliyopo Kata ya Dung’unyi, Shule ya Sekondari Mtunduru,
Shule ya Sekondari Mwaru na Wembere , huku shule ya Sekondari Issuna ikiwa na
Majengo na Hosteli nzuri lakini wanafunzi wanaosoma hapo ni wale wanaotoka
Wilaya nyingine huku wenyeji wakiwa wamejichimbia ndani.
Dc Mtaturu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
hiyo kwa kushirikiana na Polisi kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua baadhi
ya Watendaji wa Kata, Waratibu wa elimu wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na
Watendaji wa Vijiji wanaoshirikiana na baadhi ya wazazi kuwaachisha wanafunzi
shule ili wakaolewe ambapo amebaini kuwa katika Kata ya Mwaru na baadhi ya Kata
zinazozunguka katika Kata hiyo viongozi wake kwa kushirikiana na Waratibu elimu
Kata wamekuwa wakifanya biashara ya kuruhusu wanafunzi kuolewa kwa kupewa
Ng’ombe.
Hata hivyo pia
amewaagiza Watendaji wa Kata ya Makilawa na Iyumbu kumpatia taarifa ya kamati
ya maendeleo ya Kata (WDC) ili kubaini mpango wa mikakati katika kujenga shule
za Sekondari katika Kata hizo mbili ambazo zimesalia ilihali Kata 28 tayari
zina shule za sekondari kati ya Kata 30 zilizopo katika Wilaya hiyo.
Katika shule 28 ni
shule 3 tu zenye maabara, shule ya Sekondari ya Puma na Wembere ambao nao
walijenga maabara baada ya kupata msaada kutoka Benki ya dunia Mwaka 2013,
shule ya Sekondari Mkinya ina maabara 2 ambazo zilijengwa kwa msaada wa SADC mwaka
2009 hivyo kupelekea Wilaya nzima ya Ikungi kuwa na Maabara 4 pekee
zilizojengwa kwa msaada wa wahisani ambapo hakuna hata maabara moja iliyojengwa
na wananchi ikakamilika kutokana na zuio la kuchangia walilolipata wananchi
kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu.
Sawia na hayo pia Mkuu
huyo wa Wilaya amewaagiza Watendaji wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na
Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji kuwaelimisha wananchi kukaa vikao na
kupitisha maadhimio ya kuendelea kuchangisha michango ya ujenzi wa maabara kwa
mujibu wa waraka wa Elimu namba 6 wa mwaka 2015 wa elimu msingi bila malipo.
Hata hivyo agizo
limetolewa pia kwa Wazazi/Walezi pamoja na wanafunzi wenyewe kuchukuliwa hatua
kali za kisheria kutokana na utoro wa wanafunzi shuleni jambo ambalo
linapelekea kuwa na ufaulu duni wa wanafunzi Wilayani humo.
Dc Mtaturu pia
amemuagiza Afisa Mtendaji wa Katana Afisa Mtendaji wa Tarafa kutumia siku 14
kuhakikisha madawati yanafika katika shule zenye uhaba wa madawati ili
kuondokana na adha ambayo inaendelea kuwakumba wanafunzi shuleni ilihali
madawati tayari yamepatikana.
Aidha ndani ya siku
tano viongozi hao wameagizwa kuhakikisha kuwa Masoko pamoja na stendi zinaenda
katika maeneo yaliyopangiwa ili ushuru upatikane kwa wakati na kwa kiasi
kilichokusudiwa.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka amewashukuru Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji
na Watendaji wa Vijiji kwa kujitokeza kwa wingi katika mafunzo hayo jambo
ambalo limeonyesha kuwa wananchi hao wana imani na serikali ya awamu ya nne
hivyo amewaomba kuachana na siasa na kufanya kazi kwa moyo na nguvu zaidi.
Amewataka viongozi wote
wa ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na vitongoji kutekeleza maagizo yote
yanayotolewa na serikali kwa haraka na kwa ukamilifu.
Turuka
amesema kuwa kila kiongozi anapaswa Kutatua kero za wananchi kwa kutenda haki, kutofanya
kazi kwa mazoea, kutoa majawabu sahihi ya wananchi na kama hawafahamu wanapaswa
kuuliza sehemu husika ili kutozungumza jambo wasilokuwa na uhakika nalo.
Kupitia kikao hicho
kilichoitishwa na mkuu huyo wa Wilaya kilichokuwa na dhumuni la kufahamiana na
kukumbushana majukumu na wajibu wa viongozi na kueleza mtazamo wa Ikungi mpya
inavyotakiwa kuwa Afisa utumishi wa Wilaya sawia na Mkuu wa Polisi Wilaya wamepewa
nafasi ya kuelezea majukumu na wajibu wa kila mmoja katika maeneo yao.
Kwa upande wao baadhi
ya Watendaji wa Kata, Vijiji na wenyeviti wa vijiji 101 vilivyopo Wilayani humo
wamesema kuwa mafunzo waliyoyapata watayatumia vyema kuwa mabalozi wazuri kwa
wananchi na kuwaelimisha zaidi ili kutambua mipaka yao na majukumu yao katika
kuishauri serikali.
Aidha Maafisa Tarafa,
Watendaji wa Kata, Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji wote ambao
hawajahudhuria kikao hicho cha kazi wametakiwa kuandika barua za maelezo
kwanini wameshindwa kuhudhuria na zimetakiwa kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Wilaya ya Ikungi hadi kufikia tarehe 10 ya mwezi huu wa nane.
No comments:
Post a Comment