Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart & Co. Ltd, Scholastika Christian Kevela (kushoto), akiwaonesha waandishi wa habari Dar es Salaam leo (hawapo pichani), mkataba wa kimataifa walioingia na Kampuni ya Bidders Choice ya Afrika Kusini wa ushirikiano kwa ajili ya kufanya mnada wa mitambo ya kampuni ya uchimbaji ya Acacia inayomiliki mgodi wa dhahabu Bulynhulu uliopo mkoani Shinyanga. Kulia ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Stanley Kevela.
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Stanley Kevela (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart & Co. Ltd, Scholastika Christian Kevela (kushoto), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo. Kulia ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Stanley Kevela. Nyuma kushoto ni Ofisa wa kampuni hiyo, Salome Sabas na kulia ni Abdrew Kevela.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Udalali ya Yono Auction Mart imeingia mkataba wa ushirikiano na Kampuni ya Bidders Choice ya Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya mnada wa mitambo ya kampuni ya uchimbaji ya Acacia inayomiliki mgodi wa dhahabu Bulynhulu uliopo mkoani Shinyanga .
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Scholastika Kevela alisema wameingia mkataba huo Agosti 24 mwaka huu ambapo watafanya minada ya kuuza mitambo ya zamani ya kampuni ya Acacia kwa njia ya mtandaoni.
Alisema kampuni ya Bidders Choice imewapa tenda ya kufanya minada ya mitambo ya zamani ya madini mbalimbali ambayo inatakiwa kutolewa na kuwekwa mipya.
“Hivyo tunategemea kwenda kwenye mgodi wa dhahabu Bulynhulu kuangalia ni mitambo gani inatakiwa kupigwa mnada ili iwekwe mingine,”alisema Kevela.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo,Stanley Kevela alisema kampuni yake ilipata tuzo ya ufanyaji kazi kwa ubora ambayo imesaidia nchi ya Afrika Kusini kutoa mkataba huo wa kimataifa ambao haujawahi kufanyika nchini kwa kampuni nyingine ya udalali isipokuwa ya Yono.
Alisema kutokana na utendaji wao kuwa mzuri hivyo wanatarajia kuanzisha chuo cha madalali kitakachosaidia serikali kukusanya mapato ya kutosha.
“Hiki chuo cha madalali kikianzishwa kitaleta maendeleo kwenye jamii yetu na jamii wataelewa umuhimu wa kukusanya kodi hivyo taifa litapata mapato mengi, alisema Kevela.
No comments:
Post a Comment