Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 2 September 2014

NAWAKUMBUSHA TU: NYERERE ALISEMA ‘RAIS MWINYI NI DHAIFU’, TENA ‘HATUNA SERIKALI’!

Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania

Hatuwezi kujijengea utaratibu wo wote ambao utazuia kabisa makosa yasifanyike, hasa makosa makubwa; lakini tunatazamia kuwa yakifanyika wanaohusika watawajibika. Na katika makosa makubwa ya maadili na utendaji mwenye jukumu la wazi wazi la kuwadhibiti wahusika ni Rais. Mawaziri wake wanapofanya makosa makubwa, na badala yake kujiuzulu waanze kufanya hila na kutafuta visingizio vya kutofanya hivyo, ni wajibu wa Rais kuwafukuza; na tunamtazamia kufanya hivyo. Ni kazi yake mwenyewe, asiyoweza kusaidiwa na mtu mwingine. Mtu anaweza kumsaidia Rais kumnong'oneza Waziri wake kujiuzulu; lakini hawezi kumsaidia kufukuza Waziri wake. Hiyo ni kazi ya Rais peke yake. Asipoifanya kosa ni lake peke yake.
Rais alikuwa na nafasi kadhaa za kumfukuza au kumshauri Waziri Mkuu kujiuzulu. Kwanza, ni wakati Waziri Mkuu alipomshauri akubali hoja ya Utanganyika. Nilisema awali kwamba Waziri Mkuu huyo huyo huwezi kumshauri Rais wako akubali hoja, ambayo jana tu ulimshauri apinge, na badala ya kujiuzulu uendelee na kazi yako. Lakini pia Rais huyo huyo huwezi kukubali ushauri fulani leo, na kesho ukubali kinyume cha ushauri huo, kutoka kwa Waziri Mkuu huyo huyo, bila kumfukuza au kumtaka ajiuzulu. Hata kama yeye ndiye angekuwa mkuu wako ungepaswa kujiuzulu, badala ya kukubali ushauri wake. Lakini si mkuu wako, ni mshauri wako tu. Kosa la kukushauri vibaya ni lake; lakini kosa la kukubali ushauri wake mbaya badala ya kumfukuza au kumtaka ajiuzulu ni lako. Rais analo kosa hilo.
Rais alipata nafasi ya pili baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa kukataa pendekezo la Serikali la kuitaka ikubali sera ya Serikali Tatu. Azimio la Serikali Tatu lilifanya Bunge la Muungano na Serikali ya Muungano viwe na sera moja na Chama Cha Mapinduzi kiwe na sera nyingine katika suala muhimu kabisa. Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokataa pendekezo la Serikali la kukubali hoja ya Utanganyika, Rais alipaswa kutumia nafasi hiyo kukipa Chama na serikali uongozi mpya wenye msimamo. Rais hakufanya hivyo. Alifanya kosa.
Nafasi ya tatu ni wakati kikao mchanganyiko cha Dodoma kilipokubali kuwa utaratibu wa kutaka kubadili sera ya Chama ulikuwa umekosewa na kikapendekeza lipelekwe kwa wanachama wa CCM. llikuwa ni dhahiri kwamba shughuli hiyo itataka uongozi mpya wa Chama na Serikali. Kama nilivyokwisha kusema, viongozi wahusika walinong'onezwa wajiuzulu, wakagoma; na Rais akashindwa kuwafukuza. Akabaki na washauri wake wale wale. Hili lilikuwa kosa, tena la kushangaza!
Naamini kuwa wanachama wa CCM watakataa pendekezo la Bunge na Serikali la kutaka SerikaIi ya Tanganyika. Hiyo itampa Rais nafasi nyingine tena ya kubadili uongozi wa Chama na Serikali. Asipofanya hivyo atakuwa amepoteza nafasi yake ya mwisho ya kuiondoa nchi hii katika mwelekeo wa hatari; na Nchi yetu itaserereka haraka sana katika njia ya giza na wasi wasi; bila matumaini. ­
Na viongozi hawa wataachwa wamwongoze nani? Katika jambo gani? Na kutupeleke wapi? Watageuka tena wawe watetezi wa Muungano wenye muundo wa Serikali Mbili? Mpaka lini? Mpaka hapo watakapopata ndoto nzuri zaidi au kutuzulia "muafaka" mpya?
Katika haIi ya kawaida, kama Rais kashindwa kubadili uongozi wa Serikali tungetazamia Bunge au Chama kufanya hivyo. Uingereza kwa mfano Wabunge wa Chama kinachotawala walipoona kuwa Mrs Margareth Thatcher alikuwa hafai tena kuendelea kuwaongoza ni wao wenyewe walimwondoa na kuchagua kiongozi mwingine.
Bunge letu ni la chama kimoja; na Katiba ya sasa inawapa Wabunge uwezo wa kuikataa Serikali kwa kupilisha Azimio la kutokuwa na imani nayo. Bunge likifanya hivyo Rais atalazimika kuteua Serikali mpya itakayoomba upya kibali cha Bunge. Lakini wabunge wetu hawatafanya hivyo. Kwa ghiliba za viongozi na hasira za mkizi wamefanywa waonekane kuwa sasa wao wote, pamoja na viongozi wetu, wamekuwa ni mbuya na makomredi wa kushuku Muungano. Badala ya kuwasaidia wananchi wenzao kwa kuishughulikia Serikali yenyewe na ubovu wake, wanataka kuongeza Serikali ya Tatu! Na baadhi yao wangependa kumwimpichi, au kumshtaki Rais Bungeni! Hiyo kwao ni rahisi zaidi kuliko kuidhibiti SerikaIi.
NADHANI akilini mwao Muungano na Ramani ya-Zanzibar; na maadamu "tumechoka na Wazanzibari", basi na waondoke warudi walikotoka, wakifungasha na Muungano wao na Rais wao! Kwa hiyo, kama majuha au mazuge tunaendelea kuimba wimbo wa Serikali tatu, na nchi inazidi kuserereka kuelekea gema la hifaki.
Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; au upole wake na udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu, Kipindi chake cha pili kinakaribia kwisha, kwa Taifa letu jambo muhimu zaidi kwa sasa ni uongozi wa Chama na Serikali, na ni nani atakayechukua nafasi ya Rais baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani.
Kwa sababu ya minong'ono­nong'ono ya watu wasioona mbali kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amaIize kipindi chake salama. Kipindi Cha mpito, cha kujaribu kujenga utaratibu wa kikatiba wa kubadili uongozi wa nchi yetu kwa heshima na amani hakitakamilika mpaka hapo Rais Mwinyi atakapomaliza kipindi chake kilichobaki kwa usalama, na kumkabidhi madaraka Rais mpya kwa utaratibu ule ule uliompa madaraka hayo.
Suala hili la kutaka kuvunja Muungano, watu wanaostahili kuwajibika ni wale waliokuwa na wajibu wa moja kwa moja na ambao kwa makosa yao wamemfikisha Rais katika hali hii ngumu; na kuitumbukiza nchi yetu katika hali ya hofu na wasi wasi.

UHALALI WA SERIKALI
Serikali ya sasa ni halali, kwa maana ya kwamba imeteuliwa na Rais halali, kwa njia halali. Raia ye yote wa Tanzania hawezi kwenda Mahakamani na kudai kuwa Serikali hii ni haramu, kwa maana ya kwamba haikuteuliwa kisheria. Pamoja na kwamba Waziri Mkuu hakuteuliwa kwa kufuata utaratibu unaotakiwa na Katiba ya sasa, kuteuliwa kwake nje ya utaratibu huo kulihalalishwa na Bunge. Kwa hiyo, nasema, Serikali hii ni halali. Lakini ni halali kwa maana hiyo tu. Ni uhalali wa sheria bila uhalali wa uwezo na mwenendo na vitendo.

Kwa maana moja sasa hatuna Serikali, tuna Mawaziri tu. Serikali ni timu; na timu halisi ina dira na rubani. Mkusanyiko wa Mawaziri bila­ mwelekeo, bila mwongozo, bila mshikamano na bila uongozi, kila Waziri na lwake, hauwezi ukaitwa Serikali. Katika hali kama hiyo, hata hila ubovu mwingine wa nyongeza, mambo muhimu ya nchi hayawezi kujadiliwa wala kushughulikiwa. Lakini hata kama Serikali yetu ingekuwa na umoja na mshikamano wa kuiwezesha kushughulikia masuala mengine muhimu ya Nchi yetu, kwa kukubali hoja ya kuwa na Serikali ya Tanganyika, ingekuwa imejiondolea uwezo na uhalali wa kushughulikia na masuala ya Muungano wenye Katiba ya sasa ya muundo wa Serikali mbili.

REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)

No comments:

Post a Comment