Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 25 September 2014

KATIBA MPYA YAMPA RAIS MADARAKA ZAIDI


Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba, imeongeza madaraka ya Rais maradufu na kuondoa matakwa ya rais kuzingatia masharti ya uthibitisho wa Bunge katika nafasi za madaraka na kumuachia uteuzi wa moja kwa moja.

Akiwasilisha rasimu hiyo bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, aliyataja mambo mbalimbali yaliyofutwa, yaliyoongezwa na yaliyoboreshwa katika Rasimu ya Jaji Warioba.

Kwa mujibu wa Rasimu iliyotolewa Desemba 31, 2013 na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, ilipendekeza nafasi zote za uteuzi kupendekezwa na mabaraza ya kisekta kabla ya Rais kufanya uteuzi miongoni mwa majina hayo kisha kuthibitishwa na Bunge Ibara ya 73 (3)

ya Rasimu ya Warioba imependekeza kuwa Katika utekelezaji wa madaraka kama ilivyoainishwa katika ibara ndogo ya (1) na (2), Rais atazingatia masharti kuhusu uthibitisho wa Bunge katika nafasi za madaraka na vile vile ushauri wa mamlaka za Serikali, Bunge au Mahakama zilizopewa madaraka ya kumshauri katika kufanya uteuzi, kuanzisha au kufuta nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali.

 Aidha, ibara ya 74 (1) ya Rasimu ya Warioba ilipendekeza kuwa mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii,  na sheria za nchi, Rais atakuwa na wajibu wa kufuata na kuzingatia ushauri atakaopewa na mamlaka za nchi, na endapo hakubaliani na ushauri aliopewa, sharti atoe sababu katika Baraza la Mawaziri kuhusu sababu ya kutokubaliana na ushauri aliopewa.

Nafasi pekee ya uongozi ambayo baada ya uteuzi wa Rais itapaswa kuthibitishwa na Bunge ni ya Waziri Mkuu, wakati Rasimu ya Pili ya Jaji Warioba mbali na Waziri Mkuu,  ilipendekeza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Jaji Mkuu, na Mkurugenzi na Mashtaka kuthibitishwa na Bunge.

Nafasi za uteuzi ambazo hazitathibitishwa na Bunge ni Mawaziri, Manaibu Waziri, Katibu wa Bunge, Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi wa Mashtaka, Katibu Mkuu Kiongozi, Wakuu wa mikoa wa Bara.

MAHAKAMA
Rasimu hiyo imependekeza Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Juu, Naibu Jaji Mkuu, Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufani, Makamu Mwenyekiti, ambao watateuliwa na Rais kutoka majina matatu yaliyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama atateuliwa kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mtendaji Mkuu wa Mahakama atateuliwa kutoka majina matatu ya watumishi wa umma yaliyopendekezwa na Tume.

TUME YA HURU YA UCHAGUZI
Rasimu hiyo imependekeza Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wengine saba watakaoteuliwa na rais baada ya kupendekezwa na kamati ya uteuzi.
 Aidha, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa umma.

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
Rasimu hiyo imependekeza Msajili wa Vyama vya Siasa na Naibu Msajili,  watateuliwa na rais kutoka majina matatu yaliyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.

TUME YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Imependekeza Mwenyekiti, Makamu na wajumbe wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wateuliwe na rais kutoka majina yaliyopendekezwa na Tume ya uteuzi

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Rasimu hiyo imependekeza Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watateuliwa na Rais kutoka majina yaliyopendekezwa na Tume ya uteuzi.

CAG
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), atateuliwa na Rais kutoka majina matatu yaliyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, watateuliwa na Rais.

RASIMU YA JAJI WARIOBA ILIPENDEKEZAJE?
Rasimu ya Jaji Warioba ilipendekeza Mawaziri, Naibu Mawaziri, Mwanasheria Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu, Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe saba wa Tume Huru ya Uchaguzi, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji.

Wengine ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, CAG.Ambao watateuliwa na Rais na kutothibitishwa na Bunge bali kushauriana na Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

IBARA ZILIZOFUTWA
Kamati ya Uandishi BMK imewasilisha bungeni Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ambayo imefuta Ibara 28 zilizokuwemo kwenye Rasimu ya Pili iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku ikizifanyia marekebisho Ibara 186 na kuingiza Ibara mpya 41.

Chenge alisema kufutwa kwa ibara hizo pamoja na marekebisho yaliyofanyika kwenye ibara nyingine kunatokana na michango ya idadi kubwa ya wabunge wa BMK wakati wa mijadala ya kwenye kamati na ndani ya Bunge na kutokana na sababu maalum kuna maeneo ambayo maoni ya wachache yamezingatiwa.

“Rasimu hii inazo Ibara 274, kati yake ibara 233 zinatokana na rasimu iliyowasilishwa kwenye bunge hili na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ibara 186 zimefanyiwa marekebisho ya kiuandishi na kimaudhui, ibara 47 hazijafanyiwa marekebisho yoyote, lakini pia ibara 28 zimefutwa na tumeingiza ibara mpya 41,” alisema Chenge.

Rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba ilikuwa na sura 17 zenye ibara 271.
 Katika Rasimu iliyowasilishwa jana bungeni na Chenge kuna sura 19 zenye ibara 274, hivyo kuwepo kwa ongezeko la sura mbili na ibara tatu ikilinganishwa na Rasimu ya Jaji Warioba.

MAMBO MAPYA
 Kwa Mujibu wa Chenge miongoni mwa mambo makubwa yaliyoongezwa katika Sura ya Kwanza, Ibara ya Sita inayozungumzia misingi ya utawala bora jambo ambalo halikuwemo kwenye Rasimu ya Jaji Warioba.

Katika Sura ya Pili kwenye Ibara ya 16 yamewekwa masuala yanayohusu utafiti na maendeleo na katika ibara ya 17 kuna Dira ya Maendeleo na Ibara ya 18 inazungumzia Tume ya Mipango ya Jamhuri ya Muungano na matumizi ya masharti ya sura ya pili yakiwa katika ibara ya 20.

Sura ya Tatu ibara ya 22 inayohusu ardhi huku matumizi bora ya ardhi yakizaa ibara ya 23 huku mwanamke akipewa haki ya kumiliki na kutumia ardhi kama ilivyokuwa kwa mwanaume.
Aidha katika sura ya nne, imeongezwa ibara inayozungumzia utaratibu wa utwaaji wa mali ya umma iliyotwaliwa na kiongozi aliyefanya ubadhirifu.

MAMBO YALIYOFUTWA
Chenge aliyataja mambo ambayo yamefutwa kutoka kwenye Rasimu ya Jaji Warioba kuwa ni Muundo wa Muungano wa Serikali tatu uliokuwa katika Sura ya sita ambao umebadilishwa na kuependekezwa kuendelea na Muundo wa Serikali mbili na nchi moja.

Mambo mengine ni ukomo wa ubunge, wananchi kupewa mamlaka ya kumwajibisha mbunge na Mawaziri kutokuwa wabunge.

Kwa mujibu wa Rasimu inayopendekezwa, nafasi ya ubunge haitakuwa na ukomo wa kugombea, wananchi watamwajibisha mbunge kupitia uchaguzi baada ya mbunge kumaliza kipindi chake cha uongozi cha miaka mitano na mawaziri wataendelea kupatikana miongoni mwa wabunge.

YALIYOFANYIWA MAREKEBISHO
Baadhi ya mambo ambayo yamefanyiwa marekebisho ikilinganishwa na yalivyokuwa katika Rasimu ya Jaji Warioba ni Tunu za Taifa ambazo zimepunguzwa kutoka saba na kubakia nne.

Tunu zilizowekwa kwenye Rasimu mpya ni Lugha ya Kiswahili, Muungano, utu na undugu pamoja na amani na utulivu.

Katika Rasimu ya Jaji Warioba Tunu zilizopendekezwa zilikuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa.

Chenge alisema marekebisho mengine yaliyoingizwa katika Rasimu ya Katiba ni kuongezeka kwa haki za wanawake, vijana, watoto, watu wenye ulemavu, wazee na haki za wasanii.

Marekebisho mengine yapo kwenye sura ya sita inayohusu uraia, ambapo watanzania wenye uraia wa nchi nyingine hawatakuwa na uraia wa nchi mbili,  isipokuwa watapewa hadhi maalum ya watu wenye asili au nasaba ya Tanzania, tofauti na mapendekezo ya Rasimu ya Jaji Warioba iliyopendekeza watu wa aina hiyo watakapokuwa ndani Jamhuri ya Muungano watakuwa na hadhi kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.

Katika sura ya nane ya Rasimu inayopendekezwa na BMK, Rais wa Zanzibar atakuwa makamu wa pili wa Rais na Waziri Mkuu atakuwa Makamu wa tatu wa Rais huku ikitamka kwamba makamu wa kwanza wa Rais ni Mgombea Mwenza wa Rais wakati wa uchaguzi.

Aidha katika sura hiyo ya nane, Rasimu imependekeza idadi ya mawaziri kuwa 30 na Naibu Mawaziri kuteuliwa kutegemeana na mahitaji ya Serikali.

Katika Rasimu ya Jaji Warioba ambayo ililenga Muundo wa Serikali tatu, ilipendekezwa idadi ya Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano na Naibu Mawaziri haitazidi 15.

Marekebisho mengine yaliyofanywa kwenye Rasimu inayopendekezwa na BMK ni suala la Mgombea huru ambalo katika rasimu hiyo limewekewa masharti maalum, ikiwa ni pamoja na idadi ya wapiga kura wanaohitajika kumdhamini kwa ngazi ya nafasi anayogomea, kipindi ambacho amekoma kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa kabla ya siku ya uchaguzi, kutojiunga na chama chochote cha siasa katika kipindi ambacho atakuwa kiongozi baada ya kuchaguliwa, utaratibu wa kuainisha vyanzo vya ndani na nje vya mapato vya kugharimia kampeni za uchaguzi, utaratibu wa kuainisha vigezo na sifa zitakazotumiwa kuwapata viongozi wa ngazi za juu kitaifa na kuweka wazi ilani ya uchaguzi inayoonyesha mipango ya uendeshaji wa nchi.

Katika Rasimu ya Jaji Warioba, mgombea huru hakuwekewa mashariti zaidi ya kuwa na sifa za ujumla zinazomruhusu kugombea kwa mujibu wa katiba.

Kwa mujibu wa Chenge, marekebisho mengine ni idadi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao wameongezeka kutoka 75 waliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba hadi kufikia wabunge 360.

Katika Rasimu ya Pili ya Jaji Warioba ilipendekezwa wabunge 70  wa kuchaguliwa kupitia majimbo ya uchaguzi, kati yao 50 kutoka Tanganyika na 20 kutoka Zanziba, huku pia ikipendekeza kuwepo kwa wabunge watano wenye ulemavu watakaoteuliwa na Rais.

Marekebisho mengine yaliyoingizwa kwenye Rasimu inayopendekezwa na BMK ni sifa ya mtu anayestahili kugombea nafasi za kisiasa kama vile udiwani, ubunge na urais.

Katika Rasimu ya Jaji Warioba ilipendekezwa kuwa mtu mwenye sifa ya kugombea nafasi ya Ubunge ni lazima awe na elimu ya kidato cha nne, lakini katika Rasimu inayopendekezwa na BMK sifa hiyo imeondolewa na badala yake mtu anayegombea anapaswa kujua kusoma na kuandika.

YALIYOFUTWA, KUBORESHWA MUUNDO WA MUUNGANO
Ibara ya kwanza inayozungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge Maalum la Katiba limefuta mapendekezo ya rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kufuta Muungano wa serikali tatu na badala yake imependekeza serikali mbili kama ilivyo kwenye Katiba ya mwaka 1977.

 Katika Ibara 1 (i), Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.

Hata hivyo, Kamati ya Uandishi imefuta neno 'Shirikisho' kwenye ibara hiyo kwa maelezo kuwa wajumbe wengi wamependekeza Muungano wa serikali mbili.

Mapendekezo ya Kamati hiyo yanasema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili,1964 zilikuwa nchi huru.

Aidha, katika kifungu kidogo cha pili cha Ibara hiyo, Tume ilipendekeza kuwa Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu; hata hivyo, kamati ya uandishi imefuta neno 'kujitegemea' kwa madai kuwa linaleta kasoro ya mtiririko.

“Kwa msingi huo, Kamati ya Uandishi imeiandika upya Ibara hii kama inavyosomeka kwenye Ibara ya 1 ya Rasimu hii ya Katiba inayopendekezwa. Neno hilo (shirikisho), lilifutwa kwa kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Wajumbe walio wengi ndani ya Kamati zote kumi na mbili za Bunge Maalum yalilenga kuwepo kwa Muundo wa Serikali Mbili," alisema Chenge.

Kadhalika, Kamati ya Uandishi imeongeza ibara ndogo mpya ya (3) kwa kutoa mamlaka kwa Bunge kutunga sheria itakayoainisha na kufafanua mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kamati hiyo pia imeongeza sikukuu za taifa kwa kuongeza maadhimisho ya kitaifa katika Ibara ya tatu ya rasimu.

“Katika Ibara hii, Kamati sita kati ya Kamati Kumi na mbili zilipendekeza kufanya marekebisho kwenye Ibara ya (3)(1) kwa kuongeza aya mpya ya (d) kwa ajili ya kuongeza maneno na maadhimisho ili mbali na Sikukuu za Taifa zilizoainishwa katika Ibara hii, kuwapo pia na maadhimisho mengine ya kitaifa."

 Bunge Maalum pia limefuta Ibara ya tano ya rasimu ya Katiba iliyokuwa inazungumzia Tunu za Taifa kwa madai kuwa mambo yaliyotajwa kuwa Tunu ni msingi wa utawala bora.
 Katika Ibara hiyo, Tume ilipendekeza kuwa Jamhuri ya Muungano itaenzi Tunu saba ambazo ni (a) utu, (b) uzalendo (c) uadilifu, (d) umoja, (e) uwazi, (f) uwajibikaji na (g) lugha ya Taifa.

 Badala yake, Kamati ya Uandishi imesema: “Kuwa Tunu na misingi ya utawala bora ni mambo mawili tofauti, Kamati inapendekeza kuifuta Ibara ya 5 na kuiandika upya.”
Baada ya kufuta, Kamati hiyo imependekeza Tunu ziwe ni (a) amani na utulivu, (b) haki na usawa wa binadamu, (c) usawa wa jinsia na (d) Lugha ya Kiswahili.

 Kamati imeongeza Ibara ya 6 inayoeleza misingi ya utawala bora ambayo ni (a) uadilifu; (b) demokrasia; (c) uwajibikaji;(d) utawala wa sheria; (e) ushirikishwaji wa wananchi; (f) haki za binadamu; (g) usawa wa jinsia; (h) umoja wa kitaifa; (i) uwazi; na (j) uzalendo.

 Hata hivyo, Chenge alisema baadhi ya Ibara za Rasimu za Katiba zimebaki kama zilivyo kwa kuwa maudhui yake yanajitosheleza na nyingine zimefutwa kwa kuwa  maudhui yake yamezingatiwa katika Ibara nyingine.
 Sababu nyingine ya kufuta ni kwa kuwa maudhui yake yamebebwa katika mapendekezo mengine; maudhui yake yanapaswa kuzingatiwa katika sheria za nchi; maudhui ya Ibara nyingine yamehamishiwa kwenye Ibara nyingine ili kuweka pamoja maudhui yanayofanana; na maudhui mengine yamegawanywa katika Ibara ndogo tofauti kwa lengo la kuyaweka wazi zaidi.

MAADILI NA MIIKO YA VIONGOZI WA UMMA
Katika rasimu ya Tume, Ibara ya 14 (i) (a), (b) na (c), pamoja na mambo mengine, ilipendekeza kuwa kiongozi wa umma atatakiwa kulinda hadhi ya ofisi yake na kuhakikisha hatosababisha mgongano wa maslahi ya umma na binafsi; lakini Kamati ya uandishi imefuta na kupendekeza sharti hilo lijumuishwe kwenye sheria.

 Kamati hiyo inapendekeza kufuta na kuiandika upya Ibara hiyo ili kubainisha miiko ya msingi katika uongozi wa umma na kuacha mambo mengine ya kiutendaji yazingatiwe katika Sheria itakayotungwa na Bunge.

 “Sababu ya mapendekezo haya ni kuwa, maudhui ya Ibara hii ya Rasimu ya Tume, yanaelezea mambo mengi yakiutendaji na kiutawala ambayo ni muhimu yakaainishwa katika Sheria zitakazotungwa na Bunge ili kurahisisha utekelezaji pindi kunapotokea mabadiliko."

“Lengo la maboresho ni kuhamishia masuala haya kwenye sheria za nchi kutokana na ukweli kwamba yanabadilika mara kwa mara kutokana na wakati.”
Bunge Maalum pia limeongeza sura mbili mpya ambazo hazikuwamo katika rasimu ya Tume ambazo ni ile inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira na Sura inayohusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Aidha, Sura ya Pili ilikuwa na sehemu moja sasa inapendekezwa kuwa na sehemu tano na pia Ibara nyingine mpya zimependekezwa katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Kamati hiyo imeeleza sababu za kuridhia kuongeza sura hiyo ni umuhimu wa ardhi, maliasili na mazingira katika maendeleo ya nchi kwa kuwa ni vitu vinavyogusa maisha ya kila siku ya Watanzania wengi wakiwamo wafugaji, wakulima, wavuvi na wachimbaji wa madini. Alisema lengo ni kuhakikisha raia wa Tanzania pekee ndiyo wenye haki ya kumiliki ardhi.

SIFA YA KUGOMBEA UBUNGE
Sifa ya elimu kwa mtu anayegombea ubunge imependekezwa kuwa awe anajua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.Pendekezo hilo linafuta sharti la awali la kuwa na elimu ya kidato cha nne, lililopendekezwa na rasimu ya katiba iliyowasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba na aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Pendekezo la kufuta sharti hilo lililomo kwenye ibara ya 117 (1) (b) lilitolewa na Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo kupitia Mwenyekiti wake, Andrew Chenge, bungeni jana.

Chenge, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, alisema pendekezo hilo limetolewa na kamati yake ili kutoa fursa kwa watu wenye uwezo wa kugombea wafanye hivyo, ikiwa ni pamoja na kuondoa dhana ya uwapo wa nchi washirika na kulifuta neno hilo kila linapojitokeza ili kuendana na mfumo wa serikali mbili unaopendekezwa kwa sasa.


Pia alisema kamati imeridhia pendekezo la kuwapo mgombea huru katika nafasi ya ubunge na kwamba, pendekezo la kumzuia mtu mwenye madaraka kugombea nafasi hiyo, limezingatiwa na kamati kwa kufuta sharti hilo, ili lizingatiwe katika ibara nyingine.

Alisema kamati saba za Bunge hilo zimependekeza aya ya (d) ya ibara ndogo ya (1) ifutwe na kamati tano zimependekeza Ibara hiyo ifanyiwe marekebisho madogo, yakiwamo kuongeza ibara ndogo ya (1) (g) ili kutoa fursa kwa Rais kutengua uteuzi wa mbunge wa kuteuliwa.

Chenge alisema kamati yake baada ya kupitia mapendekezo hayo, imeongeza aya mpya ya (h) inayoweka sharti la mbunge aliyetokana na mgombea huru kupoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kujiunga na chama chochote cha siasa.

Kuhusu ibara ya 129 inayohusu haki ya wapiga kura kumwajibisha mbunge, alisema  kamati moja imependekeza Ibara hiyo ibaki kama ilivyo kwenye rasimu ya tume, lakini kamati saba zimependekeza ifutwe na kamati nne zimependekeza marekebisho madogo, ikiwamo kuwapo kwa haki ya wapigakura kumwajibisha mbunge, ambaye ameshindwa kuwasilisha au kutetea kero za wapigakura wake.

Alisema kamati yake baada ya kutafakari maoni hayo, inapendekeza ibara hiyo ifutwe kwa kuwa haki inayopendekezwa inaweza kutumika vibaya, ikiwamo kumwekea vikwazo vya kiutendaji mbunge aliyeko madarakani.

Pia wapigakura wanayo haki ya kumwajibisha kwa kutompigia kura mbunge katika kipindi cha miaka mitano endapo wananchi wataona mbunge anayewawakilisha hafai, wanaweza kumwajibisha.

“Kwa kuzingatia mapendekezo hayo Kamati ya Uandishi inapendekeza Ibara hii ifutwe,” alisema Chenge.

IBARA YA 132 KUHUSU SPIKA
Chenge alisema kamati yake imependekeza kuwa ibara hiyo ibaki kama ilivyo kwenye rasimu ya tume kwa kuwa maudhui yake yanajitosheleza.

Hata hivyo, alisema baada ya kuchambua na kuzingatia mapendekezo ya kamati za Bunge na mijadala bungeni, kamati yake imeifuta na kuiandika upya ibara ndogo ya (1) ili kumuwezesha Spika wa Bunge kuchaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge au watu wenye sifa za kuwa wabunge.

Pia alisema kamati yake imekubaliana na pendekezo la kufuta neno “Mbunge” katika ibara ndogo ya (2) ili kumwondoa mbunge katika orodha ya watu wanaokosa sifa za kugombea nafasi ya Spika.

Imeandaliwa na Emmanuel Lengwa, John Ngunge, Jacqueline Massano na Editha Majura, Dodoma na Salome Kitomari, Muhibu Said na Restuta james (Dar).
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment