Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 24 September 2014

HIVI NDIVYO KAMPUNI ZA KIGENI ZINAVYOILIZA TRA


Mshauri wa Kanda wa Taasisi ya Kodi ya Kimataifa, Silas Olang', ameitaka serikali kuifanyia kazi kwa vitendo rai ya kutaka kuwa macho katika mikataba yake na wawekezaji wa kimataifa katika sekta mbalimbali ikiwamo ya nishati na madini, ili kuongeza mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akizungumza katika kongamano la siku tatu jijini Dar es Salaam kujadili haki na wajibu wa ulipaji kodi lililoandaliwa na Action Aid Tanzania (AATZ), Olang', alisema kampuni kubwa zimekuwa na mbinu nyingi za kujiongezea faida na kwamba, serikali isipokuwa makini inaweza kujikuta ikiambulia patupu huku rasilimali za nchi zikiondoshwa kila uchao.


Alitaja baadhi ya mbinu zinazotumiwa na kampuni za uwekezaji za kimataifa kuwa ni pamoja na kuzidisha kiwango cha gharama zao za uwekezaji na uzalishaji; kuwekeza nchini kwa majina ya kampuni tanzu ambazo hulipa ushuru kwa kampuni mama na kuzihesabu kuwa ni sehemu ya gharama zao wakati kimsingi ni faida tupu kwao.

Nyingine ni kuhamisha gharama za uwekezaji kutoka eneo moja la mradi kwenda kwingine; kukwepa kipengele cha kuwapo kwa kodi itokanayo na kupanda kwa thamani ya bidhaa (windfall tax); kukwepa kipengele chenye kodi ya faida itokanayo na kuuzwa kwa kampuni kwenda kwa mmiliki mwingine (capital gain tax) na pia kusajili kampuni zao katika nchi zinazotoa unafuu mkubwa wa kodi kama Mauritius.

“Utatifi umefanyika na kugundua kuwa kampuni kubwa 10 duniani zina matawi takriban 6,038, hivyo kila kampuni kuwa na wastani wa kampuni zake ndogo (subsidiaries) 600 ambazo hufanya biashara zenyewe...” alisema na kuongeza:

"Kwa hiyo, nikitaka kununua, labda mashine, nanunua kwa kampuni dada. Nikitaka mkopo, napata kwa kampuni dada inayoshughulikia fedha.

Zinafanya biashara zenyewe, faida inapelekwa kwa kampuni mama. Kwa mtindo huu, kampuni (tanzu) iliyopo Tanzania inaweza kuonekana ikipata hasara kila mwaka lakini haifungwi kwa sababu mwisho wa siku hukaa mezani pamoja," alisema Olang'.

Aliitaka serikali kuwa makini wakati wa kuingia mikataba na wawekezaji kama wa madini na gesi kwa kuyafanyia kazi maeneo yote yanayochangia kupungua kwa mapato ya nchi kupitia uwekezaji unaofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Meneja wa TRA wa Elimu kwa Mlipakodi, Diana Masalla, alikiri kuwapo kwa changamoto kadhaa za ukusanyaji wa mapato sahihi kwenye miradi ya uwekezaji na ndiyo maana mamlaka yao (TRA) imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo Norad (Shirika la Maendeleo la Norway) ili kujiongezea uwezo na mwishowe kuinua mapato ya nchi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment