Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 2 September 2014

MIAKA MIWILI ILIYOPITA, SIKU KAMA YA LEO, HIVI NDIVYO WALIVYOMUUA DAUDI MWANGOSI




Leo ni miaka miwili tangu mwanahabari Daudi Mwangosi alipouawa kinyama na askari polisi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Nyororo wilayani Mufindi.
Ni tukio la kuhuzunisha kwa sababu lilitendwa katika mazingira ambayo yangeweza kuzuia umwagaji damu, tena mbele ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Tunakumbuka tu kwa majonzi, hatuna cha kusema zaidi kwa sababu kesi iko mahakamani na inasuasua kwa namna ilivyo, tusije tukashangaa tukiambiwa hata mhusika hana hatia.
Hata hivyo, ninainukuu habari hii, ambayo ndiyo iliyotoa taswira halisi na ukweli kuhusu mhusika wa mauaji pamoja na kukiri kwake. Habari hii ilichapwa kwenye gazeti la Kwanza Jamii Iringa, Jumatatu, Septemba 10, 2012 wakati huo mamlaka husika zikiendelea kusema kwamba marehemu Mwangosi aliuawa na wafuasi wa Chadema waliokwenda na bomu wakitokea Mbeya, wengine wakadai eti marehemu alikuwa na bomu kwenye koti lake!
Habari yenyewe hii hapa:

MAUAJI: Wakati inadaiwa kuwa ni bomu la machozi, sasa yadhihirika…

Ni bomu la kivita lilimuua Mwangosi

·        Aliyelifyatua ajutia, ana miaka 23, ni askari wa Iringa
·        Yadai walitumwa kuwakamata viongozi wa Chadema

Na Daniel Mbega

WAKATI ambapo dunia bado imezizima kutokana na kuuawa kwa mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi (40) mkoani Iringa, imeelezwa kwamba bomu la kishindo (kivita) ndilo limekatiza uhai wake.
Habari za awali, ambazo zimesambaa dunia nzima zimekuwa zikieleza kilichomuua ni bomu la machozi, na sasa imegundulika tofauti.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti la Kwanza Jamii Iringa, umebaini kwamba bomu hilo la kishindo lilifyatuliwa na mmoja wa askari kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Iringa, aliyefahamika kwa jina la Pacificus Cleophase Simon (23) mwenye namba G2573.
Taarifa za awali zinasema kwamba, askari huyo anayedaiwa kukiri kuua (kwa bahati mbaya), tayari ameshakula kiapo cha ungamo mbele ya Mlinzi wa Amani na kwamba anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kusomewa mashtaka yake, ingawa hatatakiwa kujibu kwa vile kesi za mauaji zinasikilizwa na Mahakama Kuu.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimebainisha kwamba, askari huyo, kabla ya kuondoka Iringa kwenda Nyololo, Mufindi, alikuwa amepewa mabomu mawili – moja la machozi na jingine la mlipuko – wakiwa wametumwa kuwakamata viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Tulitumwa kuwakamata viongozi wa Chadema, lilikuwa ni agizo, kwa sababu walikuwa wamekaidia amri ya Jeshi la Polisi ya kutoitisha mkutano, tulifanikiwa kuwakamata viongozi watano wa chama hicho,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya jeshi hilo.
Kabla ya kuuawa, Mwangosi alikuwa amezingirwa na askari wanane huku mmoja wao, OCS Mwambapa wa Mafinga, aliyekuwa ameshikiliwa na marehemu kiunoni, akiwataka wasimpige kwa vile ni mwandishi.
Miongoni mwa askari hao, wawili (akiwemo mtuhumiwa) walikuwa na bunduki maalum kwa kufyatulia mabomu, mmoja aliyevaa kiraia alikuwa na bastola wakati wengine walikuwa na virungu.
Inaelezwa kwamba, askari huyo amekiri kwamba alifyatua bomu hilo la mlipuko kwa bahati mbaya baada ya askari mwenzake kuugonga mtutu wake wakati wa purukushani na Mwangosi.
Taarifa za ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa, mtuhumiwa huyo aligundua kwamba alitumia bomu la mlipuko baada ya kurejea kituoni kwake wakati wakikabidhi silaha.
Gazeti hili lilimtafuta Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, ili kuzungumzia suala hilo, lakini msaidizi wake ambaye hakutaka hata kujitambulisha, alisema: “Huwezi kuongea naye kwa sasa, ana kazi nyingi. Kwani wewe una shida gani?”
Hata hivyo, alipotafutwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Robert Manumba, hakuwa tayari kuthibitisha wala kukanusha kuhusu madai hayo.
Kwanza Jamii: Haloo afande DCI, shikamoo na habari za kazi.
DCI Manumba: Nzuri!
KJ: Mimi ni mwanahabari, nataka kujua maelezo yako, kwamba askari aliyehusika kumfyatulia bomu mwandishi Mwangosi ametambuliwa kuwa ni wa Iringa, na kwamba inaelezwa kuwa amekiri kwa ungamo kufanya mauaji hayo akitumia bomu la mlipuko. Unalizungumziaje hili?
DCI Manumba: Jeshi la Polisi halijatoa ripoti yake, tunakamilisha ripoti na itatolewa na mkuu wa jeshi. Kwanza wewe umezipata wapi taarifa hizo?
KJ: Mimi ni mwandishi wa habari za uchunguzi naweza pia kutafuta vyanzo mbalimbali.
DCI Manumba: Basi mpaka tutakapokamilisha uchunguzi ndipo taarifa zitatolewa.
Awali, baadhi ya askari waliokuwepo siku ya tukio walisema mtuhumiwa huyo alikuwa amekamatwa pamoja na askari wengine watano ambao kwa mara ya mwisho walikuwa wamemzingira Mwangosi na kumpiga virungu, kabla mwenzao hajafyatua bomu hilo.
Hata hivyo, taarifa hizo zinadaiwa kukanushwa na Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda, aliyesema hakuwa na taarifa za askari yeyote kushikiliwa na kuhojiwa kwa tukio hilo.
Kudhihirika kwa silaha iliyomuua Mwangosi pamoja na kukiri kwa askari aliyehusika, kumeondoa uvumi wa kupotosha uliokuwa unaenezwa sehemu mbalimbali kwamba, eti bomu hilo lilirushwa na wafuasi wa Chadema huku wengine wakizusha kwamba huenda marehemu alikuwa nalo mfukoni, bila taarifa hizo kueleza lilikotoka.
Mwili wa marehemu Mwangosi ulizikwa Jumanne iliyopita (Septemba 4, 2012) kijijini kwao Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya huku ndugu, waandishi wa habari, wachungaji na wananchi wengine wakililaumu Jeshi la Polisi kwa mauaji hayo, na kwa kushindwa kuwachukulia hatua askari polisi waliosababisha kifo hicho na jina baya la jeshi hilo.

Mashuhuda
Watu mbalimbali walioshuhudia tukio hilo, hususan waandishi wa habari, walisema kwamba, baadhi walijitahidi kumwarifu RPC Kamuhanda aliyekuwa anashuhudia, kwamba aliyekuwa akipigwa virungu na polisi ni mwandishi na kiongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC).
Abdallah Said, mwandishi wa gazeti la Majira jijini Dar es Salaam aliyekuwa eneo la tukio, alisema kwamba alimgongea kioo cha gari alimokuwamo RPC Kamuhanda na kumwarifu kwamba, anayepigwa na mwanahabari, lakini kamanda huyo wa mkoa ‘akampuuza’.
“Nilimgongea kioo akiwa ndani ya gari lake, nikamwambia anayepigwa ni mwandishi wa habari na kiongozi wa wanahabari Iringa, lakini RPC aliteremsha kioo, akanitazama kwa sekunde kadhaa, halafu akapandisha kioo na kusogea karibu ya tukio kabla ya mipuko ule kusikika,” alisema Said.

Tume yapingwa
Pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuunda tume kuchunguza mauaji hayo, lakini tume hiyo imepingwa hadharani kwa maelezo kwamba inaweza isitoe ripoti iliyo sahihi, hivyo kutaka iwepo tume huru zaidi.
Tayari Chadema, kupitia kwa Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, kimesema, tume hiyo ni batili kwa kuwa kwa mujibu Katiba, Dk. Nchimbi hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza mauaji, na kwamba mwenye mamlaka hayo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee.
Nayo Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC) kimesema ni vyema tume hiyo ikamshirikisha mwakilishi wa Umoja wa Klabu za Wanahabari Tanzania (UTPC) kwa vile marehemu alikuwa Mwenyekiti wa IPC.
“Ili kuweka uwiano, pamoja na kuwemo kwa wajumbe kutoka taasisi za habari, ni vyema awepo mwakilishi wa UTPC,” alisema Frank Leonard, Katibu Mtendaji wa IPC.
Tume hiyo inaundwa na wanahabari Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication inayochapisha magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti.
Wengine ni Kanali Wema W. Wapo ambaye ni mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mungulu na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Pivel Ihema.

Matamko mbalimbali
Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zimejitokeza kulaani mauaji hayo ya kinyama ambayo hayakuzingatia haki za binadamu.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Sikika, ambayo imesema: “…Uhai ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania. Hivyo, ni jukumu la polisi kulinda maisha na uhai wa wananchi wote bila kujali itikadi au kazi zao. Hakuna sheria inayohalalisha kujeruhi, kutesa wala kuua mwananchi yeyote kwa sababu tu ati amekataa kutii amri ya polisi. Sikika inasikitishwa zaidi na utamaduni unaozoeleka ndani ya jeshi la polisi kwamba matukio ya kujeruhi, kutesa au  vifo ni halali iwapo wanasiasa au wananchi hawakutii amri...”
Jumuiya ya Wanahabari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza), ilisema: “…Tunasikitika kuona kwamba serikali taratibu inawarudi raia zake, na sasa inaua waandishi wa habari, siku chache tangu alipouliwa kijana mbichi eneo la Msamvu, mjini Morogoro, katika mazingira ambayo pia yenyewe yanatia shaka. Tena ni mwezi mmoja tu tokea serikali, inayojinasibu kuwa inaheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu, ithubutu kutumia sheria mbaya kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usojulikana…”
Jukwaa la Wahariri (TEF), lilisema: “…Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na ufa mkubwa ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili ambazo zinategemeana…”
Tasisi ya Vyombo vya Habari kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (MISA Tan), ilisema: “…Huu ni mwendelezo wa matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi kwa raia wa nchi  hii. Ni lini polisi watasimamia ulinzi wa raia na mali zao badala ya kugeuka kuwa jeshi la mauaji kila wananchi wanapokusanyika kwa minajili ya kutimiza ndoto zao?”
Naye Waziri Mkuu (mstaafu), Frederick Sumaye, amewaleza wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mjini Morogoro mwishoni mwa wiki kwamba serikali, kupitia  Jeshi la Polisi, inapaswa kutumia zaidi busara katika kuzuia maandamano, badala ya silaha na nguvu za ziada za polisi.
Sumaye amesema, kifo cha Mwangosi, pamoja na kusikitika sana, ameshauri kiwe chachu ya kujifunza zaidi kwamba nguvu za ziada kuwakabili watu wasiokuwa na silaha, zinaweza kuleta madhara makubwa badala ya kuponya au kuzuia.

 CHANZO: KWANZAJAMII IRINGA, SEPTEMBA 10, 2012


No comments:

Post a Comment