Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 20 September 2014

KAMA WAMESHINDWA SCOTLAND, MUUNGANO WA TANZANIA HAUVUNJIKI NG'O!

Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume wakibadilishana Hati za Muungano mwaka 1964.
Na Daniel Mbega

Alhamisi ya Septemba 18, 2014 wananchi wa Uskochi (Scotland) wamepiga kura ya ‘HAPANA’ kupinga nchi hiyo kujitoa katika Himaya ya Kifalme ya Uingereza (United Kingdom) na kutaka kuwa taifa huru linalojitegemea.
Hadi kufikia hatua hiyo, kulikuwepo na mivutano mingi ya kisiasa iliyochochewa na wanasiasa ambao walitaka Scotland liwe taifa huru kwa mara ya kwanza
baada ya kudumu kwenye Himaya ya Kifalme ya Uingereza kwa zaidi ya miaka 300.
Katika kura hiyo ya maoni (referendum) wananchi waliosema HAPANA walikuwa 1,914,187 sawa na asilimia 55, wakati waliosema NDIYO walikuwa 1,539,920 sawa na asilimia 45.
Waziri Kiongozi wa Scotland, Alex Salmond kiongozi wa chama cha Scottish National Party, ambaye alikuwa kinara wa kudai mabadiliko hayo ya kujitenga, hatimaye alisema ameridhia kuanguka katika mchakato wa kura ya maoni, huku akikiri kwamba tukio hilo tayari limebadilisha mfumo wa maisha eneo la Scotland.
Idadi kubwa ya wapiga kura walikuwa wamesajiliwa na kwa mara ya kwanza vijana wenye umri wa miaka 16 na 17 waliruhusiwa kupiga kura.
Kimsingi, tukio la kura ya maoni huko Scotland linaleta taswira inayoendana na hali halisi ya mambo yanayoendelea nchini Tanzania, hasa katika mchakato wa Katiba Mpya, japokuwa muundo wa muungano wa Uingereza ni tofauti na ule wa Tanzania.
Bunge la Katiba linaendelea huko Dodoma kuhitimisha majadiliano ya kuichambua Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba.
Ingawa hakuna dalili za kupatikana kwa Katiba mpya mpaka sasa baada ya mvutano wa wajumbe huku wengine wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakisusia vikao tangu Aprili mwaka huu, lakini imedhihirika wazi kwamba kipengele cha muundo wa Muungano ndicho hasa kilichozua nongwa.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo iliongozwa na wasomi, wanasheria na wajuzi wa masuala ya katiba, ilipendekeza – baada ya kukusanya maoni ya wananchi – kwamba muundo huo uwe wa Shirikisho la Serikali Tatu – Tanganyika nayo ikizaliwa upya baada ya kuzikwa tangu Aprili 26, 1964.
Kundi la wajumbe walio wengi, ambalo zaidi limejaza wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) lilipinga vikali muundo huo kwa visingizio vingi ambavyo sina haja ya kuvirudia, lakini ukweli ni kwamba wananusuru migongo yao katika kuulinda Muungano kwa gharama yoyote. Ndiyo maana haikushangaza kwa jinsi walivyokuwa wakitumia lugha za maudhi, kebehi na dharau dhidi ya wale wote waliokuwa wanaunga mkono serikali tatu.
Tume ya Jaji Warioba siyo ya kwanza kuzungumzia Serikali ya Shirikisho, kwani hata Tume ya Jaji mstaafu Franncis Nyalali nayo ilipendekeza hivyo mwaka 1992 lakini Mwalimu Julius Nyerere akasimama kidete kupinga jitihada zozote zilizolenga kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Hofu iliyopo katika muundo wa shirikisho ni kwamba, kwa nadharia utakuwepo, lakini kivitendo utakuwa umekufa na hiyo Zanzibar itakuwa imejitenga na kuwa taifa huru, ndoto ambazo wamekuwa nazo Wazanzibari kwa miaka mingi sasa.
Ikiongezwa na uchu wa madaraka wa wanasiasa ambao sasa wataona kuna fursa nyingi za uongozi, ni dhahiri muundo huo ulikuwa unawasukuma wengi kufanya kila wawezalo – kwa mitazamo yao – kuhakikisha ama zinakuwepo serikali tatu na vyeo viongezeke au zibakie serikali mbili na CCM iendelee kutawala.
Kwa nini? Kwa sababu Tanzania ilizaliwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar – kuanzishwa kwa Tanganyika tena kunaashiria kifo cha CCM ambayo nayo ilizaliwa kwa muungano wa TANU na ASP. Zanzibar ikijitenga maana yake hakutakuwa na haja ya CCM na yawezekana wakataka ama ASP irudi au waanzishe vyama ingine vya siasa.
Upande wa Tanganyika nako kutakuwa hakuna haja ya CCM kwa sababu mantiki yake haitakuwepo. Ama wengine wataifufua TANU kama alivyokuwa amefanya marehemu Joseph Nyerere mwaka 1993 au kitaanzishwa chama kingine tofauti.
Naam. Hata wakati huu ambapo imethibitika rasmi kwamba katiba mpya haitapatikana mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hiyo rasimu yenyewe tu imebakia mifupa mitupu baada ya wajumbe walio wengi kuondoa hata vipengele vyenye maslahi kwa umma.
Lililo dhahiri hapa ni kwamba, ikiwa Scotland, taifa kubwa lenye nguvu kuzidi Tanzania, imeshindwa kujitenga na Uingereza, sembuse Tanzania!
Hapana shaka kwamba suala la kujitenga kwa Zanzibar ama Tanganyika haliwezi kutokea kwa sasa wala kesho. Siwaamulii wajumbe wa Bunge la Katiba, lakini ikumbukwe kwamba baada ya rasimu hiyo kutoka Bungeni, hata kama serikali ya shirikisho itapita, bado inaweza kupingwa kwenye kura ya maoni ya wananchi kama Waskochi walivyofanya!
Ni mtazamo wangu tu.


0656-331974

No comments:

Post a Comment