Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 13 August 2014

TAARIFA YA MAKUSANYO YA DAMU TANGU APRILI - JUNI 2014


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAKUSANYO YA DAMU KWA ROBO MWAKA YA APRILI- JUNI 2014, DAMU SALAMA MAKAO MAKUU
11 AGOSTI 2014
MPANGO wa Taifa wa Damu Salama Tanzania (NBTS) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba mwekundu umekusanya chupa za damu asilimia 91 ya lengo katika kipindi cha miezi mitatu ya April hadi Juni 2014 ambapo jumla ya chupa 38,704 zilikusanywa . lengo lilikuwa kukusanya chupa 42,500. Katika kipindi hicho Mpango wa Taifa wa Damu salama uliweza kuanzisha mfumo wa kielektronic wa kuhifadhi kumbukumbu za wachangia damu kwa kanda ya magharibi Tabora.
Ofisa Uhusiano wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Bw. Rajab Mwenda akizungumza leo Dar es Salaam alisema Katika robo mwaka ya Aprili- Juni 2014 wachangia damu wa kujirudia ni asilimia 9 (3,587) na asilimia 91 ni wachangia damu wa mara ya kwanza (First time donors) hivyo Mpango wa Taifa wa damu salama kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba mwekundu wanajukumu la kuongeza idadi ya wachangia damu wa kujirudia, kwani ndio wachangia damu walio salama.
Bw. Mwenda alisema Tangu kuanza kwa mwaka 2013/2014(October 2013) Jumla ya chupa za damu 121,231 zimekusanywa ambazo ni sawa na asimilia 71 ya lengo la kukusanya chupa 170,000 kwa kipindi cha mwaka Oktoba 2013- Septemba 2014. Hivyo Mpango wa Taifa wa Damu salama kwa kushirikiana na Chama cha msalaba Mwekundu utafanya kazi kwa juhudi katika robo mwaka ya Julai- Septemba ili kuhakikisha unafikia lengo la kukusanya damu asilimia 100.
Damu iliyokusanywa pamoja na mazao ya damu zilisambazwa katika hospitali 238 (72% ya Hospitali zote hapa nchini ) zenye uwezo wa kutoa huduma ya damu.
Katika kipindi cha Aprili-juni 2014 jumla ya wachangia damu 16,183 (42%) walijulishwa majibu yao baada ya kuchangia damu lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 70 ya wachangia damu.
Bw. Mwenda alisema Pamoja na mafanikio ya kuongezeka kwa wachangia damu wa hiari mwaka hadi mwaka kumekuwepo na changamoto mbalimbali . Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na:
Mahitaji makubwa ya damu kuliko upatikanaji,Uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari, Uzwaji wa damu usio halali Hospitalini, tabia inayofanywa na watumishi wasio waaminifu.
Katika hili Bw. Mwenda alikemea tabia ambayo imezuka kwa ndugu za wagonjwa waliolazwa hospitalini kununua damu kwa vijana ambao hupatikana nje ya hospitali , alisema katika gazeti la Nipashe la julai 2014 ilinukuliwa kwamba kuna biashara ya kuuza damu za binadamu kwa nia ya kujipatia kipato ambapo ndugu na jamaa za wagonjwa wanaolala hospitali hulazimika kununua damu kwa waendesha bodaboda au madereva taksi, hii ni tabia ambayo haikubaliki na sio salama kwa sababu mtu anashinikizwa kuchangia damu ili apate kipato hivyo anaweza hatarisha afya ya mgonjwa na pia yeye mwenyewe.
Alisema mtu yoyote mwanamke au mwanaume anaweza kuchangia damu kama akiwa na afya njema, mwanamke anaweza kuchangia kila baada ya miezi minne na mwanaume kila baada ya miezi mitatu, kwa kuchangia damu ili mtu apate kipato haya yote hayazingatiwi.
Bw. Mwenda alisema Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Chama cha Msalaba mwekunde wameweka mikakati ifuatayo ili kufikia malengo kwa kipindi cha Julai- septemba 2014
Kundelea kushirikiana na Taasisi za dini katika kutoa elimu na kuhamasisha waumini wachangie damu, tarehe 31/8/2014 taasisi ya kiislam Akhla islam kwa kushirikiana na Damu salama wataendesha zoezi la kuchangia damu nchi nzima, pia Mpango umefanya maongezi na kanisa la KKKT kuhusu uwezekano wa waumini kuwa wanachangia damu siku ya matendo ya huruma aprili na wakati wa kuelekea siku kuu ya krismasi kila mwaka na pia tutawasiliana na Kanisa la Roman kuhusu kuweka utaratibu kuelimisha na kuchangisha waumini wa dhehebu hilo
Kuongeza vituo vidogo vya kuchangia damu- “Blood collection satellite sites” katika sehemu mbalimbali za nchi. Kwa sasa Mpango kwa kushirikiana na Hopsitali ya mkoa wa kigoma unatarajia kufungua kituo kidogo cha kukusanya damu ambacho kitakuwa na na uwezo wa kukusanya chupa za damu 18000 kwa mwaka
Kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Puplic private partnership (PPP) kuhakikisha Mpango unafikia malengo ya kukusanya chupa za kutosha za damu. Mwaka huu katika mechi ya hisani septemba 13, 2014 Mpango wa Taifa wa Damu salama utashirikiana na Chama cha mpira wa miguu nchini TFF kutoa elimu na kuendesha zoezi la kuchangia damu nje ya Uwanja wa Taifa siku ya mechi ya ngao ya Hisani kati ya Yanga na Azam
Kushirikiana na uongozi wa mkoa kupitia mganga mkuu wa mkoa ili wilaya zitenge bajeti ya kukusanya damu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa damu salama
Kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii (nje ya shule na vyuo) umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari
Kuendeleza utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya simu kwa wachangia damu. Ujumbe huo utakuwa wa kuhamasisha, kumkumbusha mchangiaji siku ya kuchangia tena damu n.k
Bw. Mwenda alitumia fursa ya kikao kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya homa ya Ini kwani katika damu iliyokusanya maambukizi ya homa ya Ini yameonekana kuwa juu 5.6% ikilinganishwa na HIV 1.6%
Pia aliwaomba wananchi wote wenye sifa za kuchangia damu mahali popote walipo nchini kujitokeza katika vituo vya Mpango wa Taifa wa Damu Salama au hospitali zilizo karibu wachangie damu, Tanzania haiwezi kufikia Malengo ya milenia namba 4 na 5 bila ya kuwa na akiba ya damu ya kutosha ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

No comments:

Post a Comment